Maaskofu wataja sababu watu kuiba kura, kusaka vyeo

Muktasari:

  • TEC katika ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2024, imetaja mambo iliyoyaita  donda ndugu kwa nchi za Afrika.

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetaja sababu mbili za watu kusaka vyeo, kuiba kura na kukatisha maisha ya wengine, ikiwamo watu hao kutolifahamu neno la Mungu.

Sababu nyingine imetajwa ni tamaa mbaya za kisiasa ambazo mwelekeo wake ni kulinda masilahi binafsi na ulafi wa madaraka.

Hayo yameandikwa kupitia ujumbe wa Kwaresima wa 2024 uliotolewa na TEC leo Februari 12, 2024 ukiwa na kichwa kisemacho ‘Nitawezaje kuelewa mtu asiponiongoza’.

Wizi wa kura na kukatisha maisha ya watu wengine  TEC imeyataja mambo hayo kuwa ni donda-ndugu kwa nchi za Afrika na yamekuwa yakisababisha migogoro ya kivita na mapambano ya kiitikadi.

“Mipasuko ya kisiasa ndani ya jamii huweza kutokea kwa sababu ya kikundi kimoja kujiona bora kuliko kingine, wakati mwingine kujiona kiko juu ya sheria mbalimbali za nchi. Matokeo ya haya yote ni kufarakana kijamii, lawama zisizoisha na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa jamii husika,” wamesema maaskofu katika ujumbe huo.

TEC imewakumbusha wananchi kuwa uongozi, madaraka au mamlaka yoyote ni dhamana kutoka kwa Mungu.

Dhamana hiyo wamesema hupewa kiongozi kama mwakilishi wa Mungu katika kuongoza watu wa Mungu.

“Daima, viongozi wafahamu kuwa wamepewa dhamana na Mungu kwa ajili ya wale wanaokabidhiwa (rejea Warumi 13:1), mafanikio ya kiongozi ni pale anapomtegemea Mungu kabisa,” unaeleza ujumbe huo.

Suluhisho la hayo, TEC imesema Kanisa linaamini kiongozi yeyote (halali) anatoka kwa Mungu (Rum 13:1b).

Kuhusu namna ya kuongoza kwa uadilifu, TEC imeeleza hutegemeana na uwezo alionao mtu huyo na hofu yake kwa Mungu.

“Siasa ni sauti ya watu kwa ajili ya watu wenyewe, bila shaka hawawezi kuitoa sauti ambayo wao wenyewe hawana, ikiwa siasa inafikiriwa na kuchukuliwa katika maana ya ‘siasa ni viongozi’ basi tutaendelea kuyashuhudia mengi yasiyo halali, haki wala adilifu,” umesema ujumbe huo.

TEC imesema uongozi ni kudumisha na kuendeleza yaliyo mema na kukemea yaliyo maovu na kuyasahihisha.

“Tunakumbushwa daima kuwa cheo ni dhamana, na Yesu katika Maandiko Matakatifu amesema kuwa ukitaka kuwa mkubwa huna budi kuwa mtumishi (rejea. Mt 20:26),” TEC imesema.

Maaskofu wamesisitiza fadhila ya unyenyekevu ni muhimu kwa viongozi na wananchi kuwa tayari kupokea na kutenda kadiri ya maelekezo ya ujumbe wa Kwaresima 2024, ya Mungu na Roho Mtakatifu kupitia neno la Mungu.


Kuhusu mazingira

Ujumbe wa TEC umeeleza kutolinda mazingira kumesababisha kutenda mambo yanayoathiri uumbaji wa Mungu.

“Vitendo vinavyosababisha  kuchafua hewa kwa njia ya moshi, vinavyoongeza joto, ni kama milipuko ya mabomu, shughuli za viwandani, uchomaji wa mapori na miti ovyo, matokeo yake ni maangamizi ya watu, wanyama na mimea, kutokana na kupanda kwa joto na kukosa hewa safi.

Baraza limesema, matukio mengine yanayosababisha uchafuzi wa maji au ukaushwaji wa vyanzo vya maji ni utupaji ovyo wa taka kwenye vyanzo vya maji na kufanya shughuli zingine za kibinadamu bila kujali kanuni za utunzaji wa vyanzo vya maji.

Matokeo yake ni kukosa maji safi na salama kwa matumizi ya viumbe hai.

Pia wamezungumzia ukataji holela wa miti, kutopumzisha ardhi, na idadi kubwa ya mifugo kwenye eneo moja husababisha kutifuliwa ardhi hivyo kuwapo mmomonyoko wa udongo.