Lindi kuandikisha wapiga kura 768,641

Muktasari:
- Mkoa wa Lindi unatarajia kuandikisha wapiga kura 768,641, ambapo ni ongezeko la wapiga kura wapya 121,187 sawa na asilimia 18.7 kutoka wapiga kura 645,644 wa mwaka 2020 waliopo kwenye Daftari la Wapiga Kura.
Lindi. Kufuatia kuwepo kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini, Mkoa wa Lindi unatarajia kuandikisha wapiga kura 768,641 kwa mwaka 2025.
Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa Mkoa wa Lindi utaanza rasmi Januari 28 hadi Februari 3, 2025.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Januari 16, 2025 kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari hilo mkoani hapa, Kaimu Mkurugenzi Tume ya Huru ya Taifa Uchaguzi, Giveness Aswile amesema kuwa mkoa huo unatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 121,187 sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 645,644 wa mwaka 2020.
“Mkoa wa Lindi unatarajia kuandikisha wapiga kura 768,641, ambapo ni ongezeko la wapiga kura wapya 121,187 sawa na asilimia 18.7 kutoka wapiga kura 645,644 wa mwaka 2020 waliopo kwenye Daftari la Wapiga Kura,” amesema Aswile.
Aidha, Aswile amewaomba viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kujitokeza katika kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.
"Tunawategemea sana viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kujitahidi kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili tuweze kufikia malengo," amesema Aswile.

Awali akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk amesema kuwa ni kosa la jinai mwananchi kujiandikisha zaidi ya mara moja.
"Ni kosa la jinai mwananchi kujiandikisha zaidi ya mara moja, ukibainika unaweza kufungwa jela miezi sita au miaka miwili, hivyo ili kujiepusha na kadhia hii, hakikisha unajiandikisha mara moja tu," amesema Jaji Mbarouk.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu uandikishaji huo, baadhi ya wananchi wamepongeza utaratibu ulioandaliwa kuhakikisha kuwa wanadaandikishwa.
Zuhura Meza Mkazi wa Lindi mwenye mahitaji maalumu, ameishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele watu wenye uhitaji ili nawao waweze kwenda kuhamasisha wenzao kujitokeza kwenda kuboresha taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura.
"Naishukuru Serikali na watu wa tume kwa kutuona sisi tuliokuwa na uhitaji, elimu niliyoipata itanisaidia kwenda kuhamasisha wenzangu ili kuweza kujitokeza kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura," amesema Meza.
Saidi Omary Mwenyekiti wa wazee Mkoa wa Lindi amesema watajitahidi kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kujitokeza kujiandikisha.
"Sisi kama wazee tutajitahidi kuhamasisha wananchi wetu ilikuweza kufikia malengo ya Tume kuandikisha wapiga kura 768,641kwa mkoa wa Lindi."Amesema Omary.