Kumekucha ACT-Wazalendo

Kumekucha ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo, inatarajiwa kukaa muda wowote kuanzia leo kwa ajili ya kuchambua na kupendekeza jina la mwanachama atakayemrithi Maalim Seif Sharif Hamad katika nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Dar es Salaam. Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo, inatarajiwa kukaa muda wowote kuanzia leo kwa ajili ya kuchambua na kupendekeza jina la mwanachama atakayemrithi Maalim Seif Sharif Hamad katika nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Baada ya kupendekezwa, jina la mwanachama huyo litapelekwa haraka kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa ajili ya uteuzi wa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akichukua nafasi ya Maalim Seif aliyefariki dunia Februari 17 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matitabu.

Kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, kamati ya uongozi inaundwa wajumbe tisa ambao ni viongozi wakuu wa chama hicho kati yao wawili hawapo ambao, ni Maalim Seif huku Bernard Membe akijiuzulu nafasi hiyo, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kwa sasa viongozi saba ndiyo watakaomua jina la mrithi wa Maalim Seif ambao ni Zitto Kabwe (Kiongozi wa chama), Ado Shaibu (Katibu Mkuu), Juma Duni Haji (Makamu Mwenyekiti –Zanzibar), Dorothy Semu (Makamu Mwenyekiti –Bara), Nassor Ahmed Mazrui (Naibu Katibu Mkuu –Zanzibar).

Wengine ni pamoja na Joran Bashange ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo-Bara pamoja na Omary Said Shaaban ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.

Taarifa za kuaminika ambazo Mwananchi linazo ni kwamba, tayari vikao vya maandalizi vya mchakato huo vimeshaanza mjini Unguja na wakati wowote kuanzia leo Kamati ya Uongozi itaketi kwa ajili ya kumchagua mrithi huyo wa Maalim Seif.

Miongoni mwa vikao hivyo ni viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo kukutana viongozi wa majimbo, mikoa na ngazi ya taifa wa mjini Unguja kwa lengo la kubadilishana mawazo.

Gazeti hili jana lilipomtafuta Zitto kwa simu kazungumzia mchakato huo alijibu kwa kifupi: “Mbona mna haraka subiri kwanza, chama kitatoa taarifa.”

Hata hivyo, Mwananchi linafahamu kuwa miongoni mwa wanachama wanaopewa nafasi kubwa kuchukua mikoba ya Maalim Seif kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni pamoja na Mazrui, Duni, Mansour Yusuf Himid na Othman Masoud Othman ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar enzi za utawala wa Dk Ali Mohamed Shein.

Wanachama hawa wanne wanatajwa kurithi nafasi hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mchango wao mkubwa katika kuijenga ACT Wazalendo na kufanya kazi na Maalim Seif kwa muda mrefu lakini, na uwezo mkubwa na uzoefu kwenye masuala ya uongozi.

Miongoni mwao makada hao wanne ni wanasiasa wazoefu wenye msimamo na waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali za marais Aman Abeid Karume na Dk Shein, ambaye mikoba yake imerithiwa na Dk Mwinyi.

Huu ni mtihani mkubwa kwa wajumbe wa kamati ya uongozi kuhakikisha wanampata mtu sahihi atakayeshirikiana na Dk Mwinyi na kuendeleza pale alipoishia Maalim Seif aliyekuwa na ushwawishi mkubwa Zanzibar na Tanzania Bara.

Hadi kufikia leo Jumatatu zitakuwa zimebaki siku nane na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010 inaeleza kuwa, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inatakiwa kujazwa ndani ya siku 14 tangu kufariki dunia, kujiuzulu au kufutwa kazi na Rais.

Ibara ya 40 ya Katiba hiyo toleo la 2010 (1) Endapo nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais au Makamu wa Pili wa Rais itakuwa wazi: (a) kwa sababu ya kufariki au kujiuzulu; au (b) ikiwa Rais amefuta uteuzi huo; (c) kwa sababu nyingine yoyote itakayomfanya ashindwe kuwa na sifa za Makamu wa Kwanza au Makamu wa Pili wa Rais.

Rais atamteua Makamu wa Kwanza wa Rais au Makamu wa Pili wa Rais kwa kutegemea na nafasi iliyo wazi. (2) Iwapo mtu atafutwa katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mujibu wa kifungu cha (1)( b) cha kifungu hiki chama chake si zaidi ya siku 14 kitapendekeza kwa Rais jina la mtu mwingine.