Kujifukiza Muhimbili, Mloganzila Sh5000 tu

Thursday March 04 2021
kujifukiza pic

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru akitoka kujifukiza katika moja ya mashine za kujifukiza zilizofungwa katika hospitali hiyo leo

By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Mloganzila zimefunga mashine nne  za kujifukiza.

Wakati Muhimbili zikifungwa mashine tatu, Mloganzila imefungwa moja. Gharama ya kila mashine ni Sh7.5 milioni na kila moja ina uwezo wa kuhudumia watu sita kwa wakati mmoja wanaopaswa kukaa kati ya dakika tano hadi 10.

Ili mtu aweze kujifukiza katika mashine hizo anapaswa kulipia Sh5,000 na yeyote anaruhusiwa hata wapita njia.

Akizungumza katika uzinduzi wa mashine hizo zilizopewa jina la Bupiji Sauna leo Alhamisi Machi 4, 2021 mkurugenzi mtendaji wa MNH,  Profesa Lawrence Museru amesema kuanzishwa kwa mashine hizo kutarahisisha upatikanaji wa huduma ya kujifukiza kwa watu wote wanaohitaji.

“Kujifukiza huku kunaenda sambamba na matumizi ya dawa za asili ambazo zimekuwa zikitumiwa na zimeonyesha kusaidia, mashine hii inatumia dawa ya Bupiji inayowekwa katika maji ya mvuke na mgonjwa au mtu anayetaka anaingia ndani atakaa dakika tano hadi 10,” Profesa Museru

Profesa Museru amesema uwepo wa mashine hizo kutawawezesha madaktari kujua kama njia hiyo inasaidia kwa kiwango gani vita dhidi ya corona.

Advertisement

“Kupitia njia hii ya kufanya utafiti tutaweza kuwaambia wananchi kwa uhakika kuwa hiki kinachosemwa kinasaidia au la,” amesema Profesa Museru

Kwa upande wake George Buchafe kutoka Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) amesema kwa zaidi ya miaka mitano wamekuwa wakifanya utafiti ili kupata dawa tiba inayoweza kusaidia kupambana na magonjwa ya kuambukiza wakishirikiana na wataalamu wa afya

“Tunaamini Watanzania watapata majibu hivi karibuni kupitia Bupiji, dawa hii ina mchanganyiko wa mimea, magome ya miti,” amesema Buchafe

Ili mashine hiyo ya kujifukiza ifanye kazi vizuri vichupa vitatu vya dawa hiyo huchanganywa katika maji na kutumika kwa saa moja kabla ya kuwekwa nyingine.

Advertisement