Latra: Tofauti za taarifa kero kwenye teksi mtandao

Muktasari:

  • Changamoto inayolalamikiwa zaidi kwenye huduma ya teksi mtandao ni tofauti ya taarifa za mfumo na uhalisia, Latra na Polisi waeleza.

Dar es Salaam. Kumekuwepo na changamoto mbalimbali kwenye matumizi ya teksi mtandao, kubwa ikiwa ni tofauti ya taarifa za kwenye mfumo na uhalisia.

Hayo yamebainishwa na Ofisa wa Leseni wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Jonathan Kitururu kuwa suala hilo ndilo linalolalamikiwa na abiria wengi.

“Tunapata malalamiko ya watu wengi kuhusu kupakiwa na gari ambalo ni tofauti na aliloita au kupakiwa na dereva tofauti na aliyetajiwa katika mfumo huo. Mtu ‘akirequest’ (akiitisha), anapewa taarifa tofauti na atakazokutana nazo baadaye,” amesema Kitururu.

Amesema kitendo cha watu wengi kulalamika inaashiria kuwa wanapakiwa na madereva au magari ambayo hayajaidhinishwa na Latra, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

“Hii ni hatari kwa usalama wa abiria, ndiyo maana pindi tunapopata malalamiko kama hayo tunachukua hatua na mara nyingine tunawaita watoa huduma kuzungumza nao,” amesema Kitururu wakati wa uzinduzi wa wa mtoa huduma mpya wa huduma hiyo, anayefahamika kama Suka.

Kitururu ameitaka Suka kuzingatia vigezo na masharti katika huduma zake huku wakifuata masharti ya leseni na kwamba Latra ina mamlaka ya kutoa kuhuisha na kunyang’anya leseni pale inapobidi.

Wakati Latra ikisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kwa upande wake changamoto anayoiona kwenye huduma ya taksi mtandao ni lugha mbaya ya madereva na vitendo visivyo na heshima.

Vilevile kamanda huyo amesema abiria wanalalamikia suala la mavazi yasiyofaa na uadilifu kwa madereva wanaotoa huduma hiyo.

Katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam Msimamizi wa mifumo na mtathimini biashara wa Teksol ambao ndiyo wamiliki wa Suka, Raphael Ndagala alisema mtandao huo unaweza kutumiwa na dereva na abiria kwa urahisi zaidi kuliko wengine waliopo sokoni.

“Kwanza tumetatua changamoto ya chenji, mteja anaweza kulipa kwa kutumia simu au kutumia mkoba wake wa akiba ulipo katika aplikesheni yetu, na ili kudhibiti usalama dereva ana kiwango cha mwisho cha kufanya kazi baada ya hapo anapaswa kupumzika,” alisema Ndagala.

Ndagala amesema kwa sasa wameanza na Jiji la Dar es Salaam kisha wataenda mikoani.