Daktari asema wenye tatizo la usikivu duniani kuongezeka

Daktari asema wenye tatizo la usikivu duniani kuongezeka

Muktasari:

  • Wakati dunia  ikiadhimisha siku ya usikivu leo Jumatano Machi 3, 2021 inakadiriwa kufikia mwaka 2050 watu bilioni 2.5  watakuwa na matatizo ya usikivu duniani kote.

Dar es Salaam. Wakati dunia  ikiadhimisha siku ya usikivu leo Jumatano Machi 3, 2021 inakadiriwa kufikia mwaka 2050 watu bilioni 2.5  watakuwa na matatizo ya usikivu duniani kote.

Hali hiyo inatokana na watu wengi kujiweka katika mazingira yenye kelele na matumizi yasiyo sahihi ya dawa ambayo huchangia kuondoa uwezo wa kusikia.

Akizungumza leo daktari bingwa wa masikio pua na koo, Edwin Liyombo amesema kwa sasa watu bilioni 1.5 wana matatizo ya usikivu  duniani kote.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na tatizo hilo huku idadi kubwa ya waathirika wakiwa ni watoto.

Dk Liyombo amesema mwaka 2020 asilimia 18 ya wagonjwa waliohudumiwa katika kliniki ya Hospitali ya Taifa Muhimbili waligundulika kuwa na matatizo ya usikivu.

Ameeleza kuwa watu hao ni wenye matatizo yaliyohitaji kuwekewa vifaa vya kuwaongezea uwezo wa kusikia na wengine kuhitaji kufanyiwa upasuaji wa kupandikizwa kifaa cha usikivu.

Kuhusu watoto amesema wengi wamepata tatizo hilo kwa kuzaliwa nao kutokana na wajawazito kutumia dawa kali bila ushauri wa daktari na changamoto wakati wa kujifungua.