Lissu ataja mambo matano aliyozungumza na Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu walipokutana jijini Brussels nchini Ubelgiji.

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ametaja mambo matano aliyozungumza na Rais Samia nchini Ubeligiji, ikiwemo kesi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameeleza mambo mbalimbali ambayo amezungumza na Rais Samia Suluhu Hassan walipokutana huko Brussels, Ubelgiji ikiwemo kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Rais Samia yuko nchini humo kwa ziara ya kikazi wakati Lissu anaishi Ubelgiji. Lissu alitumia fursa hiyo kuomba kuonana na Rais, akakubaliwa na wawili hao wamefanya mazungumzo kwa saa moja.

Rais Samia akutana na Tundu Lissu

Akizungumzia mambo aliyoyazungumza na Rais Samia, Lissu amesema alimweleza kwamba kesi inayomkabili Mbowe na wenzake haina manufaa yoyote kwake na kwa taifa kwa ujumla.

"Nimemwambia Rais wetu, hiyo kesi haiisaidii nchi yetu, haiisaidii serikali yake, haikisaidii chama chake, haikisaidii chama chetu. Inamuumiza mwenyekiti wetu na familia yake, inawaumiza walinzi wake na familia zao.

"Nimemwambia Rais afanye analoweza kufanya kwa mamlaka yake kama Rais, ahakikishe kwamba hii kesi inaondolewa Mahakamani, hakuna sababu yoyote ya kuendelea na kesi ambayo kila mtu anaona na ushahidi unaonyesha Mahakamani kwamba ni mambo ya kuungaunga," amesema Lissu.

Lissu amesema amemweleza Rais Samia kuhusu zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, amemwomba afute katazo hilo ili sheria ifuatwe.

Pia, amesema amemweleza Rais kuhusu suala la katiba mpya huku akimwambia kwamba ana fursa ya kuipatia Tanzania katiba mpya na mfumo wa kidemokrasia ambao utatenda haki hasa kwenye chaguzi.

Rais Samia Suluhu Hassan alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu jijini Brussels nchini Ubelgiji.

"Nimemwambia Rais kwamba mjadala wa katiba mpya utakuwa ni mjadala mrefu lakini ni muhimu tujadili masuala haya," amesema Lissu kwa njia ya mtandao akiwa Ubelgiji.

Jambo jingine amesema ni kuhusu haki zake alizonyimwa baada ya kuvuliwa ubunge. Amemwomba Rais ashughulikiwe hilo kwa maana yeye ni mbunge pekee ambaye hakupokea kiinua mgongo chake.

"Nimemwambia Rais kwa vile ana mamlaka hayo, alishughulikie suala hilo, na amelichukua," amesema Lissu.

Vilevile, mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, amemweleza Rais Samia juu ya azma yake ya kutaka kurudi nchini lakini amemwomba Rais Samia amhakikishie usalama wake kwa kutamka wazi kwamba atakuwa salama ili kumtoa wasiwasi. Amesema Rais Samia amemwambia atalifanyia kazi.