Madaktari wafichua mazito kuvuja kwa mitihani

Muktasari:

  • Wadau wa sekta ya afya nchini wamestushwa na taarifa za kuvuja kwa mitihani ya wanafunzi wa programu ya utabibu, huku madaktari wakisema ni janga kwa Taifa kwa kuwa walengwa wanahusika na afya za watu.


Moshi. Wadau wa sekta ya afya nchini wamestushwa na taarifa za kuvuja kwa mitihani ya wanafunzi wa programu ya utabibu, huku madaktari wakisema ni janga kwa Taifa kwa kuwa walengwa wanahusika na afya za watu.

Moja ya majukumu ya maofisa tabibu ambao wengi wako vituo vya afya na zahanati ni kuona, kumchunguza na kutibu wagonjwa na kufanya upasuaji mdogo, na pale inatotokea suala ni zito kwake, hutoa rufaa ngazi ya juu.

Mtaalamu bingwa wa afya ya jamii nchini, Dk Fidelis Owenya alikwenda mbali zaidi na kusema kama wizara isingebaini mapema na wakahitimu na kuingia kwenye soko, matokeo yake ndiyo yale ya kuwa na tabibu kumwandikia mgonjwa dawa A badala ya dawa B.

Mitihani inayodaiwa kuvuja ni ya masomo ya RCH, Counselling, Internal Medicine, Pediatrics, Surgery na Obstetrics na Gynecology, ambayo ilifanyika Agosti 16 hadi 18 mwaka huu, na inaelezwa kuwa ilivuja katika kiwango cha kuvunja rekodi ya uvujaji mitihani.

Inadaiwa mitihani hiyo ilivuja katika kiwango ambacho baadhi ya wanafunzi walitumiana mitihani na muongozo wa usahihishaji (marking scheme) kwa njia ya mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Telegram na barua pepe huku baadhi ya vyuo vikidaiwa kuinunua.

Tayari Wizara ya Afya inayosimamia vyuo vya afya karibu 147 nchini na ambayo ndio ilitunga mitihani kupitia kurugenzi yake ya mafunzo, imeagiza kuzuia kutolewa kwa matokeo hayo ya mitihani ngazi ya NTA 5 ambayo ni ngazi ya diploma.

Oktoba 15, 2021, Wizara kupitia barua yenye kumbukumbu CLB.112/262/01/09 iliwaandikia wakuu wa vyuo vyote vya afya Tanzania Bara ikiwajulisha taarifa ya Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi ( Nacte) kutolewa kwa matokeo ya awali ya mitihani hiyo iliyofanyika Agosti 2021.

“Baraza linapenda kuwafahamisha kuwa matokeo yote ya wanafunzi wa ngazi ya NTA level 5, program ya utabibu yamezuiwa mpaka taarifa ya uchunguzi kutoka Wizara ya Afya itakapokamilisha na kuwasilishwa Nacte kwa ajili ya maamuzi”

Barua hiyo ikaendelea kueleza “Pia matokeo ya wanafunzi 35 kutoka vyuo mbalimbali yamefutwa na wanafunzi hao kusimamishwa kuendelea na masomo (discontinued) kutokana na kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo.

Juzi gazeti hili liliwatafuta Waziri wa Afya Dk Dorothy Gwajima na Katibu mkuu wake, Profesa Abel Makubi, lakini wote hawakukiri wala kukataa kuwapo kwa tatizo hilo, huku wote wakielekeza atafutwe mkurugenzi wa mafunzo, Dk Saitore Laizer.

Hata hivyo, Dk Saitore ambaye ni mkurugenzi wa mafunzo wa Wizara ya Afya, alisita kulizungumzia suala hilo akisema kwa ngazi ya wizara si msemaji, lakini akakiri kulifahamu na taarifa zote walishazipeleka Nacte.

“Naomba mvute subira katika siku moja au mbili hizi mambo yatakuwa clear (wazi) tu,” alisema Dk Saitore alipotafutwa kwa simu na gazeti hili juzi jioni.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta tena Dk Saitore jana kuzungumzia hatua iliyofikiwa, hakupatikana kwa njia ya simu.

Madaktari wadai ni janga

Dk Owenya alisema eneo la kazi la maofisa tabibu ni kuanzia zahanati hadi vituo vya afya, lakini kutokana na uchache wa madaktari, maofisa hao hutibu wagonjwa hadi hospitali za wilaya.

“Kwa hiyo hawa ni watu muhimu sana katika utabibu na ni janga kama watapatikana katika njia za ujanja ujanja, kwa sababu wana deal (shughulika) na miili na afya za watu. Hapa ndio utasikia umepewa dawa A badala ya B,”alisema.

“Kwa ujumla, tabibu anafanya kazi kama daktari na mwananchi wa kawaida anaweza asiwatofautishe. Anafundishwa hadi kufanya minor surgery (upasuaji mdogo). Anafundishwa kubaini hii case (ugonjwa) kama haiwezi basi ampe rufaa.

“Kwa hiyo ukiwa na mtu amepatikana kwa njia za udanganyifu anakuwa na misjudgment (maamuzi potofu), maana hana skills (ujuzi) wa kutosha. Mtu wa aina hii anaweza kutoa dozi ndogo kuliko inayotakiwa na kusababisha usugu,” alieleza.

