Lema: Sifuti kauli yangu, bodaboda siyo ajira

Mbenge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akihutubia wakazi wa Jiji la Mwanza katika eneo la dampo katika mkutano wa hadhara. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema shughuli ya kuendesha bodaboda siyo ajira inayotakiwa kutegemewa na vijana wa Tanzania badala yake Serikali itengeneze miundombinu ya ajira rasmi kwa vijana.

Mwanza. Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema shughuli ya kuendesha bodaboda siyo ajira inayotakiwa kutegemewa na vijana wa Tanzania badala yake Serikali itengeneze miundombinu ya ajira rasmi kwa vijana.

 Lema ametoa kauli hiyo leo eneo la Dampo jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mkoa huo, huku akidokeza kwamba shughuli hiyo ina madhara mengi kiafya kuliko faida.

"Bodaboda mko barabarani mnavunjika miguu msipotoka kwenye hali ya kupinga umasikini huo mtaendelea kuvunjika miguu. Halafu leo mnatengenezewa majina ya sifa eti mnaitwa maofisa usafirishaji mmedanganywa, mnatengenezewa majina ya kuwafanya masikini," amesema.

Ameongeza; "Baada ya miaka 20 inayokuja bodaboda wote mtakufa kwa sababu mtakuwa wagonjwa wa vifua na majeraha yaliyotokana na shughuli hiyo. Sitaki niwadanganye wala siwezi kuomba radhi narudia tena bodaboda siyo ajira na sifuti kauli yangu,"

Lema ameitaka Serikali kutumia rasilimali zilizopo kutengeneza miundombinu ya ajira kwa vijana ili kuwawezesha kuachana na shughuli hatarishi ikiwemo kuendesha bodaboda.

"Tangu mwaka 2015 serikali ilikuwa haijaajiri, vijana wanamaliza vyuo wanakimbilia mtaani kusota, matokeo yake wanaaminishwa kwamba bodaboda ni ajira wakati wanapoendesha wanavuta upepo, kuumia viuno na mgongo matokeo yake baadaae tutakuwa kuwa na taifa la watu ambao ni wagonjwa wasiyoweza kusalisha," amesema.

"Mwanza kuna Ziwa Victoria, serikali ilitakiwa itengeneze skimu ya kilimo cha umwagiliaji wa bustani, vijana waajiriwe walime wauze mbogamboga na matunda nje ya nchi. Badala yake ni maajabu kukuta tuna rasilimali hii lakini vijana wanalalamika kukosa ajira," amesema.


Hata hivyo, Dereva Bodaboda jijini Mwanza, Samwel Martin ameeleza kukubaliana na kauli ya kiongozi huyo, huku akisema baadhi ya vijana hufanya shughuli hiyo siyo kwa mapenzi yao bali ugumu wa maisha.

"Hii kazi ni hatari kwa afya zetu wakati mwingine tunapata majeraha ya kudumu lakini hatuna namna kwa sababu tusipoifanya familia zetu zitakufa kwa njaa," amesema Martin.

Kwa upande wake, Issa Mohammed amewataka wanasiasa kutotumia changamoto ya ajira kwa vijana waliojiajiri kwenye bodaboda kama fursa badala yake watumie majukwaa hayo kutoa mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana nchini.