Leseni za migodi 470 ya madini ya Tanzanite mbioni kufutwa

Mirerani. Leseni za wamiliki 470 wa migodi ya madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara zipo mbioni kufutwa kutokana na kudaiwa Sh700 milioni za ada ya leseni za mwaka fedha wa 2021/22.

Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Fabian Mshai ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau mbalimbali na wamiliki wa migodi na wachimbaji wa madini ya Tanzanite.

Mshai amesema kutokana na hali hiyo ofisi yake imetoa siku 30 kwa kila mdaiwa kufanya malipo hayo la sivyo watafutiwa leseni na kufikishwa mahakamani.

“Wale wote watakaoshindwa kulipa madeni yao watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ya madini sura 123 pamoja na marekebisho yake,” amesema Mshai.

Amewataka wadaiwa hao kufika kwenye ofisi yake wakiwa na nyaraka za leseni halisi ya uchimbaji wa madini na risiti za malipo ikiwa mdaiwa amelipa madeni yake.

“Hivi sasa muda wa kulalamika na kuomba watu walipe madeni yao ili hali wanafahamu kuwa wanadaiwa umekwisha, inabidi tufuate sheria, kanuni na taratibu,” amesema Mshai.

Amewasihi wachimbaji hao wasijione wanyonge kwani wanapaswa kutumia fursa ya uwepo wa rasilimali wa madini ya Tanzanite na kuondokana na hali hiyo.

Hata hivyo, mmoja kati ya wamiliki wa mgodi wa Tanzanite wa kitalu B (Opec), Mwanaidi Kimu amesema wachimbaji wengi wanakabiliwa na ukata hivyo kushindwa kulipa ada za leseni.

“Tuangalieni na sisi kwani ni wanyonge na tunashindwa kuchimba madini ipasavyo kutokana na kukosa fedha za kuendeshea migodi, tunaomba tusifutiwe leseni,” amesema Kimu.