Madai mawaziri kumtukana Rais yaibua makundi manne

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda

Muktasari:

  • Ni ile anayowatuhumu watu mbalimbali wakiwemo mawaziri kuwatumia watu kumtukana mitandaoni Rais Sami Suluhu Hassan. Wanaccm, wasomi wa kada tofauti wameichambua kwa kina kauli hiyo

Dar es Salaam. Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda juu ya uwepo wa watu wakiwemo mawaziri wanaotuma watu kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan imezua mjadala huku ikigawa mtazamo wa Watanzania katika makundi manne.

Katika makundi hayo, wapo wanaoitazama kauli hiyo kama taarifa nyeti na haipaswi kupuuzwa na vyombo vya ulinzi na usalama, lakini wengine wanamkosoa aliyeitoa kwa hoja kuwa, jukwaa alilolitumia si sahihi kutoa taarifa hiyo.

Kundi lingine linahoji iwapo Makonda ana mamlaka ya kisheria ya kutoa taarifa hiyo, kadhalika wapo waliokwenda mbali zaidi wakisema tuhuma zilizotolewa na mkuu huyo wa mkoa dhidi ya mawaziri zinaliweka baraza la mawaziri katika mashaka.

Mzizi wa mitazamo hiyo ni kilichosemwa na Makonda Aprili 12, 2024, alipopewa fursa kutoa salamu za mkoa katika hafla ya kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Hayati Edward Sokoine mkoani Arusha. Sokoine alifariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984, mkoani Morogoro akitokea Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, mwanasiasa huyo alitumia jukwaa hilo, kumweleza Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi juu ya uwepo wa watu wakiwemo mawaziri wanaolipa na kutuma watu wamtukane Rais mitandaoni.

“Nitumie fursa hii kuwaambia, hasa kaka zangu mnaotuma watu na kulipa kumchokoza mama yangu, ninawajua na mimi mnanijua, narudia, hasa kaka zangu mnaotuma na kulipa watu kumchokoza mama yangu Samia, mnanijua na ninyi nawajua,” alisema Makonda.

Hakuishia hapo, mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kuweka hadharani majina ya watu hao iwapo vitendo vya matusi dhidi ya Rais Samia visingekoma kuanzia siku hiyo.

“Na leo (Aprili 12) nataka iwe mwisho kutuma watu wao wanaokutukana kwenye mitandao ya kijamii, Jumatatu (kesho) ikiendelea nakutajia majina, wengine ni mawaziri,” alisema.

Kauli na ahadi hiyo ya Makonda, imezua mjadala katika mitandao ya kijamii, wakiwemo wanaomuunga mkono kwa kutoa ahadi za kumlinda Rais Samia dhidi ya watu hao, huku wengine wakimpinga.

Kauli hiyo ya Makonda inafanana na ile aliyoitoa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, kuchapisha picha ya Rais akiwa pamoja naye na kuandika maneno ya kupongeza kazi anayoifanya na kuahidi kumlinda.

Katika chapisho lake la leo Jumapili, Aprili 14, 2024, Dk Nemba ameandika: “Hawakujua utafanya mambo makubwa yote haya, umekamilisha miradi hata iliyoshindikana, umetekeleza miradi kila kata ya nchi hii, umewapa uhuru raia, vyombo vya habari na online media zote za kijamii.

“Unawasomesha watoto wao chekechea mpaka vyuo vikuu, barabara kila kijiji, sekta za uzalishaji zote umeziongezea fedha, umefufua uchumi, umeifungua nchi, umejijengea heshima Duniani kote,” ameandika.

Kulingana na chapisho lake hilo, pamoja na yote yaliyofanywa na mkuu huyo wa nchi, watu hao hawakutaka kuyaona na kwamba wanafanya hivyo kwa makusudi.

“Lakini, hawajataka kuona mazuri yote haya na mengine, sio kwa bahati mbaya, tulijua kuwa kutakuwepo na njama za kukuchafua sana mwaka 2024 na 2025, Tunajua kwenye mikakati yao bado watakuja na mengine ya uongouongo hivi hivi.

