Madai ya Katiba yasiwe chanzo cha kugombana

Baadhi ya wananchi wakiwa na bango linaloonyesha umuhimu wa kuwapo kwa Katiba mpya. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Katiba ya Tanzania ilitungwa mwaka 1977 na imeshafanyiwa marekebisho yasiyopungua 14 na ulishafanyika mchakato wa kuandika Katiba mpya mwaka 2014.

By Deogratias Mutungi

Nianze makala hii kwa kutambua umuhimu wa siasa za upinzani ndani ya taifa lolote lile ulimwenguni linalofuata misingi ya demokrasia, haki, sheria na uhuru wa maoni. Siasa za upinzani ni afya bora kwa maendeleo ya watu na uchumi wao.

Upinzani ni nyampara na kiranja wa misingi ya uwajibikaji kwa Serikali na taasisi zake, kuwa mpinzani si jinai wala kosa la kikatiba, dhana ya upinzani chanya haifungamani na nongwa wala fujo za kisiasa, bali agenda na mikakati endelevu na imara kwa dira ya taifa, upinzani komavu ni sawa na mafuta ya upako yang’arishayo uchumi, amani na maendeleo ya watu wake.

Siasa za upinzani ni sawa na mkondo wa maji, kamwe huwezi kuzuia kasi ya maji kwa mkono, wala siasa za upinzani hazizuiliki kwa mtutu wa bunduki, kwa mantiki kuwa ni imani na dhamiri iliyo ndani ya mtu, watu au kikundi chochote kile kilichosajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kama ilivyo kwa vyama vya upinzani, ni vigumu sana kubadili dhamiri ya utashi na imani ya mtu yenye mrengo fulani kisiasa na kiitikadi.

Upinzani ni dhana na falsafa ya upendo na imani juu ya nadharia ya kitu fulani hivyo ni vigumu kuibadilisha imani ya mtu hata kwa vipande vya shilingi au rupia.

Wanasiasa na wanazuoni nguli wanaamini kuwa umuhimu wa siasa zenye mfumo wa upinzani ni sawa na mishipa isukumayo damu hili mapigo ya moyo wa binadamu yaweze kufanya kazi kwa ustadi wa hali ya juu.

Endapo mishipa hiyo itashindwa kufanya kazi basi ndiyo mwanzo wa mauti kwa binadamu, kisiasa ni mauti kwa mifumo ya utawala bora, ombwe la demokrasia na uwajibikaji wa Serikali kwa umma na ndipo udhaifu wa Serikali unapoanzia.

Vyama vya upinzani vinavyotambua wajibu na mantiki ya upinzani ni nini huisaidia Serikali iliyopo madarakani kufanya kazi kwa upeo na ufanisi wa hali ya juu sana, siasa za vyama vya upinzani hujikita katika kutengeneza na kutambulisha agenda hai zinazojikita kusahihisha na kuleta mabadiliko katika mifumo ya utawala ndani ya Serikali iliyopo madarakani.

Chama au vyama vya upinzani vinavyoshiriki kueneza dhamira ya chuki, fujo na kuhamasisha mihemuko ya kuvunja amani ya nchi dhidi ya Serikali iliyopo madarakani ni vyama vyenye itikadi mfu na mfilisi ambavyo hutambulika kama vikundi vya “Wahuni na magenge ya walanguzi yenye nia ovu na wananchi wake.

Kwa sasa hapa Tanzania hoja inayojengwa sana na kuongelewa mara kwa mara ni hoja ya “Katiba Mpya” ukweli upo wazi kuwa neno hilo linasikika sana kuliko neno jingine lolote lile kwa sasa hapa nchini. Je, nani nyampara anayesimamia muktadha wa neno hili kwa sasa?

Bila shaka nyampara mkuu wa hoja hii ni vyama vya siasa na wanaharakati wanaohodhi agenda hii kwa asilimia 80 na asilimia 20 ipo mikononi mwa wananchi wa kawaida, hata hivyo utafiti uliopo kwa sasa ni kuwa hoja hii inaongelewa sana zaidi mitandaoni kuliko mitaani.

Dhana ya Katiba mpya imenoga na kunogeshwa kuliko pengine uhalisia wake ulivyo, mantiki ya ukweli inatuonyesha chumvi iliyozidi kiwango katika dai hili.

Wadai wa Katiba mpya kwa sasa wanaidai ndivyo sivyo, wanaonekana kuvurugwa na kughadhibika kisiasa.

Pengine tutafakari kwa nini hoja hii inachomewa utambi zaidi mitandaoni na si mitaani? Sharti kwanza tutambue uwepo wa makundi mawili.

