Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umuhimu wa mazoezi kwa mama aliyejifungua

Muktasari:

  • Baada ya ujauzito na kujifungua, mwili wa mama hupitia mabadiliko makubwa ambayo huhitaji muda na mbinu sahihi ili kurejea katika hali yake ya kawaida.



Dar es Salaam. Ni saa kumi na moja alfajiri katika eneo la Kivule jijini Dar es Salaam. Kwenye uwanja wa mpira katika Shule ya Msingi Misitu kinamama kadhaa wamekusanyika kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.

Miongoni mwao yupo Aisha Jumanne (35), ambaye miezi minne iliyopita alijifungua mtoto wake wa pili.

Anasema baada ya kujifungua alikuwa akihisi uchovu wa mara kwa mara, maumivu ya mgongo na kukosa nguvu za kutosha kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Hata hivyo, baada ya kuanza kufanya mazoezi mepesi kwa ushauri wa wataalamu wa afya, hali yake ilianza kubadilika.

"Nilianza kwa kutembea dakika 15 kila siku, baadaye nikawa naongeza muda taratibu. Sasa najisikia mwepesi, nina nguvu zaidi na hata usingizi wangu umeimarika," anasema Aisha.

Wataalamu wa afya wanasema uzoefu wa Aisha ni wa kawaida kwa wanawake wengi wanaojifungua. Baada ya ujauzito na kujifungua, mwili wa mama hupitia mabadiliko makubwa ambayo huhitaji muda na mbinu sahihi ili kurejea katika hali yake ya kawaida.

Muuguzi na mkunga mkuu, Priscus Kilawe kutoka Hospitali ya Qualitas, anasema mazoezi ni sehemu muhimu ya mchakato wa kupona baada ya kujifungua kwa sababu husaidia mwili kurejesha nguvu na uwezo wake wa kawaida.

"Ujauzito na kujifungua huathiri misuli ya tumbo, mgongo na nyonga. Mazoezi yanapofanyika kwa usahihi husaidia kuimarisha maeneo hayo na kupunguza baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya kujifungua," anasema.

Anabainisha kuwa moja ya faida kubwa za mazoezi ni kuboresha mzunguko wa damu mwilini. Hali hiyo husaidia virutubisho na oksijeni kufika kwa urahisi katika sehemu mbalimbali za mwili, jambo linalochangia kupona kwa haraka.

Mbali na afya ya mwili, mazoezi yana mchango mkubwa katika afya ya akili. Kipindi cha baada ya kujifungua huambatana na mabadiliko ya homoni ambayo wakati mwingine husababisha huzuni, msongo wa mawazo au hali ya kukosa hamasa.

Muuguzi Kilawe anasema mazoezi huchochea utolewaji wa homoni zinazojulikana kama ‘endorphins’ ambazo husaidia kuboresha hali ya furaha na kupunguza msongo wa mawazo.

Hivyo anashauri familia kusimamia na kuratibu ratiba ya mazoezi ya mama aliyejifungua ili kurudisha afya na kinga ya mwili wake.

"Tunaona baadhi ya kinamama wakikumbwa na mfadhaiko baada ya kujifungua. Mazoezi imara yataisaidia kumrudisha mama katika hali yake, yanaweza kusaidia kuboresha hali ya kihisia na kuongeza utulivu wa akili. Ni wajibu wa familia sasa kusimamia ratiba za mazoezi kwa mama aliyejifungua, maana akifanya bila usimamizi hatayazingatia sana," anasema.

Kwa mujibu wa wataalamu, mazoezi pia husaidia kurejesha nguvu za misuli ya nyonga ambayo huwa imeathirika kutokana na ujauzito na kujifungua. Misuli hiyo ina umuhimu mkubwa katika kudhibiti kibofu cha mkojo na kuunga mkono viungo vya ndani vya uzazi.

Mazoezi ya pelvic floor, maarufu kama Kegel exercises, yanatajwa kuwa miongoni mwa mazoezi muhimu zaidi kwa wanawake waliojifungua.

Mazoezi hayo husaidia kuimarisha misuli ya nyonga na kupunguza changamoto ya kuvuja kwa mkojo, ambazo huwapata baadhi ya wanawake baada ya kujifungua.

Aidha, mazoezi huchangia kurejesha uzito wa mwili kwa njia salama. Ingawa wataalamu wanasisitiza kuwa lishe bora ndiyo msingi wa afya baada ya kujifungua, kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia mwili kutumia nishati kwa ufanisi na kupunguza mafuta yaliyokusanyika wakati wa ujauzito.


Tahadhari

Hata hivyo, wataalamu wanatahadharisha kuwa si kila mama anapaswa kuanza mazoezi mara moja baada ya kujifungua.

Waliopitia upasuaji wa kujifungua au waliopata matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua, wanapaswa kupata ushauri wa daktari kabla ya kuanza mazoezi.

"Kinachoshauriwa ni kuanza taratibu kwa mazoezi mepesi kama kutembea, kujinyoosha na mazoezi ya kupumua. Kadiri mwili unavyoendelea kupona, ndipo kiwango cha mazoezi kinaweza kuongezwa," anasema Priscus.

Anasisitiza kuwa lengo si kurejesha mwonekano wa mwili kwa haraka, bali kuhakikisha mama anarejea katika afya njema na kupata nguvu za kutosha za kumlea mtoto wake.

Kwa wanawake wengi, safari ya kurejea katika hali ya kawaida baada ya kujifungua inaweza kuonekana ndefu na yenye changamoto.

Hata hivyo, wataalamu wanaamini kuwa kwa kuzingatia lishe bora, kupumzika vya kutosha na kufanya mazoezi kwa usahihi, mama anaweza kuharakisha mchakato wa kupona na kufurahia afya bora katika kipindi muhimu cha malezi ya mtoto mchanga.