Prime
Simulizi masaibu ya madereva teksi mtandao
Dar es Salaam. Kuongezeka kwa matumizi ya huduma za teksi mtandao kunaendana na ongezeko la visa na mikasa vivyowakuta madereva wa usafiri huo na kuifanya kazi hiyo iwe na changamoto za hapa na pale.
Mbali na changamoto ya kufanya kazi kwa saa nyingi bila kuwa na mapumziko ya kutosha, wapo wanaolalamika kutapeliwa na abiria na usalama wao kuwa shakani na mambo mengine ya ajabuajabu hasa nyakati za usiku.
Tabata, Sinza maarufu usiku
Katika simulizi yake, mmoja wa madereva hao, Anania Sanga anasema, “kwa Jiji la Dar es Salaam mchana Posta utapata abiria, jua likizama tunasogea yaliko makazi ya watu. Tabata na Sinza ndiko kwenye biashara hasa nyakati hizo, lakini tunapakia wastaarabu, wengine akili zao wanazijua wenyewe!”
“Niliwahi kuwapakia mwanamume na mwanamke nikijua wapenzi, kumbe huyu mwanamke alikuwa anafanya ‘biashara’. Kutoka Tabata mpaka Sinza naambiwa ‘usigeuke nyuma watu wanafanya yao huko’. Nilipomshusha yule jamaa akaniambia ‘huyu (mwanamke) unamrudisha palepale nilipomtoa’, akanilipa mara mbili.”
Anania anasema walipoondoka tu, yule dada akamwambia dereva ampe zile fedha alizolipwa kumrudisha Tabata, kisha amshushe Mlimani City.
Kudura Mustapha, dereva wa bodaboda kwenye Kituo cha Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam, anasema katika miaka minane aliyofanya kazi hiyo, licha ya kumwezesha kusomesha watoto wake wawili na kutunza familia, amepitia mitihani mingi.
"Kazi hii ina vishawishi sana, wapo ambao unawabeba kama abiria, katikati ya safari wanaanza kuleta ukaribu wa kukushawishi kimapenzi,” anasema.
"Wanafanya hivyo wakati dereva haupo kwenye fikra hizo, kuna mwanamke niliwahi kugombana naye nikamshusha njiani baada ya kuanza kunitomasa wakati sikuwa na fikira hizo. Nilimfokea na sikutaka kuendelea na safari, nikamshusha."
Licha karaha hizo, Hassan Juma, dereva wa bajaji pia jijini Dar es Salaam, anasema huwezi kuchagua abiria wa aina gani umbebe.
"Kuna siku niliwahi kuwabeba kina dada wawili, nilitoka nao Segerea. Ukiwangalia ni watu wa heshima tu, kufika mbele mbele kidogo, wakaanza kuhangaika.
“Kumbe walikuwa wako mawindoni, huwezi kuamini, kina dada wale walianza kubadilisha nguo ndani ya bajaji na kuvaa nguo zingine za kazi (ukahaba).”
Juma anaeleza, "kama mwanamume nilijihisi vibaya, lakini nafanyaje, pesa yao naitaka na nipo kazini.”
Pia anasema kuna wakati huwabeba abiria wa jinsi tofauti lakini unakuja kubaini ni wapenzi ambao huanza kufanya mambo yasiyo ya staha kana kwamba wapo sehemu ya faragha.
Vilevile, katika kazi hizo mara nyingi hujitokeza masuala ya utapeli, kama anavyoeleza Dennis John, dereva wa bajaji katika kituo cha Makumbusho.
"Kuna ambao unamfikisha sehemu, anakwambia anaingia ndani kuchukua pesa, kumbe amepitia mlango wa nyuma na kutokomea,” anasema.
Si hivyo tu, John anasimulia, "kuna siku nilimpeleka abiria Buguruni, alikuwa ni mwanamume wa makamo, ukimuona hata huwezi kumdhania angefanya tukio alilonifanyia.
"Tumefika kwenye mtaa mmoja, akaniambia anaingia kwenye nyumba fulani ndipo kwake anakwenda kuchukua pesa, kumbe kuna uchochoro, nilikaa pale kama dakika 10 hatokei, kufuatilia nyumba aliyoniambia anaingia hawamfahamu na kuna njia ya kutokea upande wa pili, tayari nimeachwa. Nilijiona mjinga tu nikaondoka," anasema.
John anasema wapo wateja wengine, ambao hukupigia simu umfuate kumpeleka sehemu fulani, ukifika eneo hilo humkuti na simu haipatikani, wakati huo tayari umeshatumia mafuta na huna wa kumlaumu.
Pia wapo ambao baada ya kubebwa wakifika mwisho wa safari hawalipi, hasa usiku, wakitumia kigezo cha kuwa wamelewa chakari.
"Kuna abiria wastaarabu, lakini wengine ukishamfikisha safari yake, anaona ugumu kutoa pesa, wengine hadi mnazozana. Huwa wanaichukulia kazi hii kama kwamba isiyo ya ustaarabu, lakini wanasahau ndiyo inaendesha maisha yetu na familia zetu," anasema.
