Lissu: Wananchi msikubali wagombea kuenguliwa kirahisi uchaguzi ujao

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Bara,Tundu Lisu akizungumza na wananchi wa Kiomboi kwenye mkutano wake wa hadhara na wakazi wa eneo hilo.

Muktasari:

  • Lissu amewataka wananchi kujipanga kwa  uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na kutokubali kuenguliwa viongozi wao kirahisi na wanapaswa kujifunza kupitia uchaguzi kama huo wa mwaka 2019. 

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Bara, Tundu Lissu amewataka wananchi kutokubali wagombea wao kuenguliwa kirahisi kwenye  uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

 Amesema wananchi kama kujifunza walishapata somo zuri kwenye uchaguzi uliopita wa ngazi hiyo uliofanyika mwaka 2019, ambapo amedai kuwa walienguliwa wagombea  wote wa vyama vya upinzani.

“Huu ni ujumbe wangu kwa leo. Wajinga ndio waliwao, watakapowaengua wagombea wenu na mkakubali, makosa yatakuwa ya kwenu,” amesema.

Lissu amesema hayo leo  Jumapili Juni 2, 2024  wakati akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida katika mkutano wa hadhara. Mkutano huu ulitanguliwa na alioufanya Kinampanda jimbo la Iramba Magharibi.

“Huu mji wa Kiomboi kuna mtaa hauna mwenyekiti wa CCM, au wilaya hii kuna kijiji ambacho hakina mtu wa CCM, ninavyojua katika uchaguzi wa mwaka 2019 uchaguzi haukufanyika kabisa wapinzani wote walioenguliwa,” amesema makamu mwenyekiti huyo.

Amesema wanachopaswa kukifanya wananchi katika chaguzi hizo ni kuchagua viongozi wanaokubalika katika kila nafasi inayotakiwa na kuwasaidia wagombea wa Chadema kwa kuwapigia kampeni kwa sababu wakishinda, watakuwa wanafanya kazi ya wote na si shughuli zao binafsi.

“Mfano sisi Singida tunatambulika kwa sifa mbili, kwanza ni mkoa masikini kuliko yote nchini na hatuchekani na Dodoma na tunadharauliwa kwa umasikini wetu na pili tunajulikana kwa ujinga wetu, tumekuwa tukiwapigia kura CCM na wanatuchakaza kila mara. Tunapaswa tuchague viongozi wetu watusaidie,” amesema.

Amesema mwezi ujao Tume ya Uchaguzi itaanza  kuandikisha wapigakura hivyo hawapaswi kulala kwa kuwa watatumia wiki moja.

“Wito wangu himizaneni wote wenye umri wa miaka 18 wapate kitambulisho cha kupiga kura vinginevyo mtakuja kuamshwa siku za kiama,” amesema Lissu. 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Hashim Juma amezungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akisema hauna faida kwa pande zote, bali wanaonufaika ni viongozi wakubwa.

Juma amesema ni jambo lisilofichika umaskini unaoendelea kutamalaki kwa pande zote, chimbuko lake ni muungano huo huku akiwataka wananchi hao kuonyesha hasira na hisia zao kwenye sanduku la kura kuichagua Chadema.

Awali, Askofu Maximilian Machumu maarufu 'Mwanamapinduzi' amesema Baba wa Taifa, Julius Nyerere alisema ili nchi ipige hatua kimaendeleo lazima iwe na ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora.

“Ukimuona mtu anakunyang’anya ardhi ujue hakutakii mema, ukiona kiongozi anaiuza basi tambueni miaka ijayo tutakuwa watumwa kwani hatutakuwa na urithi tena,” amesema.

Amesema uchaguzi unaokuja ni kati ya dhuluma na haki, huku akiwataka wananchi kuchagua haki kwa kuwa utakuwa msingi katika kulinda urithi wao.