Mabweni mawili shule ya Green Valley yateketea moto
Mabweni ya Shule ya Sekondari ya Green Valley yaliyoteketea kwa moto
Arusha. Mabweni mawili ya Shule ya Sekondari ya mchepuo wa Kiingereza Green Valley iliyopo Sombetini jijini Arusha yameteketea kwa moto na kusababisha hasara ya vitu vya wanafunzi na mali za shule hiyo.
Moto huo umetokea leo Jumanne Aprili 11, 2023 kuanzia saa nne asubuhi wakati wanafunzi walikuwa darasani.
Akizungumza na Mwananchi mkurugenzi wa shule hiyo, Yahaya Njarita amesema moto huo ulianza saa nne asubuhi katika moja ya bweni ambapo anadai uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha moto huo ni itirafu ya umeme.
"Watoto wachache ambao walikuwa wameripoti shule walikuwa darasani wakati moto ukiwaka na hivyo kusababisha kuungua kwa vitanda, magodoro, nguo na vifaa vingine vya wanafunzi.
"Hasara imepatikana lakini jambo la kheri ni kuwa hakuna mwanafunzi ambaye amedhurika kutokana na moto huu uliounguza mabweni mawili kati ya matano" amesema.
Kamanda wa Mkoa wa Arusha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Osward Mwanjejele amesema jeshi hilo lilipokea taarifa ya moto huo na kufika eneo la tukio wakati moto ukiendelea kuwaka.
"Tulifanikiwa kuzima moto na kuokoa chumba kimoja huku vyumba viwili vikiteketea hii ni kutokana na msongamano ya nyumba na kutokuwa na sehemu ya kupita gari za kuzima moto kirahisi upande wa nyuma"amesema
Baadhi ya majirani katika eneo hilo, Rehema Isaya ameeleza moto huo, ulikuwa mkubwa na kama kusingepatikana msaada wa kikosi cha zima moto ungeleta maafa makubwa sio katika Shule pekee pia hata katika nyumba za jirani.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Justin Masejo amesema katika tukio hilo hakuna majeruhi na uchunguzi unaendelea.