Latra yatangaza nauli mpya za daladala, mabasi

Dar es Salaam. Vicheko kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu na daladala  huku vIlio vikiwa kwa upande wa wananchi wa kawaida kutokana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kutangaza ongezeko jipya la nauli ambazo zitaanza kutumika Desemba 8, 2023 kama hakutakuwa na pingamizi lolote.

Latra kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Habibu Suluo leo Jumatatu Novemba 27, 2023 jijini Arusha imetangaza nauli hizo mpya ambazo zimepanda kwa viwango tofauti kulingana na umbali na aina ya barabara.

Sababu kuu ya kupanda kwa bei hizo za nauli imetajwa kuwa ni ongezeko la gharama za uendeshaji ikiwamo kupaa kwa bei za mafuta (petroli na dizeli).

Nauli mpya

Suluo amesema daladala zenye ruti isiyozidi kilomita 10 itapanda kutoka Sh500 hadi Sh600, ruti ya kilomita 11 hadi 15 nauli itaongezeka kutoka Sh550 hadi Sh700 na ruti ya kilomita 16 hadi 20 nauli itaongezeka kutoka Sh600 hadi Sh800.

“Daladala zilizokuwa na ruti ya umbali wa kilomita 21 ha 25 nauli itapanda kutoka Sh700 hadi Sh900, zile zenye ruti ya kilomita 26 hadi 30 nauli itapaa kutoka Sh850 hadi Sh1,100,”amesema Suluo.

Taarifa iliyotolewa na Latra pia imesema, kwa daladala ambazo zilikuwa zinatoza Sh1,000 (umbali wa kilomita 31 hadi 35) bei itapanda hadi Sh1,300 na zile zenye ruti ambazo umbali wake ni kati ya kilomita 36 hadi 40, bei ya nauli itapanda kutoka Sh1,100 hadi Sh1,400.

Wakati nauli zikipaa kwa upande wa daladala kwa wastani wa asilimia 10, pia mabasi ya masafa marefu nauli itapaa kulingana na daraja la basi na aina ya barabara inayotumika.

“Mabasi ya daraja la kawaida katika barabara ya lami kila kilomita moja itatoza Sh48.47 kutoka Sh41.29 kama ilivyokuwa awali na kwa barabara ya vumbi daraja hilo litatoza nauli ya Sh53.32 kwa kilomita kutoka Sh51.61,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, nauli itapanda kwa mabasi ya daraja la kati (luxury na semi-luxury) kwa barabara ya lami nauli itapanda kutoka Sh56.88 kwa kilomita hadi Sh67.84.

Aidha, Latra imesema kuwa viwango hivyo vipya vya nauli vinajumuisha tozo ya asilimia 0.5 inayotozwa na mamlaka hiyo.


Mchakato wa kupandisha nauli

Latra imesema ilipokea maombi kutoka kwa makampuni ya utoaji huduma ya usafiri wa abiria ya Super Feo Enterprises, ABC Classic na Happy Nation wakiiomba mamlaka ya kufanya marejeo ya nauli za mabasi kufuatia ongezeko la gharama za uendeshaji, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta (petroli na diseli).

Aidha, katika taarifa yao Latra iliyosomwa na Suluo, imesema iliitisha mkutano na wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya maoni kuhusu viwango vya nauli.

“Mamlaka iliitisha mkutano wa wadau uliofanyika Dar es Salaam, Jumatano, tarehe Oktoba 18, 2023, katika ukumbi wa Arnaoutouglou, ili kutoa fursa kwa makampuni haya kuwasilisha mapendekezo yao kwa wadau na kisha kukusanya maoni ya wadau,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Wananchi walia na bei

Kutokana na upandaji wa nauli hizo, maoni tofauti yameibuka kutoka kwa wananchi huku wakilalamikia bei hiyo kuathiri mnyororo wa uchumi.

“Sikubaliani na bei hizo kwasababu vigezo walivyotumia kupandisha bei hizo bado sijaviona kwasababu hali ya uchumi mtaani ni ngumu, wakipandisha nauli pia bidhaa zitapanda na bodaboda nao watapandisha tu,” amesema Godson Joram mkazi wa Mbagala Chamazi.

Naye Eva Luka mkazi wa Kimara amesema kwa mara ya kwanza kuzizoea nauli hizo itakuwa ngumu ila hakuna namna.

“Kwa mara ya kwanza itakuwa ngumu kwa sababu nitakuwa sijajipanga lakini baadaye tutazoea tu, ila ni maumivu jamani maana kila kitu kitapanda bei, wasafirishaji wa bidhaa kupitia mabasi nao wataongeza bei,”amesema.