Mohamed: Elimu ya Katiba miaka mitatu itaturudisha nyuma
Dar es Salaam. Mhariri wa Siasa wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed amesema mpango wa Serikali wa kutoa elimu ya katiba ya miaka mitatu utalirudisha Taifa kwenye mkwamo wa kuandika Katiba mpya.
Mohamed ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 6, 2023 wakati akichangia kwenye mjadala wa Mwananchi X – Space ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) ukiwa na mada inayosema: “Nini maoni yako kuhusu miaka mitatu ya elimu ya Katiba kwa wananchi?”
Msingi wa mjadala huo ni kauli ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ya Agosti 28, 20-23 mwaka huu alipotangaza mkakati wa miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2026 ya uelimishaji wa wananchi kuhusu Katiba mpya kabla ya kuuendea mchakato wenyewe wa mabadiliko.
Mchakato wa Katiba uliishia Katiba Pendekezwa mwaka 2014 katika utawala wa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete.
Akichokoza mada hiyo, Salehe amesema kuna watu wanafikiria Katiba ikiwa nzuri itawarahisishia kuingia madarakani kwa sababu Katiba ya sasa imefinya baadhi ya maeneo, lakini pia walioko madarakani wanahofia wakiandika Katiba mpya wataondoka madarakani.
“Hapa tulipo lazima tupate maridhiano ya kitaifa, tunatokaje hapa tulipo na hata huu mpango wa Serikali kutoa elimu kwa miaka mitatu unatia mashaka kidogo,” amesema Mohamed wakati wa mjadala huo.
Ameongeza Rais Samia Suluhu Hasssan akigombea urais maana yake anaweza kumaliza muda wake akaacha mchakato huo bado ukiendelea na hata fedha zinazotengwa zinaweza kupotea kama tulivyoona huko nyuma.
“Tatizo liko kwenye ubinafsi, hatujaamua kuweka maslahi ya taifa mbele. Ili tutoke hapa lazima tuondoe ubinafsi, tuweke maslahi ya Taifa mbele,” amesema mhariri huyo.
Mohamed amesisitiza lazima Taifa lifike mahali liamue kwenda mbele kuhakikisha Katiba mpya inapatikana bila kuzingatia maslahi ya wanasiasa katika vyama au makundi tofauti tofauti.
“Huu muda wa miaka mitatu, Serikali inakwnda kutoa elimu kwa njia ipi? Kwa mikutano ya hadhara? Huu muda uliotengwa unaweza kuturudisha kule tulikotoka, tayari tumeona viongozi wastaafu wakikosoa
“Unapoona mawaziri wakuu wakikosoa jambo, lazima turudi nyuma tujitafakari tuone tunakosea wapi na kujisahihisha. Katiba haiku kwa ajili ya kumweka mtu madarakani, Katiba mpya siyo kwa ajili ya kumbakisha mtu madarakani,” amesema Mohamed