Kundi la kwanza ni la watu wa mitandaoni, hili kundi ni dogo kitakwimu, lakini lenye mchanganyiko wa watu tofauti, kwa maana wapo wenye utimamu wa akili na wapo wanaofuata upepo bila kujua mantiki na thamani ya Katiba mpya ni nini wala kutofautisha Katiba ya sasa (1977) na hii wanayoijengea hoja kwa sasa, wamekuwa kama bendera maana “bendera hufuata upepo”.

Kundi la pili ni kundi la watu wa mitaani, kundi hili lina muunganiko wa watu wengi sana kitakwimu, “wananchi halisi” ambao kwao Katiba mpya ni agenda isiyopewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa

Kundi hili la wanyonge wanafikiria zaidi ujamaa wa uendeshaji na uzalishaji wa kipato cha kila siku kuliko dai la Katiba mpya ambayo kwao ni takwa la kati kama sio la mwisho kimahitaji.

Wananchi wanahitaji zaidi maisha bora kuliko harakati za Katiba mpya, tunaaminishwa na kupotoshwa vibaya dhidi ya dai hili na wasaka fursa za kisiasa na kimtandao.

Mantiki ya nadharia ya Katiba mpya na maisha bora ni porojo za wanasiasa, uchumi imara na kipato cha watu kuimarika ni matokeo ya uongozi bora wenye kuzingatia demokrasia, sera na misingi ya sheria za nchi.

Unaweza ukawa na Katiba bora na imara kuliko yoyote ile duniani, lakini uwepo wa kiongozi mwenye tabia za Farao na dikteta kama alivyokuwa Adolf Hitler akainajisi katiba na kufanya mambo ya kipuuzi na wananchi wakabaki kimya wakisifu na kuabudu, je, umaskini wa Afrika ni matokeo ya ukosefu wa katiba bora na imara au tatizo ni nini? Tutafakari kwa pamoja.

Andiko hili linatambua sana umuhimu wa katiba mpya na asilani halibezi jitihada za upatikanaji wa katiba mpya zinazofuata utaratibu unaoeleweka unaoweza kutupa katiba bora zaidi itakayodumu kwa kipindi kirefu katika ufanisi wa mustakabhari wa taifa letu, lakini haliungani katu na kundi la wasaka tonge wanaotumia dai la katiba mpya kama fursa ya kujineemesha kiuchumi, kisiasa na kiitikadi.

Kuna watu wanaotumia mlango wa kudai Katiba mpya kama kivuli cha kuichonganisha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan. Watu hawa wanafahamika.

Hata hivyo, ipo wazi kuwa mitandao ya kijamii inaundwa na makundi ya watu maalumu wenye nia na kusudio la kushinikiza kupata kile wanachokihitaji kwa masilahi yao, iwe ni kitaasisi au kwa masilahi ya vyama vya upinzani.

Wapo baadhi wanadai Katiba mpya huku wakitumia lugha za matusi kuhalalisha dai lao, kitendo ambacho Evarist Chahali, maarufu kama “Jasusi” kwenye mtandao wa twitter anakiita “demokrasia ya matusi” ambapo Chahali lawama zote anawatupia vijana na wafuasi wa upinzani.

Je, ni kweli upinzani ndio wenye hoja hii ya Katiba mpya? Mantiki na historia inatuonyesha kuwa dai hili lipo kwa miongo kadhaa kwa sasa, hakuna kundi lolote linaloweza kuitambulisha Katiba mpya kama agenda yao rasmi, si vyama vya upinzani, wanaharakati, viongozi wa dini, chama tawala, wasomi wala wanafunzi wanaoweza kuhodhi agenda hii kama agenda yao kwa asilimia 100, bali hili ni hitaji la Watanzania wote kwa ujumla, tunaweza kusema ni “agenda ya kitaifa”.

Basi kama ni agenda ya kitaifa, rai ya makala hii ni kuviomba vyama vya upinzani kuacha nongwa za uchonganishi baina ya Serikali na wananchi wake juu ya agenda hii ya Katiba mpya, hii ni agenda ya wote.

Wapinzani wasijibinafsishie agenda hii ili ionekane ni yao na kutumia nguvu ili kuhakikisha takwa lao linatimia, ni umajinuni na umamluki kutumia lugha hasi na nguvu zilizopindukia kudai Katiba mpya.

Katiba bora imara na endelevu itapatikana kwa kufuata utaratibu rasmi, sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika, vinginevyo ni ubatili mtupu.


Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa gazeti la Mwananchi.

[email protected] 0717718619