Madaktari bingwa 12 BMH watua Katavi

Baadhi ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa wakiingia Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi kuanza uchunguzi, matibabu na upasuaji kwa wagonjwa. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Madaktari bingwa na wabobezi 12 kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma waanza kutoa huduma za uchunguzi, matibabu na upasuaji Katavi.

Katavi. Timu ya Madaktari bingwa na wabobezi 12 wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa Makao Makuu Dodoma, wameanza kutoa huduma za uchunguzi, matibabu na upasuaji  mkoani Katavi ili kupunguza gharama za wagonjwa kusafirishwa kwenda kupata huduma hizo.

Baada ya kuwasili mkoani Katavi leo Septemba 11, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Daktari Alphonce Chandika amesema wamefanya hivyo ili kutoa huduma na elimu kwa  wananchi waliopo pembezoni.

“Tumeona ni vyema kuwafikia wananchi kuliko kusubiri figo ziharibike ndo waletwe kwetu lakini  ni fursa pia kwa madaktari wa huku kujifunza na kupata ujuzi zaidi,”amesema.

“Wananchi wa mkoa huu na jirani wapate huduma, wazifahamu huduma zinazotolewa, zilizowekezwa na  serikali  inayoongozwa na rais Samia Suluhu Hassan wasiendelee kukaa huku bila kupata matibabu,”amesema Chandika.

Amesema  watafanya uchunguzi na kutoa matibabu kwa magonjwa  ya moyo kwa  watoto wenye viashiria, wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya fahamu, upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.

“Matatizo ya afya ya uzazi, wajawazito wenye changamoto za uzazi, kutokea hedhi mfululizo, vidonda vya tumbo, mfumo wa mkojo, nguvu za kiume na mfumo wa mwanaume,” amesema

“Wagonjwa wa mishipa na ajali ikiwemo wazee wenye maumivu sugu ya magoti na nyonga, upasuaji wa mifupa salama, matatizo ya masikio, pua na koo ikiwa ni pamoja na upasuaji wake,” amesema.

Sanjari na hayo watashughulika na wagonjwa wenye matatizo ya macho na matibabu yake, kisukari, shinikizo la damu na kiharusi pamoja na figo.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi, Daktari Damian Maluba amekiri kuwepo uhaba wa madaktari bingwa na wabobezi ambapo inawalazimu kuwapa wagonjwa  rufaa  kwenda kutibiwa nje ya mkoa.

“Hatuna watalaam wa magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, mifumo ya fahamu, figo na mtalaam wa upande wa upasuaji wa chakula na ini,” amesema.

“Fani zingine unakuta tuna mtalaam mmoja tu hawezi kukidhi kutoa huduma kwa kila anayehitaji, ujio wa madaktari hawa unasaidia wananchi kupata huduma  kuna  uhitaji mkubwa,” amesema Maluba.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Katavi waliofika hospitali ya rufaa kupata huduma hizo, John Herman amesema awali walikabiliwa na changamoto ya kutumia gharama kubwa kusafiri kwenda kupata huduma.

“Nilikuwa nimepewa rufaa ya kwenda Bugando na leo nilikuwa naondoka lakini kuna daktari aliniambia subiri watakuja madaktari bingwa kutoka Mkapa nikasubiri,” amesema.

“Nimefurahi kwa sababu imepunguza gharama ningetumia zaidi ya Sh50, 000 za nauli kwenda Bugando lakini kwa sasa nimetumia Sh2,000 naamini nitachunguzwa na kupatiwa matibabu,”amesema Herman.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi na kupata huduma.

“Ni mafunzo pia kwa watalaamu wetu kuongeza ujuzi, mkiona wanasinzia sinzia tuambieni tuwalazimishe wajifunze, tunafahamu tunayo hospitali ya rufaa, bado haina madaktari bingwa wa kutosha,” amesema Mrindoko.

Huduma hizo zitatolewa  kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 11, 2023 hadi Septemba 15, 2023 ambapo kwa siku ya kwanza pekee  waliojiandikisha kufanyiwa uchunguzi ni watu 150.