Madanguro 700 yavunjwa Dar
Muktasari:
- Licha ya wadau mbalimbali kupinga utaratibu uliotumika kuwakamata watu wanaodaiwa kuendesha na kumiliki madanguro ya ukahaba, Serikali imesema imefanikiwa kuyavunja zaidi 700.
Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umevunja madanguro 700 ikiwa ni kupambana na mmomonyoko wa maadili na maambukizi ya magonjwa ya ngono.
Madanguro hayo yameondolewa kufuatia operesheni maalum, iliyofanywa na timu ya mkoa iliyolenga kutokomeza madanguro na biashara ya ukahaba jijini Dar es Salaam iliyoanza Oktoba na Novemba 2023.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba wakati akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP).
Komba amesema operesheni hiyo maalum iliyoanzia Wilaya ya Kinondoni na Ubungo wamefanikiwa kuondoa idadi kubwa ya makahaba ambao waliweka kambi maeneo mbalimbali.
"Tumekuwa na operesheni ya kupambana na biashara ya ukahaba, tukiwa na Mkuu wa Mkoa tulienda Kinondoni, jumla ya madanguro 550 yamefikiwa, Ubungo madanguro 150 yakiwemo ya Kata ya Manzese na Mbezi Luis yamefikiwa hivyo tumefanikiwa kuyaondoa," amesema Komba
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaoongoza kuwa na watu wengi hivyo kuwa katika hatari ya mwingiliano wa watu wenye tabia na hulka tofauti.
"Tupo tayari kuendelea kupambana na kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya zinaa hasa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa kupambana na kuhakikisha tunaondoa madanguro yote yaliyopo katika mkoa huu, kazi inaendelea," amesema.
Hata hivyo, amesema mapambano hayo pia yanalenga kuleta maadili miongoni mwa jamii na kwamba mpango huo pia unawafikia wanafunzi wa vyuo vikuu kwani ni muhimu katika kuhakikisha wanapewa elimu ili kujiepusha na maambukizi," amesema
Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Charles Segoe-Moses amepongeza juhudi hizo na kutaka elimu zaidi itolewe kwa jamii namna ya kuepuka maambukizi, waviu kutumia dawa kwa usahihi na kuhakikisha wanapata matibabu sahihi.
Wakati kukiwa na harakati hizo, maambukizi ya vvu bado yameendelea kuongeza nchini ambapo tafiti za mwaka 2020 zinaonyesha maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima miaka 15 na zaidi yalikuwa 68,000.
Novemba 3, 2023, Chalamila alitoa siku tano kwa wamiliki wa madanguro akiwataka kuyavunja wenyewe na wasipofanya hivyo angetaifisha nyumba zilizohusika.
Pia, aliziagiza baa ambazo nje kuna biashara za ngono zinafanyika akiwataka wamiliki kuwaondoa watu hao kabla hajafanya uamuzi wa kuzifungia.
Baada ya uaamuzi huo, baadhi ya wadau walikosoa mbinu zinazotumika na mkoa katika kupambana na biashara hiyo wakitaka waangalie mzizi wa tatizo hilo badala ya kuwakabili wahusika wa vitendo hivyo.
Walisema ni muhimu kuzikabili sababu zilizowafanya wajiingize katika biashara hizo na si kuwakabili wahusika wakisisitiza utafiti ni jambo la msingi kabla ya oparesheni.
Jana Alhamisi, Baraza la Madiwani Manispaa ya Kinondoni lilikubaaliaba kuendelea na operesheni ya kutokomeza madanguro ambayo yamekuwa yakiharibu vijana wadogo wakike kwa wakiume.
Akizungumza katika Baraza la Madiwani, Meya wa Manispaa hiyo Songoro Mnyonge alisema kwa mara ya kwanza wamefanikiwa baada ya kuungana na kuwa kitu kimoja.
"Tumefanikiwa kwa mara ya kwanza Mwananyamala kulikuwa na madanguro 155 yote tumeyapiga chini, tulikuwa na danguro maarufu tangu miaka ya 1947 la uwanja wa fisi lililokuwa limewashinda watu nalo tumelipiga chini," alisema Songoro
Akitaja idadi yake alisema jumla ya madanguro 505 kwenye manispaa hiyo wamefanikiwa kuyasambaratisha na kubakiza danguro moja lililopo Msasani hivyo wanajiandaa kwaajili ya Operesheni hiyo siku za karibuni.
