Prime
Kuhusu elimu ya katiba, Wazee waweka ngumu
Dar es Salaam. Mpango wa Serikali kutumia miaka mitatu kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi kabla ya kuendelea na mchakato umepata upinzani mpya baada ya mawaziri wakuu watatu wastaafu kuhoji sababu za uelimishaji huo.
Mawaziri wakuu hao ni, Cleopa Msuya na Frederick Sumaye na Jaji Joseph Warioba kwa nyakati tofauti wametoa msimamo huo, wakishauri elimu inayotolewa isiathiri kuendelea kwa mchakato wa mabadiliko, bali yote yafanyike pamoja.
Pamoja na hao, wanasiasa wengine wakongwe wameonyesha kuunga mkono mpango huo kwa hoja kuwa, wao watafuata kile kinachoelezwa na Serikali.
Kauli hizo zinatokana na mpango ulitangazwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alioubainisha Agosti 28, mwaka huu, kuwa kabla ya kuuendea mchakato wenyewe wa mabadiliko ya Katiba, Serikali ingetumia miaka mitatu kuelimisha wananchi kuhusu Katiba mpya.
Dk Ndumbaro ambaye sasa ni waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema hatua hiyo inatokana na utafiti uliobainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu Katiba iliyopo na wengine hawakuwahi hata kuiona.
Kauli hiyo imeibua mijadala mikali kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wengi wakikosoa mpango huo wa Serikali.
Alichokisema Msuya
Akizungumza katika mahojiano na ITV, Waziri mkuu mstaafu, Cleopa Msuya alisema hakupaswi kutengwa muda wa miaka mitatu kuelimisha watu.
Badala yake, Msuya aliyewahi kushika uwaziri mkuu mara mbili (Novemba 1980 - Februari 1983) na Desemba 1994 - Novemba 1995), alisema inapaswa kuangaliwa nini kinapungua katika Katiba ya sasa na kinarekebishwaje.
“Tuone jinsi ya kushauriana na kufikia muafaka tuujumuishe katika marekebisho ya hiyo Katiba mpya iliyopo tuendelee na kazi na watu waendelee na shughuli.
“Kwa mfano, unakuja kule kijijini kwangu (Chomvu Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro) kunielimisha kuhusu Katiba, unamuelimisha nini kwa sababu hakuna Katiba ‘standard’ (kipimo) duniani kote, kila nchi inatunga Katiba kulingana na mazingira na historia yake,” alisema Msuya aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais.
Kwa mujibu wa Msuya (92), tume mbalimbali ziliwahi kuundwa hata wakati wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na fedha nyingi zilitumika.
Hata hivyo, mtazamo wa Msuya ni tofauti na wengine wanaolenga kutungwa kwa Katiba mpya, akisema kinachohitajika ni kurekebisha mapungufu yaliyopo katika ya sasa.
“Yafanyike marekebisho kulingana na nini kimeonekana kimepungua na kinaathiri uhuru na matumizi ya uhuru wa watu katika utendaji wa kazi,” alisema.
Alisisitiza kuwa tatizo si elimu, bali kunahitajika kufanywa maboresho katika Katiba iliyopo kwa kuondoa maeneo yanayokera watu.
Hata miaka 10 isingetosha
Mtazamo wa Msuya, hauko mbali na wa Frederick Sumaye, waziri mkuu mstaafu (Novemba 1995-Desemba 2005), aliyesema hata ingetolewa miaka 10 ya elimu isingetosha wananchi kuielewa Katiba.
Kinachopaswa kufanywa kwa mujibu wa Sumaye, michakato mingine ya kufanikisha mabadiliko ya Katiba iendelee, elimu ya Katiba nayo iendelee kutolewa.
“Kuelimisha watu ni sawa, lakini eti katika miaka mitatu, kwamba watu watakuwa wamejua Katiba si sahihi. Wakati tunaendelea na kuelimisha na michakato mingine ya Katiba ingeweza kuendelea,” alisema.
Akifafanua hoja yake, Sumaye (73), alisema ingawa Katiba ni mali ya wananchi, wapo wanaopaswa kuijua kwa kina kwa niaba ya wenzao.
“Wapo waliosoma na walipo katika vyombo vya sheria lakini hawaijui Katiba, ili wasome wanarejea kwenye vifungu mbalimbali,” alisema Sumaye.
Hata hivyo, Sumaye alisema uelimishaji lisiwe jambo lenye ukomo liendelee kufanywa wakati wote.