“Hatutakubali kuyumbishwa, tutapambana na wanaotumwa na wanaowatuma,” ameandika katika chapisho lake hilo.

Chapisho la Dk Mwigulu ni kama lilikoleza mjadala huo mitandaoni kwa washiriki kuendelea kuhoji kipi kinaendelea ndani ya wasaidizi wa Rais.


@DrCyrilo alisema: “Mwanzoni nilijua tu ni mzaha wa Makonda kumbe ni siriaz hivi. Nani anawatuma watu kumtukana Rais wetu.”

@AwesiAlly

“Si muwataje wanaotumwa na wanao tuma ili tuwashughulikie sisi wananchi kwanza!.”


Taarifa isipuuzwe

Kwa mtazamo wa Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde taarifa iliyotolewa na Makonda haipaswi kupuuzwa hasa na vyombo vya ulinzi na usalama.

"Nina uhakika vyombo vimesikia na ulivyoona Rais alivyoipokea hiyo taarifa haikumshtua sana kwa sababu anayesemwa vibaya ni Rais na Rais ni taasisi sio Rais Samia. Kwa hiyo kwa sababu taasisi ndio inasemwa vibaya natarajia vyombo vitachukua hatua za haraka," amesema.

Hata hivyo, mbunge huyo amesema uhakika wa uwepo wa mawaziri wanaofanya hivyo au kutokuwepo kwao, utatokana na uchunguzi.

"Kwa hiyo kama mjumbe wa NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM) na mbunge ninavitaka vyombo vya dola kuchunguza jambo hilo kwa sababu imetolewa na mtu mzito ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha na vile vile ni mteule wa Rais," amesema.

Kauli hiyo ya Makonda imekuwa vigumu kuzungumziwa na mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustino Vuma aliyesema mkuu huyo wa mkoa ndiye anayepaswa kueleza zaidi.

Pamoja na kujiweka kando huko, mbunge huyo alilaani vitendo vinavyoendelea katika mitandao ya kijamii dhidi ya Rais Samia.

Hata hivyo, alihusisha vitendo hivyo na rasharasha za kuelekea uchaguzi, nyakati ambazo amesema aghalabu fitina hushamiri.

"Sisi ambao tumeshuhudia mambo haya mazuri hatuwezi kukubali na natoa rai kwa vijana wenzangu lazima tusimame imara na Rais wetu tumtie moyo lakini tuwaambie kuwa hao wanaomtukana hawawezi kumfifisha zaidi wanazidi kimng’arisha.

“Na Rais tumtie moyo sisi watanzania tuko nyuma yake, hao wahuni wachache wanaojaribu kumchafua sisi tutadeal (tutashughulika) nao," amesema.

Haikutolewa eneo sahihi

Lakini wapo wanaokosoa hatua ya Makonda kutumia jukwaa hilo kutoa taarifa hiyo, wakisema hapakuwa mahala sahihi kuzungumzwa hayo kama inavyofafanuliwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karambo mkoani Rukwa, Vitus Nandi.

"Unaposema jambo uwe na uhakika, huenda mwenzetu ana uhakika, lakini sio pale hadharani kwa sababu CCM tuna utaratibu wetu. Hali hii itasababisha athari ndani ya CCM ikiwamo kuwepo kwa makundi ya baadhi ya watu.

"Angefikisha ujumbe kimyakimya maana hii itampunguzia uaminifu, ingawa ametumia haki yake ya kusema ukweli daima, lakini sio kwa njia aliyoitumia," amesema, mwenyekiti wa CCM wilayani Kalambo mkoani Rukwa

Wakati Nandi akieleza hayo, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa katika Mkoa huo, Yasin Ismail amesema kulipaswa kutafutwa njia mbadala ya kufikisha taarifa badala ya kumwaga mchele hadharani.

Kufanya hivyo, amesema kumewapa ajenda wanasiasa wa vyama vya upinzani.

