Kova asaidia wenye changamoto ya upumuaji
Muktasari:
- Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Polisi Kilwa Road imepokea mashine mpya za kisasa kuwasaidia wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji.
Dar es Salaam. Taasisi ya Sukos Kova Foundation imetoa msaada wa mashine za kisasa za mkusanyiko wa oksijeni (oxygen concentrators na oximeters) zitazotumika kupima na kuongeza kiwango cha Oksijeni kwenye mwili wa binadamu.
Mashine hizo maalumu kwa kuwasaidia wagonjwa mahututi zenye thamani ya Sh20 milioni, zimetolewa kwenye Hospitali ya rufaa ya Polisi Kilwa Road iliyopo chini ya Jeshi Polisi nchini.
Oxygen concentrators ni mashine yenye uwezo wa kuzalisha oksijeni kwa kutumia umeme bila kwenda kujaza kama ilivyo mitungi ya gesi inayotumika kwa sasa kwenye Hospitali nyingi nchini ambapo gesi ikiisha lazima ikajazwe tena.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Kamishna wa Utawala na Raslimali watu wa Jeshi la Polisi (SACP) Suzan Kaganda, ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa msaada huo kwani ni muhimu kwa wagonjwa hasa wanye shida ya kupumua.
"Niwashukuru taasisi ya Sukos foundation kwakujitoa kwenu na kukumbuka nyumbani kwa sababu tendo lilofanyika leo na kamshina mstaafu Suleman Kova ni kukumbuka nyumbani alikoishi na kufanya kazi Kwa muda mrefu," amesema
Amesema vifaa hivyo vitasaidia kutoa huduma kwa askari na jamii inayowazunguka kwakuwa asilimia 68 wanaopata huduma kutoka Hospitali hiyo ni wananchi.
"Vifaa vilivyotolewa leo ni chachu ya huduma hii inayotolewa na wataalamu ambao ni askari na watumishi raia wanayofanya kazi kwenye vituo vyetu, hivyo vitaongeza utoaji huduma,” amesema.
Amesema hospitali hizo zina changamoto ya vifaa tiba kama vile MRI, an CT Scan na kwamba hata mkuu wa jeshi hilo anajua.
SACP Kaganda ameongeza kuwa leong ni kufanyia kazi changamoto hizo na kwamba malengo ni kuhakikisha hadi kufikia 2025, hospitali hiyo iwezi kutoa huduma bora za afya mikoa yote.
"Tunaendelea kuongeza vifaa tiba na maboresho pamoja na kupanua huduma hizi kwani ipo baadhi ya mikoa ambayo haijafikiwa na huduma hizi jambo ambalo ni changamoto kwa Polisi wetu na watendaji," amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sukos, Suleman Kova amesema taasisi hiyo yenye miaka tisa tangu kuanzishwa imejikita katika kutoa misaada ya vifaa vya kujikinga wakati wa majanga au maafa.
"Hakika sote tunafahamu athari zinazojitokeza pindi majanga au maafa yanapotokea ikiwa ni pamoja na watu kupoteza maisha, mali, uchumi wa nchi kuathirika na kupoteza nguvu kazi kutokana na maafa," amesema.
Amesema kwa kutambua idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali mbalimbali, wanaimani msaada huo utarahisisha kutoa huduma kwa wagonjwa.
"Ni imani yetu vifaa hivi ambavyo vinauwezo wa kufua oksigeni vyenyewe, vitaleta ufanisi mkubwa na tija wakati wa kuhudumia wagonjwa hasa walio mahututi," amesema.
Ameleza kuwa wadau wanaendelea kuhamasika kuunga mkono juhudi za kuboresha Jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya kwa maslahi mapana ya taifa.
Naye Mganga Mkuu mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Lushina Nyanda ameishukuru taasisi hiyo kwa msada huo akisema: “Msaada huu ni muhimu sana katika kuwahudumia wagonjwa wenye tatizo la upumuaji na hasa wanapofikishwa hospitalini hapa.”