Sita mbaroni Bagamoyo kwa amri ya DC

Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kidogozero na Ruvu Darajani wakisindikizwa na Polisi baada ya kukamatwa kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya uchochezi wa migogoro ya ardhi

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Halima Okash amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vya Ruvu Darajani na Kidogozero, Kata ya Vigwaza kusikiliza kero zao huku akiagiza wananchi sita kukamatwa kwa tuhuma za kuchochea migogoro ya ardhi.

Bagamoyo. Watu sita wamekamatwa na Polisi wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Okash wakidaiwa kuchochea migogoro ya ardhi.

Watu hao wamekamatwa jana, Alhamisi Januari 11, 2024 wakati wa mkutano kati ya mkuu huyo wa wilaya (DC) na wananchi wa vijiji vya Ruvu Darajani na Kidogozero, Kata ya Vigwaza uliokuwa na lengo la kusikiliza changamoto na kuziwekea mikakati ya kuzitatua.

Amesema amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa watu hao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya uchochezi wa migogoro katika vijiji hivyo kwa njia mbalimbali ikiwemo kuandika barua za kuchafua Serikali na kughushi saini za wanakijiji na kuziambatanisha katika barua bila wao kujua na kisha kuzisambaza maeneo mbalimbali

"…nimewakamata wachochezi wa migogoro ya ardhi, wanagushi nyaraka, wanawashawishi wanachi waikatae Serikali na pia wanaandika barua za malalamiko wakidai zimeandikwa kwemye mikutano halali na kupeleka kwenye uongozi wa juu, wakati si kweli.

"Nilijua wananchi wa vijiji hivi wote mko pamoja, kumbe hamko pamoja wengine wana nia ya kuchochea migogoro ya ardhi kwa maslahi yao binafsi, sasa tutawasaka na kuwafikisha mahakamani na wananchi tutakapowaita mahakamani msisite kuja kutoa ushahidi," amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ofisi yake imekuwa ikipata mihtasari ya mikutano ya kijiji hicho kila ifikapo tarehe nne ya mwezi kuhusu vikao vya vijiji na namna utaratibu wa uuzaji wa ardhi unavyofanyika, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai hawashirikishwi jambo alilobaini halina ukweli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Piusi Lutumo akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Januari 12, 2024 amesema kama mkuu wa wilaya ameamuru hivyo haina tatizo, kwani ana mamlaka kamili kwenye eneo lake la kazi.

"Kama ameamuru hivyo hajafanya tofauti kwa kuwa ana mamlaka kamili na huenda hilo suala linagusa maslahi na hisia kwa wananchi hivyo hilo halina tatizo," amesema.

Mwisho