Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makosa ya familia matumizi ya dawa za meno

Muktasari:

  • Watu wengi huchukua dawa moja tu kwa ajili ya kila mtu nyumbani, wakiamini kazi ya dawa zote za meno ni moja tu yaani kusafisha meno.



Dar es Salaam. Mzazi anapokwenda dukani au kuagiza dawa ya meno kwa ajili ya familia mara nyingi huangalia bei, ladha au chapa anayoifahamu. 

Wengine huchukua dawa moja tu kwa ajili ya kila mtu nyumbani, wakiamini kazi ya dawa zote za meno ni moja tu yaani  kusafisha meno.

Shedrack Jackson, mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, anasema mara zote hununua dawa moja kwa ajili ya familia yake.

"Dawa ni dawa tu, mimi nachukua dawa kubwa na tunatumia wote nyumbani, sioni kama kuna utofauti wowote, hata tunapokwenda kununua hatuambiwi zipo za aina mbili kwako ndio nasikia, anasema na kuongeza:

"Kama ipo elimu inapaswa kutolewa kwa kweli kwa sababu sote tunatumia aina moja tu, tukiamini ukimwekea mtoto dawa kidogo ndio inavyotakiwa kumbe wana aina yao.’’

Wataalamu wa afya ya kinywa na meno wanasema, mtazamo huo wa kina Jackson, unakuwa chanzo cha matatizo ya afya ya meno kwa watoto na hata watu wazima.


Tofauti ya dawa

Ukweli ni kwamba dawa ya meno ya mtoto na ile ya mtu mzima si kitu kimoja. Tofauti kubwa ipo kwenye kiwango cha madini ya Fluoride; kiungo muhimu kinacholinda meno dhidi ya kuoza na kutoboka.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza magonjwa ya kinywa na meno yanaendelea kuwa tatizo kubwa la afya duniani, yakikadiriwa kuwaathiri watu wengi zaidi.

Aidha, kuoza meno ndiyo ugonjwa usioambukiza unaowaathiri watu wengi zaidi duniani, ukiwakumba takribani watu bilioni 2.5.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa afya ya meno si suala la mwonekano pekee, bali ni sehemu muhimu ya afya ya binadamu.

Katika dawa zote za meno, Fluoride ndiyo madini yanayofanya kazi kubwa ya kuimarisha meno na kuyalinda dhidi ya mashambulizi ya bakteria wanaosababisha kuoza.

Daktari wa kinywa na meno wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbeya (Mbeya COHAS), Flaviana Nyatu, anasema watu hawafahamu kuwa kiwango cha Fluoride kinachohitajika kwa mtoto ni tofauti na kile cha mtu mzima.

“Dawa ya meno ya watoto walio chini ya miaka mitano inapaswa kuwa na Fluoride ya 1,000 ppm, wakati dawa ya watu wazima inatakiwa kuwa na kati ya ppm 1,450 hadi 1,500,” anasema.

Kwa mujibu wa daktari huyo, tofauti hiyo imewekwa kisayansi ili kuendana na mahitaji ya mwili katika kila hatua ya ukuaji.

Dk Nyatu anataja sababu ni kwamba watoto wadogo bado hawajakomaa katika matumizi ya dawa za meno. Wakati wa kupiga mswaki, wengi wao humeza sehemu ya dawa badala ya kuitema.

Hali hiyo anasema husababisha mwili wao kupokea kiwango kikubwa cha Fluoride kuliko kinachohitajika, ikiwa watatumia dawa ya meno ya watu wazima.

Akifafanua zaidi hilo, daktari wa kinywa na meno wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Isaya Magombola, anasema matumizi ya muda mrefu ya Fluoride nyingi,  yanaweza kusababisha ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Dental Fluorosis.

“Dental Fluorosis hutokea mtoto anapopata Fluoride nyingi wakati meno yake yanapokua. Hali hii husababisha mabadiliko ya rangi na mwonekano wa meno, ambao watu wengi huifahamu kama meno ya kichaga,” anasema.

Kwa upande mwingine, anasema mtu mzima akitumia dawa ya meno ya watoto, hapati madhara ya moja kwa moja, lakini kiwango kidogo cha Fluoride hupunguza uwezo wa meno kujikinga dhidi ya kuoza.

“Meno ya mtu mzima yanahitaji kiwango kikubwa zaidi cha Fluoride. Akitumia dawa ya mtoto kwa muda mrefu, kinga dhidi ya kuoza inapungua na uwezekano wa kupata matundu huongezeka,” anafafanua Dk Magombola.


