Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuishi kwa ajili ya Mungu tunapata amani ya kweli, furaha

Bwana Yesu asifiwe ninaitwa Aika Ombeni karibu kwenye tafakari ya neno la Mungu leo Jumapili. Kichwa cha somo letu ni “Kuishi kwa ajili ya Mungu tunapata amani na kweli, furaha na uzima wa milele”.

Ninakukaribisha msomaji wangu katika tafakari ya leo inayotukumbusha namna ya kuishi katika kumpendeza Mungu

 Kuishi kwa ajili ya Mungu ni wito wa msingi kwa kila Mkristo. Katika ulimwengu wa leo unaosisitiza sana mafanikio binafsi, maendeleo ya kiuchumi na kujijenga kama mtu, ni rahisi kupoteza mwelekeo wa kusudi la kweli la maisha ya Kikristo.

Ingawa ukuaji binafsi siyo jambo baya, unakuwa na maana tu pale unapowekwa chini ya mapenzi ya Mungu.

Biblia inatukumbusha wazi kwamba maisha yetu siyo yetu wenyewe. Katika Warumi 14:8 imeandikwa: “Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa ajili ya Bwana; na kama tukifa, twafa kwa ajili ya Bwana.

 Basi kama tukiishi au tukifa, tu mali ya Bwana.” Hii inaonyesha kwamba kusudi kuu la maisha ya Mkristo ni kumtukuza Mungu katika kila jambo.

Katika jamii ya sasa, watu wengi wanahamasishwa kufuatilia ndoto zao, kujipenda zaidi na kutafuta furaha kwa njia ya mali, mafanikio, au hadhi.

Lakini Yesu Kristo alifundisha tofauti kabisa. Katika Mathayo 16:24 anasema: “Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Hapa tunaona kuwa kumfuata Kristo kunahusisha kujikana nafsi, siyo kuikuza kupita kiasi.

Kuishi kwa ajili ya Mungu kunamaanisha kuweka mapenzi yake mbele ya tamaa zetu. Ni kuchagua haki hata pale inapokuwa ngumu. Ni kuishi maisha ya unyenyekevu, upendo na huduma kwa wengine.

Wagalatia 2:20 inasema: “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu.” Hii inaelezea mabadiliko ya ndani ambapo maisha ya Mkristo yanaongozwa na Kristo, siyo matakwa binafsi.

Moja ya changamoto kubwa ni kwamba mafanikio ya dunia mara nyingi huonekana kuwa na mvuto mkubwa kuliko maisha ya kiroho.

Hata hivyo, Biblia inatuonya katika Mathayo 6:33: “Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Hapa tunaona mpangilio sahihi Mungu kwanza, mengine baadaye.

Kuishi kwa ajili ya Mungu pia kunaleta amani ya kweli na utoshelevu ambao vitu vya dunia haviwezi kutoa. Wafilipi 4:7 inasema: “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Hii ni ahadi ya utulivu wa ndani unaotokana na kumtegemea Mungu.

Zaidi ya hayo, maisha ya kumtumikia Mungu yana athari kwa wengine. Tunakuwa nuru na chumvi ya dunia kama ilivyoandikwa katika Mathayo 5:13-14. Watu wanapoona matendo yetu mema, wanamtukuza Mungu. Hivyo basi, kuishi kwa ajili ya Mungu siyo kwa faida yetu tu, bali pia kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Ni muhimu pia kuelewa kwamba Mungu anajali ukuaji wetu binafsi lakini ukuaji huo unapaswa kuwa wa kiroho kwanza. 2 Petro 3:18 inasema: “Lakini kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo.” Huu ndio ukuaji wenye thamani ya milele.

Maisha ya Kikristo siyo safari ya kujitafuta binafsi pekee, bali ni safari ya kumtafuta Mungu na kuishi kulingana na mapenzi yake.

 Dunia itapita na tamaa zake, lakini anayefanya mapenzi ya Mungu adumu milele (1 Yohana 2:17).

Hivyo basi, ni hekima kuchagua kuishi kwa ajili ya Mungu kwa sababu ndani yake ndipo tunapata maana ya kweli ya maisha, amani ya kudumu, na tumaini la uzima wa milele.


Kwa ushauri, Aika Ombeni anapatikana kupitia simu 0719 705 271.