Kukithiri ajali barabarani: ‘Tatizo ni madereva’

Gari ndogo ainaya Mazda iliyogongana uso kwa uso na lori la mafuta na kusababisha watu 13 kufariki na 6 kujeruhiwa jana.Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Vyama vya madereva wa malori na mabasi vimeitaka Serikali kuanzisha mfumo maalumu wa kuwachuja na kuwapata madereva bora ili kupunguza matukio hayo ya ajali nchini.

Dar es Salaam. Wakati ikielezwa kuwa chanzo kikuu cha ajali za barabarani ni uwepo wa madereva wasio na sifa wanaoendesha magari ya abiria na mizigo, vyama vya madereva wa malori na mabasi vimeitaka Serikali kuanzisha mfumo maalumu wa kuwachuja na kuwapata madereva bora ili kupunguza matukio  ya ajali.

Hayo yanakuja wakati ajali zikiendelea kusababisha vifo na majeruhi, huku vyanzo vya ajali hizo vikitajwa kuwa ni uzembe wa madereva, ubovu wa barabara na ubovu wa magari.

Mwananchi limekusanya matukio ya ajali sita za barabarani zilizosababisha vifo na majeruhi kwa watu tangu Januari hadi Aprili 2024.

Miongoni mwa ajali hizo ni ile iliyotokea juzi Kijiji cha Somanga Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na kusababisha  vifo 13, huku abiria wengine sita wakijeruhiwa.

Akizungumzia ajali hiyo kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari dogo la abiria aina ya Mazda lililokuwa likitokea Somanga kuelekea Nangurukuru, kugongana uso kwa uso na lori la mafuta katika barabara kuu ya Lindi – Kibiti.

"Huyu dereva wa lori alihama upande wake na kulifuata gari la abiria bila kuwa na tahadhari yoyote na kusababisha vifo vya watu 13,” alisema Kamanda Imori.

Ajali nyingine ilitokea Machi 29, 2024 na kusababisha vifo vya mashabiki wawili wa Klabu ya Soka ya Simba.

Ajali hiyo imetokea eneo la Vigwaza wilayani Chalinze ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster lililobeba mashabiki wa Simba tawi la Kiwira, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya waliokuwa wakielekea Dar es Salaam kushuhudia mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly ya Misri na Simba.

Ajali nyingine ilitokea Rufiji Machi 26, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wawili wakitokea jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye gari dogo lililogongana na lori eneo la Nyamwage.

Nyingine ilitokea eneo la Ruvu, Machi 28, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wawili na majeruhi watatu ikihusisha mabasi mawili ya kampuni za Sauli na New Force ambayo yaliligonga lori ubavuni na baadaye kutokea mlipuko wa moto, uliosababisha magari hayo kuteketea.

Ajali nyingine ilitokea Machi 10, 2024 wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani ikihusisha magari ya Toyota Coaster iliyokuwa ikisafirisha abiria kuelekea Bagamoyo na Fuso lililobeba mawe yakagongana uso kwa uso.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu tisa chanzo kikitajwa ni uzembe wa dereva wa Fuso aliyejaribu kuyapita magari yaliyo mbele yake.

Ajali nyingine ilitokea Februari 24, 2024 jijini Arusha ikihusisha lori mali ya Kampuni ya KAY Construction ya Nairobi, Kenya na magari mengine madogo matatu, ilisababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi wengine 21.

Chanzo cha ajali kinaelezwa kuwa ni kufeli kwa mfumo wa breki wa lori na kwenda kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake.

Mfumo kuwapata madereva bora

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 23, 2024, Mwenyekiti wa Madereva wa Mabasi, Majura Kafumu amesema kuwa madereva wana nafasi kubwa ya kusababisha ajali kama watakuwa hawajaandaliwa vizuri.

“Serikali itengeneze mfumo wa kumpata dereva sahihi kupitia leseni. Ajali inategemea na uelewa wa dereva je,  madereva waliopo wana uelewa wa kutosha kupewa leseni? Au unamkabidhi gari shemeji yako ili kulinda uhusiano?

“Sisi kama chama tumepiga kelele tangu mwaka 2011 tukidai kuwa madereva watambuliwe kisheria na Serikali, lakini Serikali inasema hii ni sekta binafsi kwa hiyo tujadiliane na tajiri mwenye gari,” amesema.

Kafumu aliyeanza udereva tangu maka 1987, amesema hatua ya Serikali kuziacha ajira za madereva kwa watu binafsi, imesababisha taaluma hiyo kudharauliwa na kuingiliwa na madereva wasio na sifa.  

