Tenga aipa tano FCC, ni katika sakata la Twiga, Tanga Cement

Muktasari:

Tenga asifu jitihada zilizochukuwa na FCC, kumaliza ndani ya muda sakata la kampuni mbili za kuzalisha saruji nchini huku akitaka mbinu hizo kutumika kwenye migogoro mingine ya aina hiyo ili shughuli zingine ziendelee.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga ametoa kongole kwa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) kwa kushughulikia ndani ya muda Sakata la kampuni kubwa mbili ya Twiga na Tanga zinazozlishaji saruji hapa nchini.

Katika sakata hilo la muda mrefu kampuni ya Twiga, iliweka nia ya kutaka kuimiliki, hisa asilimia 60 za kampuni inayozalisha saruji ya Tanga Cement, hatua iliyoibua wasiwasi kwa baadhi ya wadau na washindani wa soko hilo ikiwemo Chama Cha Walaji Tanzania waliopinga uamuzi huo kufanyika.

Msingi wa hoja ya wadau hao walikuwa wanaamini iwapo mpango huo ungeruhusiwa kufanyika basi ungeenda kuathiri soko la bidhaa hiyo na serikali ingepoteza vyanzo vya mapato na watu kukosa ajira.

Akizungumza Dar es Salaam leo, baada ya kuhitimisha semina ya uhamasishaji wa masuala ya ushindani na udhibiti bidhaa bandia kwa shirikisho la wenye viwanda,liyoandaliwa na FCC, Tenga amesema sakata hilo liliwapa wasiwasi kwa namna lilivyokuwa linatokota.

‘’Tunashukuru baada ya kufika kwenu mlikaa na mkalimaliza zikapatikana kampuni mbili zinaendelea kufanya kazi ajira zinaendelea na serikali inapata mapato yake,’’ amesema

Tenga amesema kwa hatua walizochukua kumaliza sakata hilo basi ni muhimu ikifika changamoto nyingine kwenye taasisi hiyo inayofanana na sakata hilo basi wazingatie muda katika kumaliza.

‘’Wafanyabiashara wanazingatia zaidi muda na ndiyo biashara,muda ni kitu muhimu zaidi katika kupiga hatua hususan kwenye nyakati zilizopo,’’ amesema

Amegusia hata semina zinazoendelea kutolewa na taasisi hizo zinawapa nidhamu ya kudumisha utawala wa sheria katika kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia miongozo.

‘’Ni lazima sokoni tushindane kwa haki tusipofanya hivyo tutaua soko letu,hasa katika kipindi hiki ambacho nchi imeshaingia mikataba ya soko huru ni lazima tujipange kiweledi vinginevyo bidhaa za nje zikianza kuingia tutashindwa kuendana na kasi,’’amesema

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Urio amesema wafanyabiashara waache kufanya vitendo vinavyolenga kuwaondoa wazalishaji wengine sokoni huku akieleza kufanya mbinu hizo ni kutaka kuikosesha serikali vyanzo vya mapato.

‘’Si mchezo mzuri huo, hata kupanga bei ya chini mnaisababishia serikali hasara katika jitihada za kuendeleza uchumi wa nchi kwa kuwaletea wananchi huduma muhimu,’’ amesema

Amesema muunganiko wa makampuni ni jambo la kawaida katika uchumi wowote unaokua lakini sheria inazuia muungano wowote wa makampuni unaosababisha kuwepo au kuimarisha hodhi ya soko.

‘’Sheria imeweka kizingiti ambacho kikifikiwa na kampuni zinazotaka kuunganisha shughuli zao za kibiashara ni lazima ziitaarifu FCC kabla ya kuungana tuchunguze tujiridhishe,’’ amesema

Amesema kwa sasa kigezo cha kuungana kampuni kiwango cha mtaji kilichotangazwa na tume hiyo tangu mwaka 2017 kinaanzia Sh3.5 bilioni na kabla ya hapo ilikuwa Sh8 bilioni na kiwango cha chini kinaachwa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.

‘’Ikibainika watu waliingia makubaliano bila kuzingatia sheria, kifungu namba 60, kifungu cha kwanza kinataja faini yake ni isiyopungua asilimia tano au isiyozidi asilimia 10 ya pato ghafi la mwaka,’’ amesema

Amesema tangu mwaka 2007 taasisi hiyo inayosimamia haki ya mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia nchini imepitisha jumla ya maombi 691ya miungano ya kampuni kutoka sekta mbalimbali ikiwemo madini na kilimo.