Aidha Songoro alisema ni lazima kuitengeneza Kinondoni na kuweka bishara zinazokubalika na sio biashara ambayo inatweza utu wa mwanadamu.
"Biashara kama hiyo haiwezi kukubalika ifanyike mahali popote, kama nikufanyika ifanyike kwa faragha sio mambo yanafanyiksa hadharani na kuaharibu watoto wetu," alisema
"Tumethibitisha hadi watoto wa shule za msingi walikuwa wanashiriki biashara hii, sisi kama viongozi hatuwezi kukaa tukasema wale ni wapiga kura wetu hatuwezi kulea wapigakura kwa namna hii lazima tuwabadishe,"alisema Mnyonge.
Kuhusu Operesheni hiyo Songoro alisema itakuwa agenda ya kudumu na hivyo wataiweka kwenye utaratibu katika baraza lijalo, kamati zinzohusika na Afya, mipango miji na Mazingira na Jamii wapitienmaeneo hayo Ili kuona hali ikoje.
"Hayo mambo yao waendelee nayo kwenye hali ya faragha, hakuna mtu anayeingilia faragha ya mtu sisi tunachopambana nacho ni mambo ya ajabu yaliyokuwa yanafanyika," alisema.
Songoro ambaye pia ni Diwani wa Mwananyamala alisema katika Operesheni hiyo miongoni mwa mambo waliyobaini ni pamoja na baadhi ya wasichana chini ya umri wa miaka 18 kusafirishwa na kwenda kutumikishwa kingono.
Alisema kila msichana waliyemhoji, alisafirishwa kuja jijini Dar es Salaam:“Watu wanasema tungetumia njia zingine, mara watabakwa, tusitetee ubakaji hiyo ni hulka ya binadamu. Kule tumekuta mpaka methadone dawa inayotakiwa itolewe hospitali chini ya uangalizi pale kuna chumba kinatoa.”
Alisema asilimia 70 ya wanaotoa ngono kwenye hayo madanguro wanaonekana tayari wameshakata tamaa kwani binadamu halali hawezi kufanya kile kinachofanyika.
Alisema jiji limeamua kwani hata mashine ya kondom iliyokuwa imewekwa pembeni ya madanguro ya Mwananyamala ameiagiza kamati ya afya kwa kushirikiana na mganga mkuu wa mkoa ikaondolewe.
“Pale tumemkuta mama mwenye miaka si chini ya 80 anaendesha danguro tukashangaa, mwingine ni kiongozi wa kidini tuliyetegemea ahubiri mambo mema, anaenda kwenye ibada akirudi nyumbani anakuja kuchukua fedha kwenye danguro lake,” alisema na kuongeza;
“Hawa wanaofanya biashara wanafanya kwa bei rahisi kuanzia Sh1000 hadi Sh2000 kiasi kwamba wateja sasa hata wanafunzi wanapewa hela ya shule wanakwenda kununua hawa makahaba hivyo madanguro yanachangia kuharibu kizazi,” alisema
Upande wa Kinondoni mpaka wiki iliyopita katika madanguro yaliyopo Mwananyamala na Uwanja wa Fisi yalivunjwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saadi Mtambule pamoja na Meya wa Kinondoni.
Baada ya kuvunjwa kwa madanguro hayo, Songoro alisema makahaba hao wamebadilisha namna ya kufanya biashara hiyo na baadhi wameenda kupanga vyumba na wengine wamehamia kwenye madanguro ya maeneo mengine nje ya Kinondoni na wengine wameanza kufanya biashara hiyo usiku kwa kujipanga barabarani.
Songoro alisema wanaomiliki danguro lililobaki Msasani kwa taarifa walizozipata baada ya kuona operesheni imeanza kwenye maeneo mengine, wameanza kubadilisha dizaini kwa kubadilisha milango ‘kuilekeza ndani uani.’
“Haisaidii kwa maana tumeazimia kuondoa madanguro yote, taarifa tunazo.
Hata hivyo, huko nyuma tulidhani kwamba kulikuwa na madanguro ya wanawake pekee, lakini tumekwenda huko tumebaini kuna madanguro hadi ya watoto wa kiume, hatuwezi kukaa na kusema ni wapiga kura wetu hatuwezi kukaa na watu wa aina hiyo.
Gharama yao ya kwanda ipo chini ya Sh5000 lakini iwapo mteja akitaka bila kutumia kondom ni maelewano na ni lazima gharama inakuwa kubwa kulingana na watakavyokubaliana.