Madaktari kutoka Cuba kuwanoa wanafunzi chuo kikuu Mwanza

Balozi wa Cuba nchini, Yordenis Despaigne (wapili kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara yake aliyoifanya Chuo Kikuu cha Mwanza. Kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabian.

Muktasari:

  • Wataalamu hao ni wa upasuaji, magonjwa ya watoto na wanawake, mifupa, macho, masikio na pua.

 Mwanza. Wataalamu wabobevu 15 wa magonjwa ya binadamu kutoka nchini Cuba wanatarajia kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kuungana na wenzao wa chuo kikuu kipya cha Mwanza kuwanoa wanafunzi wa fani ya afya.

 Ahadi hiyo imetolewa jijini Mwanza jana, Februari 19, 2024 wakati wa ziara ya Balozi wa Cuba nchini, Yordenis Despaigne baada ya kutembelea chuo hicho ambacho tayari kimedahili wanafunzi 94 wa kozi mbalimbali za afya ikiwemo utabibu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Balozi Despaigne, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabian ametaja wataalamu bingwa wanaotarajiwa kutoka nchini Cuba kuwa ni wa upasuaji, magonjwa ya watoto na wanawake, mifupa, macho, masikio na pua.

Ametaja wataalamu wengine watakaokuja nchini kutokana na maombi yao waliyoyawasilisha kwa Serikali ya Cuba kupitia ofisi ya balozi wao nchini kuwa ni mabingwa wa dawa ikiwemo za usingizi, vipimo vya mionzi na madaktari wa huduma za dharura.

 “Chuo chetu ni kipya na kimeanza kupokea wanafunzi Oktoba, 2023 na tumeanza na wanafunzi 94 wa kozi ya utabibu.

“Tatizo tunalokabiliana nalo ni kupata wataalamu wakiwemo wahadhiri wa kutosheleza kutoka ndani ya nchi, ndio maana tukawasilisha maombi kwenye ubalozi wa Cuba kuomba wataalamu kutoka nchi hiyo ambayo imepiga hatua kwenye eneo la afya ya binadamu,” amesema.

Amesema chuo hicho tayari kimefanikiwa kupata wataalamu kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda wanaoshirikiana na wenzao wa nchini kuwanoa wanafunzi wakati wakisubiri kuwasili kwa wataalamu kutoka nchini Cuba.

Profesa Fabiana amesema chuo hicho pia kinasomesha madaktari 13 katika fani mbalimbali za afya kwa lengo kuongeza idadi ya wahadhiri na wataalamu wabobevu wa ndani.

Akizungumzia mafunzo kwa vitendo, Profesa Fabian amesema uongozi wa chuo unatekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali ambayo pamoja na kutoa huduma kwa umma, pia itatumika kama sehemu ya mafunzo kwa wanafunzi.

‘’Ramani ya ujenzi wa hospitali hiyo itakayokuwa na majengo ya ghorofa 10 tayari imewasilishwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya kibali cha kuanza ujenzi,” amesema Profesa Fabian

Akizungumza baada ya kukagua miundombinu ya chuo hicho kilichopo eneo la Igoma jijini Mwanza, Balozi Despaigne ameahidi kuwa ofisi yake itasaidia kupatikana kwa madaktari bingwa kutoka nchini Cuba ikiwa ni sehemu ya kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Cuba katika nyanja ya maendeleo, hasa sekta ya afya.

Mwanadiplomasia huyo ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Mwanza kwa kuwekeza katika eneo la teknolojia, akisema itasaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa wataalamu kupitia elimu masafa inayotolewa kwa njia ya mtandao.

Catherine Robert, mmoja wa wanafunzi wa fani ya utabibu chuoni hapo amesema ujio wa madaktari hao utatoa fursa kwa wataalamu wa ndani na wanafunzi pia kujifunza mengi kutokana na nchi hiyo.

“Nchi ya Cuba ina wataalamu bingwa na wenye uzoefu mkubwa katika fani ya afya; ujio wao utatunufaisha kitaaluma,” amesema Catherine.

Tanzania ina takriban vyuo vikuu na taasisi za elimu 70 zilizosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinazotoa shahada katika fani na kozi mbalimbali.