Lafarge Tanzania yaeleza matumaini, kampuni ya Uswizi ikiuza hisa zake

Muktasari:

  • Holcim imetia saini makubaliano ya kuuza asilimia 65 ya hisa zake katika kampuni ya Mbeya Cement inayomilikiwa na Lafarge Tanzania, kwa kampuni ya Amsons Group kwa kiasi ambacho bado hakijawekwa wazi, huku pia ikikubaliana kuuza kampuni yake tanzu ya Uganda, Hima Cement, kwa kampuni ya Sarrai Group yenye makao yake makuu nchini Uganda kwa dau la Dola za Marekani 120 milioni (Sh298.299 bilioni).

Dar es Salaam. Baada ya kampuni ya saruji ya Uswisi ya Holcim kueleza kuwa inauza hiza za kampuni zake katika nchi za Tanzania na Uganda kwa kampuni za ndani, kampuni tanzu ya Lafarge Tanzania imesema uamuzi huo utaifanya kampuni hiyo kustawi na kupata faida.

Wiki iliyopita, Holcim ilitia saini makubaliano ya kuuza asilimia 65 ya hisa zake katika kampuni ya Mbeya Cement inayomilikiwa na Lafarge Tanzania, kwa kampuni ya Amsons Group kwa kiasi ambacho bado hakijawekwa wazi, huku pia ikikubaliana kuuza kampuni yake tanzu ya Uganda, Hima Cement, kwa kampuni ya Sarrai Group yenye makao yake makuu nchini Uganda katika mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani 120 milioni (Sh298.299 bilioni).

Hata hivyo, mikataba hiyo lazima iidhinishwe na wadhibiti.

Nchini Tanzania, kampuni ya Holcim Group ilmesema imeingia makubaliano ya mauziano na kampuni ya Amsons Group, ambayo ilisema itahakikisha mustakabali mwema na wenye faida kwa kampuni ya Mbeya Cement.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Lafarge Tanzania, Medhat Ismail amesema katika taarifa yake kwamba mkakati wa Holcim wa mwaka 2025 wa kuongeza kasi ya ukuaji wa kijani, unalenga kuimarisha uongozi wake katika masoko yake ya msingi.

“Inalenga kuwa kiongozi wa kimataifa katika suluhisho la kiubunifu na endelevu katika ujenzi. Katika muktadha huu, Holcim inatathmini kila mara fursa za kuoanisha shughuli zake na dira hii na kufungua fursa mpya za kukuza kampuni,” amesema Medhat Ismail.

Amesema Holcim imechukua uamuzi wa kuuza kampuni yake hiyo tanzu na kuingia mkataba wa mauzo na kampuni ya Amsons Group, kwa ajili ya kuiuzia kampuni ya Pan African Cement Limited (kampuni tanzu ya Holcim) ambayo ina asilimia 65 ya hisa za Mbeya Cement.

“Tunafurahi kupata mshirika wa kimkakati na wa kuaminika wa biashara katika kampuni ya Amsons Group ambaye amejipanga vema kuendelea kuwekeza katika ukuaji wake wa muda mrefu. Holcim inaona ni fursa kwa pande zote na inaamini kuwa mpango huu utakuwa mustakabali mzuri na wenye faida kwa kampuni ya Mbeya Cement,” imesomeka taarifa hiyo.

Kampuni ya Amsons Group ni biashara inayoendeshwa na familia katika sekta ya mafuta na gesi na uzalishaji wa bidhaa nchini Tanzania, Msumbiji na Zambia, ikimiliki na kuendesha kiwanda cha saruji nchini Tanzania. Utwaaji huu ni sehemu ya mkakati unaoendelea wa ukuaji wa kampuni ya Amsons Group katika tasnia ya ujenzi.

Shughuli hiyo kwa sasa inapitia mchakato wa kuidhinishwa na mamlaka husika. Zaidi ya hayo, Mchakato huo uko katika hatua ya kushikilia na vipengele vyote vya uendeshaji vinabaki vilevile ha wakati wa kufungwa (inayotarajiwa kuwa robo ya kwanza ya mwaka 2024).

Shughuli za kampuni zitadumishwa na kuendelea kama kawaida, “Mbeya Cement tunathamini sana wafanyakazi wetu ambao wamejenga biashara hii kwa miaka mingi.”