Lissu amjibu Ndugai gharama za matibabu yake
Muktasari:
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu leo Alhamisi ametoa ufafanuzi wa fedha anazolipwa na Bunge la nchi hiyo.
Dar es Salaam. Tundu Lissu amesema Bunge la Tanzania halijawahi kutoa hata senti moja kugharamia matibabu yake.
Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 31, 2019 saa chache tangu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kusema Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni zikiwa stahiki zake na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu kwake.
Lissu amekiri kulipwa Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.
Ametoa sababu tatu ambazo Spika Ndugai alizitoa Aprili mwaka jana, kwamba Bunge haliwezi kulipia gharama za matibabu yake.
Lissu amezitaja sababu hizo kuwa hawajapata barua ya kibali ya madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili; hawajapata barua ya kibali cha Katibu Mkuu Wizara ya Afya; na tatu hawajapata barua ya kibali cha Rais (John) Magufuli kuidhinisha malipo hayo.
“Sasa anaposema wamenilipa pesa hizo anapaswa kuulizwa, je, ni lini walipata barua hizo tatu za vibali?” amehoji Lissu na kuongeza:
“Ukweli pekee uliopo ni kwamba Bunge halijawahi kunilipa hata senti moja ya gharama za matibabu yangu. Hata senti moja!”
Amesema pesa pekee aliyolipwa ni mshahara na posho zake za kila mwezi kama mbunge tu ambazo wanalipwa wabunge wote, waliopo bungeni au hospitalini.
“Hata Spika Ndugai mwenyewe alipougua na kulazwa India kwa zaidi ya miezi sita mwaka 2016, alilipwa mshahara na posho zake za kila mwezi. Hiyo siyo pesa ya gharama za matibabu,” amesema Lissu aliyeko Ubelgiji kwa matibabu.