Pamoja na mtazamo huo, mwanasiasa huyo aliweka wazi kuwa haamini kwamba Katiba mpya ndiyo itakaokua mwarobaini wa shida za watu.
“Kuna mambo mengi yanahitajika ili Katiba ifanye kazi sawasawa,” alieleza kwa ufupi.
Ipo elimu ya kutosha
Waziri mkuu mstaafu mwingine aliyetoa kauli kuhusu suala hilo ni Jaji Warioba (1985-1990), aliyesema tayari wananchi wana elimu ya kutosha kuhusu Katiba mpya na kinachopaswa kufanyika ni kwenda kwenye mchakato wa kura za maoni.
Warioba aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema kinachohitajika sasa ni utashi wa kisiasa kuliendea jambo hilo, au Serikali ieleze wazi kuwa Katiba mpya si jambo la sasa hivi.
“Tunachohitaji sasa ni utashi wa kisiasa, vyombo vya habari vinazungumza sana kuhusu Katiba mpya, ndivyo vinavyofikisha ujumbe kwa Watanzania sambamba na vyama vya siasa. Wananchi wamepata elimu ya kutosha kuhusu Katiba mpya,” alisema mwenye umri wa miaka 83.
Alisema alipokuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitoa elimu kwa wananchi hadi vijijini kwa kusambaza nakala za Katiba ya Tanzania na ya Zanzibar, hivyo wananchi wanaifahamu.
Wakati Warioba akisema hayo, Joseph Butiku aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, alisema “nilishashiriki kwenye kutengeneza maoni ya mabadiliko ya Katiba, ngoja wananchi waseme wanachoendelea kusema, mimi sina maoni juu ya hilo.”
Kauli kama hiyo ilitolewa na Waziri wa zamani, Anna Abdallah aliyesema “Ahh… mimi sina maoni yoyote, kitakachoamuliwa na Serikali ndicho nitakachokisikiliza, mimi nitoe maoni ya nini tena.”
Mjadala wa kitaifa
Ili kuondoka katika mkwamo huo, Dk Willibrod Slaa, katibu mkuu wa zamani wa Chadema alisema uandaliwe mjadala wa kitaifa utakaoshirikisha wananchi kama njia ya kupata Katiba mpya.
“Mjadala wa kitaifa ndiyo mchakato wa kawaida kwenye Taifa lolote katika upatikanaji wa Katiba mpya kwa kuwa unasaidia kukubaliana na mambo ya msingi, si sahihi kwa viongozi wachache kujifungia na kuamua au kufanya wanasiasa wengine wanavyoshauri,” alisema akizungumza na wanahabari jana.
Dk Slaa alisema Afrika ya Kusini ilianza na mjadala wa kitaifa, kisha ikatengeneza njia bora ya kufanikisha mchakato wa Katiba yake.
Alipotafutwa kuzungumzia msimamo wa sasa wa Serikali baada ya maoni kinzani kutoka kwa wananchi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema kwa sasa amejielekeza kwenye Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula (AGRF).
“Naomba tuzungumzie kwanza AGRF kisha hayo mengine tuzungumzie baadaye kaka,” alijibu Msigwa.
Hatua za mchakato
Mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini unaweza kusema ni mfupa mgumu ambao umekuwa kwenye vinywa vya wanasiasa tangu mwaka 1992 nchi ilporejesha mfumo wa vyama vingi.
Mchakato huo ulishika kasi wakati wa Serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete na aliyeunda Tume ya Warioba mwaka 2012 ambayo ilikusanya maoni na kuandaa rasimu mbili kabla ya kukwama mwaka 2014 baada ya Bunge Maalumu la Katiba.
Awamu ya tano chini ya Hayati John Magufuli haikujishughulisha na mchakato huo ikisema si kipaumbele chake.
Matumaini ya kufufuka kwa mchakato wa Katiba mpya, yalifufuka katika awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliposema, “suala la katiba hakuna anayekataa, hata chama changu hakuna anayekataa, na muda si mrefu tutatangaza kamati ambayo itashughulikia jambo hilo,” alisema Rais Samia Machi 8, mwaka huu alipohutubia Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani liliondaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Pamoja na ahadi hizo, utekelezwaji wa michakato kuelekea mabadiliko hayo ndicho kitendawili kisichoteguka hadi sasa, huku kauli mbalimbali za Serikali zikiashiria haja ya kuwepo subira ya muda mrefu kabla ya kuifikia hatua hiyo, hali inayofifisha matumaini hayo.
Nyongeza na Bakari Kiango