Kuvaa nguo fupi ni ukatili kwa wanaume

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Fatuma Mganga

Muktasari:

Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma, Dk Fatuma Mganga amesema kumekuwa na kauli kwamba wanawake wanafanyiwa ukatili wa kijinsia, huku wenyewe wakifanya ukatili kwa wanaume bila kutambua.

Dodoma. Mavazi yasiyo na staha na mienendo kwa baadhi ya wanawake imetajwa kuwa ni ukatili mkubwa kwa wanaume.

Kauli hiyo ilitolewa juzi Desemba 18 na Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma, Dk Fatuma Mganga wakati akizungumza kwenye Kongamano la Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI) wa Kanisa la Anglikana Tanzania.

Kongamano hilo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kupinga ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni ambapo Kanisa likieleza kubeba vita hiyo kwa nguvu zote.

Dk Mganga amesema kumekuwa na kauli kwamba wanawake wanafanyiwa ukatili wa kijinsia, huku wenyewe wakifanya ukatili mkubwa kwa wanaume bila wengine kutambua.

Kwa mujibu wa Mganga kuvaa nguo fupi, zilizobana, zenye kuonyesha baadhi ya viungo huku wanawake wakionyesha kujipitisha kwa wanaume ni ukatili mkubwa hata kuzidi mengine yanayotajwa.

"Mtu unapita kwa mwanaume ukiwa na mavazi yasiyo na staha, unachekacheka na wanaume kwa mitego unajiona mjanja kumbe unafanya ukatili mkubwa wa makusudi, wanawake wenzangu tuache hayo," amesema Dk Mganga.

Kiongozi huyo aliwakumbusha wanawake kujiheshimu na kuepuka mitego ambayo hata huepelekea kuzaliwa kwa watoto ambao wanapewa majina yasiyofaa kwamba ni watoto wa Mitaa wakati Mitaa haijawahi kuzaa watoto.

Kwa upande wake Mratibu wa Umaki, Magreth Massawa amesema lengo la Kongamano hilo ni kuwaweka wanawake pamoja ili wafanye majukumu ya kutimiza wajibu kwa Jamii badala ya kuachia Serikali pekee.

Massawa amesema Kanisa lina uwezo mkubwa wa kuzuia ukatili kwa jamii kwani vitendo vinginevyo vinavyofanyika katika mazingira ambayo waumini wanaona na kushuhudia lakini wanadhani mhusika ni Serikali pekee.

"Kudhulumu mali, kumnyima mtu mshahara au madalali wa kazi navyo ni vitendo vya ukatili na uvunjifu wa amani, tabia hizi zinajitokeza ndani ya waumini sisi au tunaoishi nao na majirani, lazima tuamke," amesema Massawe.

Mratibu huyo ametaja silaha kubwa ya kuyashinda hayo ni kuendelea kutoa elimu kwani mambo mengi yanachangiwa na mila, tamaduni, kutokuwepo upendo na umoja.

Alisema ukatili huepelekea umasiki na mwisho wake Kanisa hupoteza nguvu kazi, muda na mali ambavyo si msingi wa kuanzishwa kwa Kanisa la Kristo.

Awali Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Winifrida Dickson amesema vita ya ukatili ikipiganwa ndani ya nyumba za ibada itakuwa na nguvu zaidi ya kuishinda.

Mchungaji Winifrida alisema uamuzi walioufanya wenzao wa Kanisa la Anglikana una maana kubwa ambao unapaswa kuigwa na wanawake wa madhehebu mengine ili kuunganisha nguvu kwani vita ya ukatili haichagua.