"Mwenezi wa zamani wa CCM naye ni binadamu, inawezekana alikuwa na nia njema lakini ulimi ulimteleza kwa kufikisha ujumbe wake haraka kwa njia ile. Inawezekana ana ushahidi wa kutosha kwa sababu ana uzoefu kwenye uongozi," alisema Ismail.

Hoja za makada hao, zinawekewa msisitizo na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, (THRDC), Onesmo Olengurumwa aliyesema zilipaswa kutumika taratibu nyingine kutoa taarifa hiyo na si mbele ya watu wengine.

Katika kauli yake hiyo amesema taarifa hizo zilipaswa kutolewa ndani kwa ndani kwa kuwa zina hatari ya kusababisha mgawanyiko kwa viongozi.

“Mkanganyiko huu unaweza kuchelewa shughuli mbalimbali za kimaendeleo, badala ya viongozi kushirikiana kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo wanakuwa na migongano,” amesema Olengurumwa


Ana mamlaka ya kusema hilo?

Kauli hiyo imeibua hoja juu ya Makonda kuwa na mamlaka ya kuitoa, kama inavyoelezwa na Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Luisulie.

Amesema mamlaka ya kutoa taarifa kama hiyo ni ya vyombo vya ulinzi na usalama.

“Lakini upande mwingine kauli ile inaleta mgawanyiko mkubwa ndani ya Serikali kuwa sasa watu watakuwa wanatuhumiana, mambo mengine ni kuonyana ndani kwa ndani, jambo hili likija katika macho ya umma huwezi kuzuia tafsiri mbalimbali.”

“Uzuri wa ile kauli inawafumbua mambo mamlaka, inaleta ujumbe kuwa watu wasibweteke kwa sababu Rais na makamu wa Rais, vyombo vya usalama wanapata ujumbe kuwa mambo si mazuri katika maeneo fulani,” amesema Dk Luisulie.

Amesema kauli hiyo pia inajenga kutoaminiana na hata Rais atakuwa na sauti kichwani inayomuambia kuwa kuna watu wanalipa watu ili atukanwe na hata mawaziri watakosa kujiamini.


Baraza mawaziri shakani

Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini amesema tuhuma hizo dhidi ya mawaziri zinaliweka baraza la mawaziri katika shaka.

“Lakini ajabu ni kuwa Makonda anao uwezo wa kumfikia Rais sehemu yoyote, kwanini avumilie Rais aendelee kutukanwa hadi apate wasaa wa kuzungumza mbele ya watu vile. Nini kilimfanya Makonda asichukue hatua mapema hadi azungumze sehemu kama ile,” amesema Selasini.

Naibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo amesema kwa sababu Rais ndiyo mwenyekiti wa baraza la mawaziri kauli ya Makonda inaonyesha Rais Samia hufanya kazi na watu wanaomlia njama.

“Hiyo inatoa picha kuwa umefika muda wa Chama cha Mapinduzi kuondoka madarakani kikae chama kingine kinachoweza kuongoza,” amesema Ayo.

Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Saumu Rashid amesema jambo hilo ni tuhuma na anayepaswa kuzungumzia ni vyombo vya ulinzi na usalama.

“Lakini amesema Makonda ambaye si hata msemaji wa chama halina uzito, Makonda ni vitu vingi anaongea ukichukulia kila kitu kwa uzito wake na kulikuza inaweza kuchangia kuharibu nchi,” alisema Saumu.

Akitoa mtazamo wa kisheria, Wakili Dominic Ndunguru amesema inakuwa vigumu kumtia mtu hatiani juu ya kauli yake ikiwa hakutaja jina la mtu.

“Mtu akisema baadhi ya watu; mtu akisema amshtaki itakuwa ni ngumu kwa sababu hakuna mhusika aliyeguswa sasa kwa kile alichokisema Makonda labda tusubiri mpaka Jumatatu,” alisema Ndunguru.

Amesema wakati mwingine kauli kama hizo zinaweza kuwa za kisiasa kuendana na mazingira ambayo kauli hiyo imetolewa kama njia ya kujinadi.

