Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TEC: Tume huru kurejesha imani katika chaguzi

Baadhi ya viongozi wa dini na vyama vya siasa wakifuatilia mkutano wa kupokea taarifa ya uzoefu wa Tume ya uchaguzi Kenya na Afrika ya Kusuni uliofanyika kwenye ukumbi wa baraza la maaskofu (TEC).

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wamekuwa wakiona mapungufu mengi yakijitokeza katika chaguzi mbalimbali zilizopita nchini.

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limeshauri mabadiliko ya kisheria, kimuundo na kimfumo ili kupata tume huru ya uchaguzi ambayo itaondoa mapungufu yanayojitokeza katika uchaguzi mbalimbali zilizopita.

Akizungumza leo Novemba 17, 2023; na wadau wa siasa nchini, Katibu Mkuu wa baraza hilo, Dk Charles Kitima, amesema uwepo wa tume huru ya uchaguzi nchini, utarejesha imani ya Watanzania katika chaguzi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa TEC, baraza hilo limekuwa likiona mapungufu mengi yakijitokeza katika chaguzi zilizopita, jambo lililowasukuma kujifunza kutoka mataifa mengine, ambapo Kenya na Afrika Kusini ndizo nchi zilizotembelewa katika ziara hiyo ya mafunzo.

“...kwa mujibu wa ripoti ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 na 2020 tuliona mambo hayakuwa mazuri kwani kulikuwa na mapungufu mengi. Kama viongozi wa dini tunapenda watu washiriki katika kujitawala, ibara ya 21 ya Katiba...inaeleza raia wote ikiwa ni pamoja na sisi taasisi, tuna haki ya kushiriki masuala yote yanayohusi nchi yetu," amesema na kuongeza;

"Kwa mantiki hiyo sisi huwa tinajihusisha pia na mambo yanayofanyika kwenye siasa kila mtu ashiriki asiwepo mtu anayejiona amebaguliwa, ametengwa au kunyanyaswa. Sasa kuzingatia mapungufu tuliyoyaona, tuliamua kuanza na dhana ya kutafakari kwani bila uchaguzi huru na haki, huwezi kuwa na viongozi wanaokubalika kutawala wananchi.”

Dk Kitima ambaye licha ya kuwa Kasisi katika Kanisa Katoloki, pia ni mbobezi wa mambo ya sheria na amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut), amesema kuwa TEC ilihitaji kuangalia na kujifunza kutoka mataifa ambayo hufanya chaguzi za haki kutokana na kuwa na tume ambazo zinakubalika.

"Ni kwanini sisi tulikuwa na uchaguzi usioridhisha wengi? Serikali kupitia ahadi za Rais, imeonyesha kwamba sheria zetu hazijakaa vizuri katika kutekeleza masuala ya chaguzi nchini, tume ya uchaguzi ndiyo waratibu wakubwa wa uchaguzi," amesema.

Padre Kitima alitumia nafasi hiyo ya kukutana na wadau siasa nchini na kubainisha kuwa: “...miswada iliyoletwa inahitaji kuwafanya watu kuwa na uelewa wa maana ya uchaguzi na mratibu wa uchaguzi, ahadi zilizoletwa na Rais zinaonyesha nia nzuri...lakini inapaswa kuangalia mambo ya msingi yanayohusiana na uchaguzi.”

Miswada hiyo ni pamoja na ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Ananilea Nkya amesema inawezekana kufanyika uchaguzi huru na wa haki na wananchi kupata viongozi wanaowataka. Hii inatokana na mafunzo aliyoyapata katika nchi za Kenya na Afrika Kusini.

“Nimejifunza kwenye tume za uchaguzi za Kenya na Afrika ya Kusuni, namna ambavyo wananchi katika nchi hizo, kuanzia ngazi ya chini walivyona imani kubwa kwenye tume kuliko Serikali zao. Kama Tanzania tutaweza kuwa na tume huru kama hizo naamini Watanzania wengi watarudisha imani kwenye uchaguzi,” amesema na kuongeza;

“Unajua hivi sasa kunai le hali ya watu wengi kuona hakuna sababu ya uchaguzi kutokana na yule anayechaguliwa hatangazwi kuwa ameshinda. Wenzetu tume zao zinaaminika kwa namna wajumbe wanavyopatikana, hawachaguliwi na mtu; Mkurugenzi huomba kazi na kufanyiwa usaili bila kushinikizwa kufanya lolote na chama au mgombea.”

“Mimi kwangu naona ni jambo la muhimu kwa kuwa kila baada ya miaka mitano tunafanya uchaguzi lakini hatupati kiongozi bora, Kama miswada inayopelekwa bungeni ikisimama namna hiyo bado tuna kazi kubwa tunahitaji miswada itakayotupa tume bora," amesema Mwenyekiti huyo wa Jukata.

Kwa upande wa Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Katibu Mkuu

John Mnyika, amesema ipo haja ya kupeleka mswada wa marekebisho ya katiba katika Bunge litakaloanza Januari 2024.

Mnyika anaamini kuwa Tanzania inahitaji kuwa na uchaguzi huru na wa haki, na kwamba ili iwe hivyo, anapendekeza uwepo wa tume huru ya uchaguzi kwa kuwa mchakato wa Tanzania kupata katiba mpya kabla ya uchaguzi, umeshachelewa.

"Serikali inapaswa kupeleka mswada bungeni wa marekiebisho ya sheria ya mwaka 1977, bila kushughulikia katiba kutapelekea kuwa na miswada yenye mapungufu ikiwemo chaguzi za serikali za mitaa kuendelea kusimamiwa na Tamisemi badala ya tume huru," amesema Mnyika.