Madeni PSSSF yalishtua Bunge

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ina wadai wengi hivyo kushindwa kujiendesha vizuri.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ina wadai wengi hivyo kushindwa kujiendesha vizuri.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka amesema hayo baada ya kuipitia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kwa mwaka 2019/20.

Kwa kifupi, alisema wamebaini shirika hilo ambalo ni muunganiko wa mifuko minne ya hifadhi ya jamii ya GEPF, PPF, LAPF na PSPF bado halijakaa vizuri kutokana na madeni linayodai.

Alisema PSSSF imeweka hatifungani katika Benki ya Maendeleo (TIB) ya Sh86.1 bilioni na dola 111.4 milioni za Marekani, lakini hadi jana benki hiyo imeshindwa kuwalipa. Benki hiyo, alisema haijakaa vizuri hivyo haieleweki kama itaweza kuwalipa ama la.

“Kwa hiyo inalifanya shirika hili lisiweze kufanya kazi zake vizuri, kuna madeni mengine pia. Serikali ilikopa fedha kwa ajili ya kuwekeza katika majengo mbalimbali ikiwamo Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma) ambayo fedha yake haijarejeshwa katika mfuko huo,” alisema.

Pia, Kaboyoka alisema kulikuwa na wafanyakazi waliokuwa wanachangia kabla ya mwaka 1999 ambao michango yao ilifika Sh4.6 trilioni lakini fedha zao zilikuwa hazipelekwi kwenye mfuko wa jamii na Serikali ikaahidi kulipa fedha hizo lakini haijafanya hivyo.

Alisema Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh731.3 bilioni kutokana na mkopo wa ujenzi wa majengo yakiwamo ya Udom na hadi jana deni lilikuwa limebaki Sh231 bilioni.

Alisema kamati inahofu kuwa iwapo Serikali haitolipa madeni hayo itaufanya mfuko uyumbe na tathimini ya kujua uhimilivu wa mfuko kama ilivyoagizwa na Bunge mwaka jana, bado haijafanyika.

“Kamati tumeshindwa kujiridhisha kama shirika hili litaweza kufanya kazi kikamilifu kama ilivyotarajiwa maana Serikali ilivyounganisha mashirika haya yaweze kufanya kazi kwa tija lakini hadi leo hatujaona hilo linatendeka,” alisema.

Pia, alisema waliuagiza mfuko huo kuweka mkakati wa kuhakikisha majengo yao yanapata wapangaji likiwamo la Twin Tower lililopo Dar es Salaam na kufuatilia madeni wanayowadai wapangaji wachache waliopo.

Hivi sasa, alisema mfuko unalipa pensheni za wastaafu kuliko unavyopokea michango kutoka kwa wafanyakazi kutokana na Serikali kutotoa ajira mpya kwa miaka mitano.

Kaboyoka alisema wameuagiza mfuko kupeleka mpango mkakati utakaoonyesha unakua kwa kiasi gani kuweza kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati.

Alisema wameuagiza mfuko huo, hadi mwishoni mwa mwezi ujao wapeleke tathimini ya uhimilivu wao.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga alisema ukaguzi wao umebaini kuna viashiria kuwa Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) nalo halifanyi vizuri kwani lina mtaji hasi wa Sh132 bilioni na madeni makubwa kuliko mtaji wake.

Shirika hilo alisema lina jumla ya mtaji wa Sh243 bilioni lakini lina madeni ya Sh403 bilioni.

“Hicho ni kiashiria kuwa bado shirika haliendi vizuri. Shirika letu linalipa hadi kodi lakini mapato yao hayajaingizwa katika vitabu vyao,” alisema Hasunga.

Alizitaja kampuni inayoshughulika na mkongo wa Taifa na kituo cha takwimu (data center) kwamba kamati imeona haja ya kukaa na Serikali ifafanue kwa nini mapato ya kampuni hizo hayaingizwi katika vitabu vya TTCL kama sheria inavyotaka.

Pia, alisema wamebaini soko la shirika hilo haijakaa sawa ukilinganisha na wapinzani wao wa kibiashara. Ili kulinusuru shirika hilo, Hasunga alisema Serikali inatakiwa kuongeza mtaji ama kuruhusu vyanzo vingine viingize mtaji huo.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mitaa (LAAC) imemuagiza CAG kufanya ukaguzi maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe baada ya kugundua dosari katika hesabu zao.

Aliyataja maeneo ya ukaguzi huo kuwa ni makusanyo yenye udanganyifu (defaulter) wa Sh500 milioni, ujenzi wa soko la kimataifala Kakozi na fedha za mpango wa Elimu wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ambazo zimekaa kwa mwaka mzima bila kutumika.