“Kama mtu wa upinzani lazima ajionyeshe kama upande wa pili hawafanyi vizuri ili wao wapigiwe kura na hata waliopo madarakani vilevile,” amesema Ndunguru.

Inahusishwa na fitina za uchaguzi

Hata hivyo, upo uhusiano wa kile kinachofanywa na watu hao dhidi ya Rais Samia na fitina za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hilo linathibitishwa na kilichoelezwa Aprili 11, mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba siku moja kabla ya Makonda naye kugusia suala hilohilo.

Makamba amesema miongoni mwa nyakati ambazo ndani ya CCM kunashamiri fitina ni pale Uchaguzi Mkuu unapokaribia huku Rais aliyepo madarakani akipaswa kuendelea na muhula wa pili.

Akizungumza mbele ya wananchi wa Kijiji cha Mahezangulu mkoani Tanga, Makamba alisema katika nyakati hizo watu ndani ya chama hicho hufanyiana fitina.

“Kwenye CCM kipindi kikubwa cha kufitiniana huwa ni hiki, tunapokuwa na Rais anayeendelea ambaye anapaswa kuendelea basi kama vile ada kwenye CCM watu kusema unaona huyu bwana.

Hataki huyu aendelee, umeona huyu bwana anazamazama ili aonekane huyu hafai, umeona huyu bwana anatega huyu ashindwe,” alisema Makamba.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alieleza aghalabu fitina hizo hukoma siku ambayo mgombea huyo anayepaswa kuwania urais kwa muhula wa pili anapokwenda kuchukua fomu.

“Kwa hiyo tuendelee kuombeana hii fitina pia isiwe na mashiko kwenye nchi yetu na chama chetu na bahati nzuri muda utafika kwa sababu mwakani itapangwa tarehe, anayechukua fomu anakuwa huyu mmoja, siku hiyohiyo ile fitina imekufa,” alisema.

Katika hotuba yake hiyo, aliweka wazi kuwa, pamoja na fitina zote zinazofanyika, lakini wakati ndiyo unaoamua atakayetwaa wadhifa huo.

Alisisitiza katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani, mgombea pekee atakayegombea nafasi hiyo ni Rais Samia, kama ulivyo utaratibu wa siku zote wa chama hicho.


Kikwete aliwahi kunena

Mbali na Makamba Desemba 8, 2022 katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alidokeza kuhusu fitina kuelekea uchaguzi.

Katika kipindi hicho, Kikwete alisema maneno ya uongo huwa mengi, ikiwamo watakaosema fulani anaungwa mkono na mzee huyu, akisisitiza hayo yote ni upuuzi.

"Utasikia kijana gani atagombea, mzee gani atagombea huo ni upuuzi mtupu, sio kama nawazuia lakini simuoni mwana-CCM atakayechukua fomu kukupinga 2025 labda mambo yaharibike sana kati ya sasa na wakati huu," alisema.

Alimwambia Rais Samia asibabaishwe na maneno, ambayo hata wakati wake (alipokuwa Rais) yalikuwepo.

“Na wengine wanasema sijui waziri gani, kaenda wapi kukusanya pesa waganga njaa. Tulipata sana maneno ya namna hiyo, alikuwa anajiita mwanaharakati, lakini ni uongo mtupu. Nawaomba achene uongo,” alisema.

Mkuu huyo wa nchi mstaafu, aliwataka makada wa chama hicho kuacha uongo kwani unawatengenezea viongozi msongo wa mawazo na kukigawa chama hicho bia sababu.

"Naombeni tuache uongo, mnawatengenezea viongozi wetu msongo wa mawazo, zisizokuwa na msingi kabisa, badala ya kukusanya nguvu zao kujenga chama na kutimiza majukumu yao ya Kikatiba ya kuongoza Taifa wanaanza kuangaikia upuuzi wenu, this is not fare (hii sio sawa)," alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa kwa nguvu.

(Imeandikwa na Juma Issihaka, Aurea Simtoe (Dar), Bakari Kiango (Rukwa), Sharon Sauwa (Dodoma))