Lema kutua nchini Machi Mosi, kuhutubia Arusha

Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amepanga kurejea nchini Machi Mosi 2023 kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Canada.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Godbless Lema, anatarajia kurejea nchini Jumatano Machi Mosi 2023 Saa sita mchana kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Canada.
Taarifa Lema kurejea nchini imeotolewa leo Jumanne Januari 31, 2023 na Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa ikiwa ni siku sita tangu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu aliporejea akitokea uhamishoni nchini Ubelgiji.
Lissu aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka 10 mfululizo kuanzia 2010, aliondoka nchini na familia yake na kuelekea nchini Kenya Novemba 8, 2020 ambako alikaa kwa mwezi mmoja kabla ya kuondoka nchini humo Desemba 8, 2020 kuelekea nchini Canada alipopata hifadhi ya kisiasa kwa madai ya kuwepo kwa tishio la kuuawa yeye na familia yake.
  “Atakapowasili atapokelewa uwanja wa ndege wa KIA na viongozi wa chama, wanachama na wananchi watakao jitokeza kisha kwenda moja kwa moja kwenye mkutano wa hadhara utakao fanyika Arusha Mjini.  
  “Atakaporejea Lema atakuwa na vikao vya kazi ya kuongoza kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kanda na Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini na kisha ziara za mikutano ya hadhara na vikao vya ndani kwenye mikoa yote ya kanda ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha Lema pia atashiriki kwenye mkutano mkuu wa jimbo la Arusha Mjini na atakuwa na ratiba ya ziara kwenye kata mbalimbali za jimbo la Arusha Mjini kwa tarehe ambazo zitaratibiwa na ofisi ya kanda.
“Tunawaalika wanachama na Watanzania wote katika mapokezi makubwa ya Godbles Lema siku hiyo ya Machi Mosi 2023.”