Familia, dawa mbili za meno

Kutokana na tofauti hizo, wataalamu wanashauri familia zenye watoto chini ya miaka mitano kuwa na aina mbili za dawa za meno.

Kwa mujibu wa Dk Nyatu, dawa ya mtoto na dawa ya mtu mzima zinapaswa kutumika sambamba pale mtoto atakapofikisha angalau miaka sita.

“Watoto wakifikisha miaka sita na kuendelea wanaweza kutumia dawa ya meno ya watu wazima yenye kiwango cha Fluoride kinachopendekezwa,” anasema.

Anawashauri wazazi kuzoea kusoma maelezo yaliyoandikwa kwenye vifungashio kabla ya kununua bidhaa hizo.

Miongoni mwa mambo ya kuangalia ni kiwango cha Fluoride kilichoandikwa kwa mfumo wa ppm na umri uliopendekezwa kwa mtumiaji.

Daktari wa magonjwa ya meno, Dk Iddi Mnyonge  anasema inashauriwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku lengo kuondoa mabaki ya chakula mdomoni.

Anasema mtu huanza kupata athari endapo kutatokea mzunguko wa saa 24 na kuendelea kama mabaki ya chakula hayataondolewa mdomoni.

Mtu anatakiwa kupiga mswaki kabla ya kunywa chai na usiku kabla ya kulala,angalau mara mbili kwa siku ili mabaki ya chakula yasikae mdomoni.

Anasema hilo linahusu watoto na watu wazima, kwani chakula kinapokaa mdomoni kwa muda hutengeneza tindikali itakayounguza meno na kuumiza fizi.

Naye anasisitiza kuwa dawa ya watoto ya meno na watu wazima lazima zitofautiane kulingana na kiwango cha kemikali ya floradie iliyowekwa kwenye dawa hizo.

Ukubwa wa changamoto

Pamoja na maendeleo ya huduma za afya, takwimu zinaonyesha kuwa matatizo ya meno bado ni changamoto kubwa nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2022/2023, watu 541,159 waliripotiwa kuwa na meno yaliyooza.

Kati ya hao, watu 174,749 sawa na asilimia 32.3 walizibwa meno, huku watu 323,419 sawa na asilimia 59.8 wakilazimika kung’olewa meno.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi hufika hospitalini wakati tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kutoweza kuokoa jino.

Akizungumza katika mkutano wa   Tanzania Dental Expo 2026 wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno wa Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo, alisema asilimia 76.5 ya watu wazima nchini wameoza meno.Kwa upande wa watoto, alisema asilimia 31 tayari wameathiriwa na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Dk Nzobo, hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuimarisha elimu ya afya ya kinywa na matumizi sahihi ya bidhaa za meno kuanzia ngazi ya familia ikiwamo matumizi sahihi ya dawa za mswaki.

Wataalamu wanaeleza hata dawa bora ya meno haiwezi kutoa matokeo mazuri ikiwa haitatumika kwa njia sahihi.


Mswaki gani sahihi kwako?

Taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Rochester Medicine nchini Marekani zinaeleza kuwa mswaki unaofaa unapaswa kuwa na nyuzi laini, kichwa kidogo na mpini unaowezesha kushikika vizuri.

Aidha, kutumia nguvu nyingi wakati wa kupiga mswaki kunasababisha fizi kurudi nyuma na kuharibu tabaka la nje la meno.

Chama cha Madaktari wa Meno Marekani (ADA) kinashauri watu kupiga mswaki kwa angalau dakika mbili mara mbili kwa siku, bila kujali kama wanatumia mswaki wa kawaida au wa umeme.


Sukari  ni adui 

Licha ya umuhimu wa Fluoride, wataalamu wanasema mapambano dhidi ya kuoza kwa meno hayawezi kufanikiwa bila kudhibiti matumizi ya sukari.

WHO inaeleza kuwa matumizi makubwa ya sukari ndiyo chanzo kikuu cha ugonjwa wa meno kuoza duniani.

Shirika hilo linashauri ulaji wa sukari usizidi asilimia 10 ya mahitaji ya nishati kwa siku, huku kiwango cha chini ya asilimia tano kikitajwa kuwa bora zaidi kwa afya ya meno.

Kwa watoto chini ya miaka miwili, WHO inapendekeza kuepuka kabisa vinywaji vyenye sukari iliyoongezwa.