Madaktari wabaini mende kwenye sikio

Daktari asema wenye tatizo la usikivu duniani kuongezeka

Muktasari:

Madaktari wameshauri elimu itolewe kuhusu afya ya sikio ili kuondoa changamoto ya usikivu inayowaathiri zaidi watoto huku Dk Cosmas Mnyanyi akienda mbali zaidi kwamba katika vipimo wapo waliokutwa na mende kwenye masikio.

Arusha. Madaktari wameshauri elimu itolewe kuhusu afya ya sikio ili kuondoa changamoto ya usikivu inayowaathiri zaidi watoto huku Dk Cosmas Mnyanyi akienda mbali zaidi kwamba katika vipimo wapo waliokutwa na mende kwenye masikio.

Hayo yalielezwa katika  siku  ya afya ya sikio duniani iliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Patandi.

"Katika kuadhimisha siku hii tumekuwa tukitoa huduma maalumu ya upimaji wa afya ya sikio na kutoa tiba kwa wanaokutwa  na tatizo, tumegundua watu wengi hawana elimu juu ya utunzaji wa masikio yao na kuwasababishia kupata matatizo.”

“Kuna watu hawayafanyi usafi masikio hivyo unakuta uchafu unalundikana na kusababisha uziwi kutokana na kuziba kwa uchafu, mengine tumekuta hata kuna mende ndani,  elimu ni muhimu sana,” amesema Dk Mnyanyi.

Dk Mnyanyi ambaye ni mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu Huria Tanzania na mkuu wa kitengo kinachosimamia huduma za wenye ulemavu amesema kuna haja wadau mbalimbali na watafiti waliobobea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa afya ya sikio.

Amesema tatizo la kutokusikia bado ni changamoto kubwa kwa Mkoa wa Arusha,  walioathirika zaidi ni watoto kutokana na umakini mdogo wa wazazi huku akiwataka kujenga utaratibu wa kuwapeleka watoto kupima afya.

Naye daktari bingwa wa masikio, pua na koo wa hospitali ya KCMC, Kenneth Mlay amesema baada ya kufanya upimaji wa watoto na watu wazima wamegundua tatizo kubwa la usikivu hasa kwa watoto.

Amesema watoto wengi wana matatizo ya kupasuka kwa ngoma ya sikio, “nawaomba wazazi mtoto akizaliwa wampeleke mara kwa mara kupima masikio  ili  waweze kupata tiba mapema kabla tatizo  halijawa kubwa.”

Mratibu wa mradi wa ushirikiano kati ya chuo hicho na Shirika la Sintef la Norway, Isaack Myovela amesema mradi huo umejikita kusaidia watoto wenye changamoto ya usikivu Tanzania.

Amesema wametembelea shule za msingi tisa Mkoa wa Arusha na nne mkoani Kilimanjaro,  katika uchunguzi wamebaini tatizo la usikivu kwa watoto bado kubwa na  wamewashirikisha wazazi ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kutunza masikio.

Imeandikwa na Happy Lazaro