Kliniki migogoro ya ardhi yatatua 29

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, wakiwa katika kliniki ya kusikiliza kero za wananchi hususani masuala ya migogoro ya ardh. Picha na Happiness Tesha

Muktasari:

  • Migogoro mingi inatokana na wananchi kuuzia kiwanja ndani ya kiwanja, mmoja anakuwa na ofa mwingine hana.

Kigoma. Kliniki ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji iliyoanzishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli imezaa matunda baada ya kufanikisha utatuzi wa migogoro 29 ya ardhi.

 Akizungumza leo Jumatatu Machi4, 2024 katika kliniki hiyo, Kalli amesema karibu asilimia 90 ya malalamiko yanayotolewa na wananchi yanahusu migogoro ya ardhi.

Ametumia nafasi hiyo kuwaonya watumishi wa Serikali akiwataka waepuke kuwa kikwazo kwa wananchi katika upataji wa haki zao.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kero ya mgogoro wa ardhi imekuwa ikitajwa kila anaposikiliza kero za wananchi katika maeneo mengi ya wilaya hiyo.

Hivyo, amesema atahakikisha anasikiliza kero hizo hatua kwa hatua na kuzipatia ufumbuzi, lengo likiwa ni kila mwananchi apate haki yake.

“Popote mnapotaka kujenga huduma za kijamii au kuwekeza, iwe ni mtu binafsi au taasisi, hakikisheni mmekubaliana na mtu mwenye eneo lake, kwa sababu kinachoonekana hapa hakuna mawasiliano mazuri baina ya pande mbili, haiwezekani tukawa na hati mbili kwenye eneo moja,”amesema Kalli.

Wakizungumzia baadhi ya migogoro hiyo, wananchi wanasema ipo kwa miaka mingi lakini inakosa ufumbuzi wa moja kwa moja.

Athuman Yusuph, mjini Kigoma, amesema ameishi katika eneo hilo kwa miaka 17 akimiliki mashamba ambayo amepanda michikichi, miti ya miembe na amechimba visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Lakini Oktoba 10, 2023 kuna watu ambao hawafahamu walifika na kuvamia shamba lake wakidai eneo hilo ni lao na wanataka kulichukua kwa kuwa ni wamiliki halali.

Jambo hili amesema hakukubaliana nao na akaamua kufikisha mgogoro huo kwa mkuu wa wilaya kwa ufumbuzi zaidi.

Naye Miriam James amesema shamba lake lina mgogoro kwa kipindi kirefu na amekuwa akienda kwa kamishna wa ardhi kila mara lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kumaliza kero hiyo.

“Na ninachoshangaa, watu nisiowajua ndiyo wanadai eti eneo hili ni la kwao wanalimiliki kihalali wakati mimi nina hati yangu kabisa,” amesimulia James.

 “Mimi ndiye mmiliki halali na nina hati, kila siku naenda kwa kamishna wa ardhi ninamwambia wewe ndiye ulinipatia mimi hati halali ya eneo langu, iweje mtu mwingine aje aseme ni eneo lake, naomba tu leo mnisaidie kunipa majibu kama serikali,” alisema.

Ofisa Ardhi Mwandamizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Zabron Magesa amekiri uwepo wa migogoro ya ardhi isiyoisha na kutaja sababu ni ukosefu wa elimu kwa baadhi ya wananchi.

Amesema licha ya baadhi ya kesi kuamuliwa na mahakama, lakini bado zimeendelea kuleta mgongano.

“Migogoro mingi ni wananchi kuuzia kiwanja ndani ya kiwanja na mmoja anakuwa na ofa mwingine hana, alafu baadaye anakuja kudai haki, sasa unapataje haki wakati kiwanja kimeuzwa kwa zaidi ya mtu mmoja?” amehoji Magesa.