Wengine hunasa tundu bovu
Katika uzoefu wake, Awadh Juma, dereva wa bodaboda, anasema wapo madereva walioingia matatani kwa kubeba abiria ambao ni wahalifu.
"Nakumbuka niliwahi kumbeba abiria, kumbe ni mwizi. Amenikodi kijiweni nimpeleke Goba, katikati ya safari tukakamatwa na polisi, wote tukajumuishwa kwenye msala hadi naaminika na kuachiwa nimeshasota sana na kuwa na picha mbaya," anasema.
Awadh mwenye miaka 12 katika kazi hiyo, anaongeza, "hii kazi ina mitihani mingi, kuna rafiki yangu aliwahi kukodiwa kijiweni na mtu akamwambia ampeleke Mbezi Mwisho, akamwambia amlipe Sh30,000 yule abiria hakubisha kumbe alikuwa na nia ya kuiba pikipiki,” anasema na kuongeza:
"Siku hiyo hakurudi, baada ya siku tatu tukasikia mwili wake umepatikana Pugu amefariki dunia na kutobolewa macho. Ilituumiza lakini ndiyo hivyo, mara nyingi ukienda kazini na kurudi nyumbani salama unamshukuru Mungu."
Vikwazo barabarani
Madereva hao wa pikipiki wanasema inapotokea ajali za barabarani, mara nyingi wao ndio huonekana chanzo.
"Bajaji na pikipiki huwa zinaonekana zinakatisha na kupenyapenya, wakati mwingine mwenye gari anaweza kukutengenezea tu ajali na hapohapo kukubadilikia na kuonekana wewe ndiye chanzo, wapo ambao hadi wanadiriki kujichukulia sheria mkononi,” anasema Abdallah Juma, dereva bodaboda.
Upo pia usumbufu wanaouoata kutoka kwa askari wa usalama barabarani kwamba wanapoona namba nyeupe kwenye chombo cha moto ambayo ni kwa ajili ya biashara askari hao wamekuwa wakiwasumbua.
Baruani Omary (31), anasema wamekuwa wakisimamishwa mara kwa mara na trafiki hivyo kuna wakati hulazimika kutumia namba za njano ambazo ni kwa ajili ya watu binafsi.
“Wenye namba nyeupe wanasumbuliwa sana kwa kuwa wanajua ni gari la biashara, lakini kwa mfano nikikamatwa kosa langu litakuwa kwa nini natumia namba ya njano iwapo nitajitambulisha kwamba mimi ni teksi mtandao,” anasema.
Kuhusu hilo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi anasema trafiki wana haki ya kuwasimamisha na kuwahoji madereva wa teksi mtandao kwa kuwa wanatimiza wajibu wa kazi zao.
Alisema trafiki akimkamata na kumlipisha dereva faini na akakubali kuilipa, maana yake ni kuwa amekubali kosa.
“Kama huna kosa mwambie hii silipi nipeleke mahakamani au nipeleke kwa mkubwa wako, kwa kulipa amekiri kosa aliloonyeshwa kwamba hukufunga mkanda, gari yako mbovu, umevuka taa nyekundu au umepaki pasipo stahili, ndiyo maana anakubali, kama hajafanya kosa lolote akatae,” alisema.
Vituko vingine
James Boniface (26), dereva kwa miaka miwili sasa, anasema, “abiria kaniomba kupitia mtandao Kimara Suka, nafika ramani iliponielekeza ananiambia ingiza gari ndani. Nilipoingia walileta sufuria lililojaa mtori, wakanitaka nifungue buti wapakie, sufuria halikutosha wakaniambia nilaze siti, tukaweka sufuria.
“Sikuwa nimeangalia mteja anaenda wapi, aliagiza niongozane na kijana akisema tunaenda Ubungo ambako gharama imesoma Sh4,000. Ninafika mtori umemwagika kidogo kwenye kiti nikalazimika kwenda ‘car wash’ nikatumia Sh10,000 kuliosha.”
Kuchezea mifumo
Madereva pia wanalalamikia changamoto ya baadhi ya abiria kuchezea mifumo, hivyo wanapomaliza safari inasoma gharama kidogo ikilinganishwa na umbali wa safari husika.
Hata hivyo, baadhi ya abiria pia wanalalamika kufanyiwa vivyo hivyo na madereva hao.
Neema Kambi, mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni mtumiaji wa teksi mtandao anadai madereva wamekuwa wakichezea mtandao na kuzidisha nauli.
“Niliwahi kuita teksi mtandao maeneo ya Mbagala inipeleke Tandika Sokoni. Wakati naita ilisoma Sh9,000 hadi Sh11,000 wakati wa safari niliona kwenye ramani kama ruti imecheza na kuonyesha tuko pande za Kipawa - Gongo la Mboto tunaitafuta Temeke. Kufika Tandika nauli inasoma Sh23,000,” anasema.