Korti yaamuru katekista kunyongwa

Muktasari:
- Mwalimu huyo ametiwa hatiani kwa mauaji ya mtumishi wa kanisa lililoko Makambako, mkoani Njombe.
Njombe. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa katika kikao kilichoketi mkoani Njombe imemuhukumu kunyongwa hadi kufa mshtakiwa Daniel Mwelango baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya Nickson Myamba.
Mwelango (42), ambaye ni katekista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makambako mkoani Njombe ametiwa hatia kwa mauaji ya Myamba (43), aliyekuwa mtumishi wa kanisa hilo Kigango cha Makambako.
Akisoma hukumu leo Desemba 12,2023, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Said Kalunde amesema mshtakiwa alitekeleza mauaji hayo Februari 8, 2022 katika Mtaa wa Bwawani kwenye duka la kanisa hilo.
Amesema siku ya tukio mshtakiwa alifanya maandalizi kwa kuandaa panga, chuma na mifuko minne, miwili kwa ajili ya kuzuia damu isisambae na miwili kwa ajili ya kuhifadhi mwili wa marehemu.
Amesema mshtakiwa alimpiga Myamba kwa chuma kisogoni na alipoanguka chini na kubaini amefariki dunia alimkata vipande viwili na kuvihifadhi kwenye mifuko ili iwe rahisi kubeba mwili huo na kwenda kuutupa mbali.
"Baada ya kuona mke wa marehemu anapiga simu mara kwa mara kwenye simu ya Myamba pamoja na mwenyekiti wa kigango, alishindwa kuubeba mwili huo na kuamua kuondoka, huku akiwa amebeba panga na kwenda kulitumbukiza kwenye shimo la choo cha Shule ya Msingi Makambako," amesema Jaji Kalunde, akirejea ushahidi uliotolewa mahakamani.
Amesema chuma alichotumia mshtakiwa kumpiga nacho Myamba alikificha kwenye gata ya kukingia maji karibu na duka, kisha akatorokea mkoani Dar es Saalam.
Amesema Mahakama kupitia upande wa mashtaka imejiridhisha pasipo shaka kutokana na ushahidi uliotolewa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Kutokana na ushahidi huo, Mahakama imemtia hatia kwa mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na marejeo ya mwaka 2022.
Kesi hiyo namba 74 ya mwaka 2022 kwa upande wa utetezi imesimamiwa na Wakili Alex Mgani, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Magdalena Hyasint Whero.
Awali, Wakili Whero ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine, kwani kitendo alichokifanya ni cha kikatili na hakikubaliki katika jamii.