Maadhimisho ya uhuru kufanyika kilele cha Kilimanjaro
Muktasari:
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), Imani Kikoti amesema maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika yatafanyika katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
Moshi. Wakati maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika yakiadhimishwa kila mwaka ifikapo Desemba 9, mwaka huu maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika kilele cha uhuru, katika mlima Kilimanjaro.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 16 na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa KINAPA, Imani Kikoti wakati akipokea timu ya wafanyakazi sita wa benki ya NMB waliopanda mlima Kilimanjaro kwa siku saba kwa ajili ya kupandisha bendera katika kilele cha uhuru ikiwa ni siku ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
Wafanyakazi hao wa benki ya NMB walianza safari ya kupanda mlima huo kuanzia Oktoba 8 mwaka huu kupitia geti la Machame ambapo baada ya kusimika bendera katika kilele cha uhuru walishuka kupitia geti la Mweka liliopo wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
"Mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kwenye kilele cha uhuru, nitoe wito kwa Watanzania wote kushiriki katika maadhimisho haya.
"Najua kila mtu anafahamu historia ya kilele cha uhuru pamoja na uhuru wa nchi yetu, kwa hiyo kutakuwa na utaratibu wa kupanda mlima kwa Watanzania wote, taasisi za serikali na binafsi na utaratibu kamili utatolewa," amesema.
Kikoti ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kupanda mlima huo ili kushereka maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika na kwamba kufanya hivyo ni uzalendo na ni fursa katika kutangaza utalii wa ndani.
"Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunadhihirisha uzalendo na ukirudi nyuma mwaka 1961 wakati tunapata uhuru kapteni Nyirenda ndio alikabidhiwa mwenge na bendera ya Taifa aipandishe kwenye kilele cha uhuru na kufikisha bendera ile pale, huu ulikuwa ni uzalendo mkubwa," amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa benki ya NMB kanda ya Kaskazini, Dismass Prosper amesema kupanda mlima ni moja ya uzalendo katika Taifa na kwamba wao kama benki wameamua kwenda kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja katika mlima Kilimanjaro.