Machinga wataka kamati ndogo kutatua migogoro

Muktasari:

  • Wakati agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapanga machinga katika maeneo rasmi likiwa halitekelezwa katika baadhi ya mikoa, Makamu Mwenyekiti wa Machinga Christian Msumari ametoa ushauri ili kulitekeleza bila migogoro.

Dodoma. Machinga wameshauri Serikali kuunda kamati ndogo itakayowashirikisha wao na wadau lengo likiwa ni kushughulikia migogoro na upangaji wa wafanyabiashara.

 Hatua hiyo imekuja huku katika maeneo mbalimbali ikiripotiwa migogoro kati ya Machinga na halmashauri wakati wa kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Hayo yamesemwa Jumatatu Juni 5, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa Machinga mkoani hapa, Christian Msumari wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya mazingira duniani yaliyofanyika kwenye Soko la Kisasa la Machinga jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

 “Sisi Wamachinga wa Dodoma tunapenda kuona wamachinga wote wanatulia kama sisi tulivyotulia, hivyo ni vyema Serikali ikaona namna ya kuunda kamati ndogo itakayohusishwa na suala la upangaji wa Machinga nchi nzima na utatuzi wa migogoro ya Machinga kama sisi tulivyofanya Dodoma,”amesema.

Msumari ameshauri kamati hiyo ihusishe wadau na machinga wa Dodoma ambao wamehusika katika zoezi la upangaji wa Machinga ili wawe washauri wazuri katika upangaji wa wafanyabiashara hao.

Aidha, Msumari ameiomba Serikali kutengeneza lami katika eneo la mbele na nyuma ambalo ni hatari kwa afya za wafanyabiashara na watumiaji wa soko hilo la Machinga kutokana na vumbi.

“Pia tunaomba tusaidiwe mitambo ya umeme wa jua ili kusudi kutuwezesha kupata umeme wa uhakika katika soko letu na kuipunguzia Serikali na wamachinga gharama ya umeme inayolipwa kila siku,”amesema.

Ameomba kuwekewa taa katika maeneo ya nyuma ya soko ambayo yamekuwa siyo rafiki nyakati za usiku na makinga mvua na jua pembeni mwa soko hilo.

Akijibu Dk Mpango amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru kuyafanyia kazi vumbi lililopo, kuwawekea vikinga jua na mvua kwenye soko hilo.

Pia amemtaka kuzungumza na Waziri wa Nishati, January Makamba kuangalia namna atakavyowasaidia kuweka umeme wa jua.

“Uniachie hili la uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo wadogo, wamesema nilikuwa waziri wao wa fedha achene niende nalo nikapige bongo kidogo basi nitaishauri mamlaka ipasavyo tuone tunachoweza kufanya,” amesema.