Madaktari wapendekeza chanjo Uviko kuwa lazima


Muktasari:

  • Katika kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19, waganga wakuu wa mikoa wameishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, iangalie uwezekano wa kuifanya chanjo ya ugonjwa huo kuwa ya lazima.

Dar es Salaam. Katika kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19, waganga wakuu wa mikoa wameishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, iangalie uwezekano wa kuifanya chanjo ya ugonjwa huo kuwa ya lazima.

Wito huo wameutoa, kufuatia vifo vinavyoendelea kuwakumba baadhi ya wataalamu wa afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa wagonjwa, tangu ugonjwa huo uingie nchini Machi 2020.

Akisoma risala katika ufunguzi wa kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma, Katibu wa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, Dk Japhet Simeo, alisema tangu kuanza kwa janga hilo, nchi imepoteza wataalamu muhimu wa afya waliokuwa mstari wa mbele kuwahudumia wagonjwa wa Uviko-19.

“Kutokana na umuhimu wa chanjo katika kukabiliana na Uviko-19 tunashauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, iangalie uwezekano wa kuifanya chanjo hii kuwa ya lazima kwa watu wote wenye vigezo vya kuchanjwa” alisema.

Dk Simeo ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, aliomba halmashauri ziwezeshwe kifedha ili ziweze kuwa na ufanisi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipozungumza na Mwananchi alisema kama nchi bado haijafikia hatua ya kufanya chanjo kuwa lazima, na kwa sasa uchanjaji utaendelelea kuwa suala la hiari.

“Ili kufanya watu wengi zaidi wapate chanjo, tumekuja na mpango mpya wa jamii shirikishi na rahisi kwa wananchi kupata chanjo. Mpango umelenga kuhamasisha upataji chanjo kwa ngazi zote katika jamii,” alisema Profesa Makubi.

Kwa mujibu wa takwimu, hadi Septemba 12, mwaka huu, Watanzania waliochanjwa walikuwa 345,000, kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa mbalimbali za matukio ya Taifa hivi karibuni.

Alisema ili kuhamasisha watu wengi zaidi kuchanja, Serikali inajiandaa kuzindua chanjo ya Uviko-19 inayokwenda kugusa makundi ambayo hayakuwa yakifikika kwa urahisi.

Ulazima wa chanjo

Suala la ulazima wa chanjo liliwahi pia kuzungumziwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, lakini baadhi ya wasomi na wanasiasa walikuwa na mtazamo tofauti. Wapo waliopinga na kukubali maoni hayo.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan kwa nyakati tofauti katika hotuba zake, amekuwa akisisitiza kuwa suala la wananchi kupata chanjo litakuwa ni hiari na sio lazima.

Dominic Ndunguru ambaye ni mwanasheria, alisema hajawahi kuona sheria inayoweza kufanya chanjo kuwa lazima, huku akibainisha kuwa labda kama itatungwa sheria ya aina hiyo.

Lakini kabla ya kufanya hivyo alitoa ushauri kuwa ni lazima wajiulize ugonjwa huo umeathiri watu kwa kiasi gani, kabla ya kuwalazimisha kupata chanjo.

“Badala ya kulazimisha wangetumia njia za nyuma ambazo zilionekana kuzaa matunda na watu hawakuathiriwa sana na virusi hivi, ikiwamo kuondoa watu hofu na matumizi ya dawa za asili,” alisema Ndunguru.

Alisema chanjo kuwa lazima ni kama kutangaza biashara za watu (wazalishaji chanjo) badala ya kuhamasisha wataalamu wa ndani kuzalisha za kwao.

Msikie na huyu

Mtaalamu wa afya ya jamii ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini alisema katika Sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009 hakuna kipengele kinachoonyesha kuwa kitu kinaweza kulazimishwa kwa wananchi wote.

Alisema lakini sheria hiyo imeacha wazi mazingira wezeshi ya kulazimisha jambo fulani kufanyika kuzuia uwezekano wa kuambukizana magonjwa au mazingira ya kulazimisha jambo fulani lifanyike.

“Inaweza kuwa lazima lakini si kwa sheria hii, lakini pia bado unahitajika utafiti sana katika hili, nchi zilizoendelea tu hazijawahi kufanya ulazima na ndiyo ambazo zina vifaa vyote vya kutunzia chanjo hizi na zinatengeneza,” alisema.

Aliongeza; “Chanjo ni kitu kinachokaa ndani ya mtu, haiwezi kulazimishwa ila nchi inaweza kuweka vizuizi katika upatikanaji wa baadhi ya huduma kama mtu akiamua kusema hospitalini kwangu nataka watu waliochanjwa tu au waliovaa barakoa.’’

Akifafanua mazingira yaliyoachwa na sheria yanayoweza kulazimisha jambo kufanyika, alitolea mfano katika udhibiti wa ugonjwa unapotokea katika eneo.

“Kama kikitokea kipindupindu eneo fulani, watasema labda watu wote lazima mnawe mikono kuzuia kuambukizana, ikithibitika hujanawa utashtakiwa kwa kuhatarisha afya ya jamii lakini si kosa jinai kwamba utafungwa,”alieleza mtaalamu huyo.