MAT: Mitihani ni nyara za Serikali

Rais wa Chama cha Madaktari (MAT) Dk Shadrack Mwaibambe alisema chama hicho kinakemea vikali uvujaji wa mitihani, kwani hizo ni nyaraka za Serikali.

“Tunakemea na hatupendi kuwa na wataalamu waliopitia hatua hizo, hatutaki. Mitihani ni miongoni mwa nyakara za siri za Serikali, lazima iheshimiwe na ilindwe kwa hali yoyote ile.

Kipindi cha awamu ya tatu ya uongozi, liliwahi kujitokeza hili nakumbuka lilivaliwa njuga na kusimamisha kazi pamoja na kuwafungulia mashtaka waandamizi waliohusika, nadhani hatua hizo zifuate,” alisema.

Dk Mwaibambe alisema mitihani kuvuja ni kutengeneza wataalamu feki na vifo, kwani ndiyo haohao watakaowatibu Watanzania maeneo mbalimbali nchini.

“Hili halitakiwi lijirudie tena Serikali ina mkono mrefu ichukue hatua iwe fundisho kwa wanafunzi wengine, ambao wanaweza kulega wakiamini watanunua mitihani. Tunahitaji mtu aliyefunzwa, akafundishika na amepimwa kwani sayansi haina ujanja ujanja,” alisema.

Dk Mwaibambe aliongeza kuwa ikiwa mitihani ya matabibu imevuja ni rahisi pia mitihani mingine kuvuja, hivyo wahusika wachukuliwe hatua.

Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya, kwanza alianza kwa kutoa ufafanuzi akisema wauguzi hawahusiki na mitihani iliyovuja.

Alisema kuwa jamii imekuwa ikichanganya wauguzi na matabibu akisema ni kada mbili zenye majukumu tofauti ndani ya sekta ya afya. Pia, alisema kuwa wauguzi walishafanya mitihani na matokeo yao kutoka na kwamba, hakuna suala la kuvuja kwa mitihani kwao.

“Taarifa hii ilileta taharuki kwa wauguzi kwa sababu hawahusiki na wenyewe walishafanya mitihani muda na matokeo kutoka. Limeleta taharuki kwa wanataaluma,” alisema Baluhya.

Naye mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema kuna utitiri wa vyuo vya utabibu nchini, huku vingi vikikosa sifa stahiki, hivyo kuzalisha wahitimu wasio na ubora.

Alisema tatizo wanaloliona kwa sasa ni kuruhusiwa kwa vyuo bila kutazama uhalisia wa utoaji wa huduma, wingi wa wanafunzi na ukosefu wa maeneo ya kufanyia mafunzo kwa vitendo.

Alisema vyuo hivyo vimekuwa vikiwapeleka wanafunzi wao katika hospitali, ambazo madaktari wake wanashindwa kuwasaidia kimafunzo, kwa sababu ya kutingwa na majukumu ya kuwahudumia wagonjwa.

“Wanafunzi wa udaktari madarasa yao ni wagonjwa, sasa unapokuwa na vyuo saba vinapeleka wanafunzi katika hospitali moja, unapokuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko wagonjwa hutarajii mwanafunzi atajifunza kitu,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Issa Mmbaga ambaye kwa sasa ni daktari mstaafu aliyehudumu hospitali za Mawenzi na St Joseph mjini Moshi, alisema tabibu anafanya majukumu ya kutibu hadi kuzalisha isipokuwa matukio magumu.

“Kwa sasa hawa clinical officers (maofisa tabibu) hawatakiwi kuwa kwenye hospitali za wilaya. Wanatakiwa wawe kwenye zahanati na vituo vya afya, wakiona huu ugonjwa ni complicated (umewazidi uwezo) wanampa rufaa mgonjwa,” alisema.

“Ukiniuliza kama kuna uthibitisho wa leakage (kuvuja) hiyo inayosemwa ningeshauri hiyo mitihani ifutwe na wafanye mingine na ni wajibu wa wizara sasa kutafuta kiini cha kuvuja mitihani na nani achukuliwe hatua,” alisisitiza.

Daktari mwingine ambaye anahudumu katika hospitali moja ya Serikali aliyetaka jina lake lisitajwe, alisema kada ya maofisa tabibu ni muhimu hasa kwa sasa ambapo Tanzania ina vituo vingi vya afya na zahanati hadi maeneo ya vijijini.

Mjadala wahamia mitandao ya kijamii

Katika mitandao ya kijamii, suala la kuvuja kwa mitihani hiyo limekuwa gumzo, huku baadhi ya wachangiaji wakidai uvujaji huo ulivunja rekodi kwa kuwa wanafunzi walipata mitihani yote kuanzia sehemu ya kwanza hadi ya mwisho.

“Level (ngazi) 5 mitihani yote ilivuja tena ule mvujo konki. Paper (mitihani) zote from section (sehemu) A hadi mwisho. Ndio tatizo na wizara imejua. ” alidai mchangiaji mmoja.

Mwingine akaandika: “Mie nasikia kwa level 5 semester (mhula) 2 hatari tupu naona sasa hivi mchawi ni kuvuka mwaka wa pili,” alieleza mchangiaji huyo.

Mchangiaji mwingine akaandika: “Hiyo iliyovuja ni level 5 ila uvujaji huu ni wa ajabu sana yaani hakuna chuo hawajapata.”