Lukuvi: Marufuku 'tozo' za madalali

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepiga marufuku kitendo cha madalali wa nyumba kutoza fedha sawa na kodi ya mwezi mmoja kwa wapangaji wanapo watafutia makazi au maeneo ya biashara.


Mufindi. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepiga marufuku kitendo cha madalali wa nyumba kutoza fedha sawa na kodi ya mwezi mmoja kwa wapangaji wanapo watafutia makazi au maeneo ya biashara.

Kwa muda mrefu madalali wamekuwa wakitoza fedha sawa na malipo ya mwezi mmoja ama kutoka kwa wapangaji, wenye nyumba au kotekote.

Lukuvi ambaye hakusema ni kiasi gani madalali wanatakiwa kulipwa au utaratibu upi utumike, amesema huo ni wizi kama wizi mwingine.

Amesema hakuwahi kulijua jambo hilo mpaka jana lilipoibuka kwenye mjadala kuhusu madalali wanaowaumiza wakulima, wanunuzi na wawekezaji kwenye sekta ya misitu.

Wakati Lukuvi akipiga marufuku, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro yeye alitoa wiki mbili kuanzia jana kwa wataalamu wa wizara yake kuanzisha mpango wa kusajili madalali wote walio kwenye sekta ya misitu, ili watambuliwe.

Lukuvi alikuwa akifunga kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya misitu mkoani Iringa ambalo liliwakutanisha wavunaji na wawekezaji zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi.

“Hawa wanaochukua kodi ya mwezi mmoja ni majambazi, wizi huu ukome na ni marufuku mpangaji kumlipa dalali. Watasema itawezekanaje, wao waendelee tu na wananchi wengi wanayo namba yangu,” amesema Lukuvi na kuendelea.

“Mimi nakomesha jambo hili leo, na tulishasema kodi ni ya mwezi mmojammoja si miezi 12. Fikiria mtu analipa kodi ya miezi 12 halafu anamlipa dalali mwezi mmoja, yaani miezi 13 ni mwaka gani una miezi 13?”