Wagonjwa waishukuru Serikali kuwaletea madktari bingwa nchini

Mmoja wa wagonjwa walionufaika na matibabu ya upasuaji yaliyotolewa na jopo la madaktari wa mifupa na nyonga kutoka Los Angeles, Marekani, Victoria Sui (70) akifurahi mara baada ya kupokea zawadi ya khanga kutoka kwa Mratibu wa mpango huo, Lazaro Nyalandu alipomtembelea nyumbani kwake Mkuranga mkoani Pwani.
Muktasari:
- Siku chache baada ya jopo la madaktari bingwa kutoka nchini Marekani kuweka kambi ya upasuaji nyonga na goti katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, wagonjwa waliopewa matibabu hayo wameishukuru Serikali kwa kuwezesha wataalamu hao kufika nchini huku wakielezea kuimarika kwa hali zao kiafya.
Dar es Salaam. Wagonjwa walionufaika na matibabu ya upasuaji wa nyonga yaliyotolewa na jopo la madaktari wa mifupa na nyonga kutoka Los Angeles, Marekani Agosti mwaka huu kupitia mpango wa 'Samia Love', wameelezea hali zao baada ya upasuaji huo.
Wakizungumza katika mahojiano maalum leo Jumatatu Septemba 11, 2023, wamesema hali zao zimebadilika kwa kiasi kikubwa mara baada ya upasuaji huo baada ya kuishi katika baiskeli za kutembelea na maumivu makali kwa muda mrefu.
Madaktari hao 60 waliobobea katika tiba ya mifupa, nyonga na mishipa ya fahamu waliwaona na kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa takribani 200 ikiwa ni pamoja na kuwafanyia upasuaji wa nyonga na goti wagonjwa 51 katika Hospitali ya Selian inayomilikiwa na Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania iliyopo jijini Arusha.
"Nilipitia maumivu makali kwa takribani miaka 13 na mguu wangu wa kushoto uliendelelea kuwa mfupi kadri muda ulivyozidi kusonga, nilikata tamaa ya matibabu kwani gharama ilikuwa kubwa," ameelezea Diana Maziku (26).
Diana aliyehitimu shahada ya uhandisi wa umeme Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2022 amesema kwa sasa amesahau maumivu aliyokuwa akiyapata kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kurefushwa mguu wa kushoto ambao ulikua mfupi.
Mratibu wa jopo la madaktari hao walioweka kambi ya siku saba hapa nchini, Lazaro Nyalandu amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na madaktari hao ambao umewezesha wagonjwa hao kufikiwa.
“Tunamshkuru Rais Samia mpango huu mzima uliandaliwa, ulisukumwa na ulisisitizwa naye maana amehusika kwa asilimia 100, ujio wa wale madaktari 60 waliokuja na Serikali yake kupitia mamlaka zote zinazohusika na madawa, madaktari, vifaa tiba na madaktari wa ndani na wataalamu wa Wizara ya Afya, Waziri, Naibu Waziri.
“Pia taasisi zote ambazo zilikuwa muhimu kushiriki ili kufanikisha zoezi hili, zote zimeshiriki kwa uadilifu na upendo mkubwa na kipekee kama ambavyo imekua na tunamshkuru sana kwa kuleta huu mpango wa Samia Love amegusa mioyo na maisha yao na sasa wanatabasamu,” amesema Nyalandu alipowatembelea wagonjwa hao leo.