DC Mtwara aingilia kati mgogoro wa ardhi na wananchi

Baadhi ya wananchi wa kata ya Likombe mtaa wa Mtepwezi wakiwa katika kikao na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya (hayupo pichani). Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
Serikali ya wilaya ya Mtwara imemwagiza Kamishna wa Ardhi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kupima eneo la uwekezaji la Mtepwezi lililopo katika Manispaa hiyo kwakutumia GPS ili kuondoa sinofahamu ya mipaka katika eneo hilo.
Mtwara. Serikali ya wilaya ya Mtwara imemwagiza Kamishna wa Ardhi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kupima eneo la uwekezaji la Mtepwezi lililopo katika manispaa hiyo kwa kutumia GPS.
Upimaji huo unafanywa ili kuhuisha uthamini wa ardhi ambayo ilipimwa mwaka 2016, hatua ambayo itasaidia kuondoa sintofahamu kwa wamiliki wa maeneo hayo ambao wamekuwa na mgogoro kwa muda mrefu.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Likombe mtaa wa Mtepwezi, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya amesema kuwa wataalamu hao wanapaswa kuja na vipimo sahihi ili kujua mipaka ya kila mmoja.
“Wapo wananchi wanasema hawajalipwa, wengine wanasema kuwa wameonewa, hali ambayo imenisukuma kutoa maagizo ili kumaliza mgogoro katika eneo hilo ambalo limetengwa kwaajili ya uwekezaji.
“Nataka kila mmoja ajue eneo lake, ajue ukubwa wa eneo lake, nipate majina yote kwa kila block na baada ya kuhuisha uthamini uendane na wakati wa sasa ili wananchi walipwe kabla ya mwezi wa kumi mbili.
“Uwekezaji tunautaka, mwekezaji ameshalipa eneo hili anaitwa Alistea na utaratibu unafanyika na ameishaingia mkataba, kama kuna mwekezaji mwingine aje tutampa utaratibu. Hakuna mtu mwenye nia ya kuvuruga uwekezaji zaidi ya kufuata utaratibu ni muhimu kila mtu kupata haki yake kwa mujibu wa sheria” alisema Kyobya.
“Hawa wananchi walipwe mapema kila mmoja alipo mapema lakini wapo waliorudishiwa viwanja vya na wapo ambao hawajui maeneo yao vizuiri ya pimwe kwa GPS waliolipwa sawa ambao hawajalipwa tutahakikisha wanalipwa,” amesema.
Nae Seif Akaliwaza, mkazi wa Mtepwezi amesema kuwa wapo watu wajanja wanafika katika maeneo ya watu wengine na kupiga picha.
“Katika mgogoro huu wapo watu wanaingia kwenye eneo lisilo la kwetu letu wanajifanya kuwa ni la kwao hii inaweza kuleta mgogoro zaidi naomba tulipwe ili kupunguza maneno na migogoro” amesema Akaliwaza.