“Serikali imeitupa sekta ya udereva hivyo  kila mtu anakwenda tu kuchukua. Kwa nini tusiwe na chuo kamili cha kumfunza dereva ili akitoka hapo awe amehitimu kama dereva kamili?” amehoji.

Amesema uwepo wa vyuo vya mitaani kufundisha madereva ndio unazalisha wasio na sifa.

“Umewahi kuona hivi vyuo vya mitaani vikitoa mafunzo ya malori na mabasi? Halafu unashtuka mtu amepewa leseni daraja C na hizo ni nyaraka za Serikali. Unategemea nini?”

Amesema madereva wengi wanaokwenda kuongeza ujuzi kwenye vyuo vya Serikali kikiwemo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wanakuwa tayari na leseni kubwa na wanaendesha malori na mabasi.

“Ili dereva afuzu kuendesha gari la abiria anatakiwa uende chuo miezi sita, baada ya hapo unatakiwa uwe chini ya dereva mwandamizi kwa miaka minne. Baada ya hapo anatakiwa kupanda kuwa dereva mwandamizi maana umeshakomaa.

“Lakini leo na uzoefu wangu, halafu anaajiriwa dereva mpya tunalingana mshahara. Halafu ukimwelekeza, anapiga simu kwa tajiri anakushitaki. Hiyo yote ni kwamba hakuna utaratibu wa kuwapata madereva,” amesema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Jaeka Mdami, akisema baadhi ya wamiliki wa magari ndio wanavuruga mfumo wa kuwapata madereva bora.

“Baadhi ya wamiliki wanataka madereva wa bei ya chini, ili iwe rahisi kuwaburuza wanavyotaka. Ili uwe na dereva bora, kwanza angalia historia yake, uwezo, nidhamu na tabia yake,” amesema.

Amesema wamekuwa wakiiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwapata madereva kupitia vyama vyao ili kupima vigezo vyao.

Kuhusu vyuo amesema, madereva wengi hawakujifunza kuendesha malori vyuoni bali udereva wa magari madogo.

Hata hivyo, Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema kabla ya kumwajiri dereva ni lazima kwanza aonyeshe vyeti.

“Chanzo kikuu cha ajali ni uzembe wa madereva, hata ukiangalia ajali ya hivi juzi Kilwa chanzo kilikuwa ni dereva wa lori kulala.

“Sisi tunataka unapokuja kuomba kazi uwe na vyeti vyote vinavyotakiwa na Latra. Hatuwezi kukupa kazi bila kuwa na nyaraka zilizokamilika.

“Hata tukienda Latra (Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu), kuomba leseni huwezi kupewa kama huna vyeti vya dereva vilivyokamilika,” amesema.


Madereva wanapatikanaje?

Mwanasheria ya Kitengo cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni amesema utaratibu wa kuwapata madereva wa mabasi na malori ni hadi wapitie mafunzo kwenye vyuo vya Serikali.

“Dereva anayepewa leseni daraja C ni lazima aende darasani akasome vyuo vilivyosajiliwa. Dereva anaweza kusoma vyuo hivyo vya chini lakini akitaka daraja C lazima aende NIT au vyuo vya Veta au Chuo cha Teknolojia Arusha,” amesema.

Amesema kabla dereva hajapewa leseni yoyote kwanza anatakiwa kusoma, kisha atafanyiwa majaribio na akifaulu ndio atapewa leseni.

“Dereva akishaenda kuajiriwa, sisi hatuhusiki, ni mwajiri akiona anafaa, atakuja kuomba hati ya tabia njema kutoka polisi,” amesema.

Amesema ili kuwadhibiti madereva wamekuwa wakiwasajili ili kuhakiki vyeti vyao.

“Madereva wako zaidi ya milioni tatu, si wote waliosajiliwa na tumegundua ajali nyingi zinasababishwa na ambao hawajasajiliwa,” amesema.

Latra waanza kuwathibitisha madereva

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesema tangu mwaka 2020 wameshaanzisha utaratibu wa kuwathibitisha madereva bora.

“Sheria ya Latra namba 3 ya 2019 inaipa mamlaka ya kuthibitisha madereva. Kwanza dereva aliye na leseni aliyopewa Mamlaka ya Mapato (TRA), anatakiwa kuja Latra na kitambulisho cha Taifa (Nida), kisha atafanya mtihani na baada ya nusu saa atapewa majibu. Akifaulu atapewa cheti cha kuthibitishwa.”

“Tulianza mwaka 2020 na bado tunaendelea. Tukipata idadi kubwa tutawatangazia wenye kampuni za mabasi wasiajiri dereva asiyesajiliwa.

Amesema wameanza kuwapa sharti la kuwa wamethibitishwa madereva wanaosafiri usiku.