Madeni ya vikoba yamuondoa uhai

Muktasari:
- Mwanamke mmoja muuza ndizi katika Soko la Mamsera na mkazi wa Kijiji cha Manda Chini, Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro, Patricia Kisela (57) anadaiwa kujiua kwa kujinyonga kutokana na madeni ya Vikoba.
Rombo. Patricia Kisela (57) anadaiwa kujinyonga na kamba ya kufungia ng'ombe huku akiacha ujumbe kuwa kuzidiwa na madeni ndiyo sababu ya kuchukua uamuzi huo.
Mwanamke huyo, mkazi wa Kijiji cha Manda Chini, Tarafa ya Mengwe, Rombo mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kujiua asubuhi ya Desemba mosi, 2023; siku moja baada ya kutoka hospitali alipokuwa akipata matibu kutokana na jaribio la kujiua kwa sumu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema wanalifuatilia suala hilo alilolitaja la kifamilia zaidi kwa kuwa tukio la kujinyonga husababishwa na msongo wa mawazo.
"Mtu anapojinyonga, hili mara nyingi husababishwa na msongo wa mawazo, na ni suala la kifamilia zaidi, lakini mtu akinyongwa hiyo ni jinai, kwa hiyo suala hilo tunalifuatilia ili kujiridhisha kama amejinyonga au amenyongwa,” amesema Kamanda Maigwa.
Inadaiwa kuwa, mama huyo ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi katika Soko la Mamsera, amekuwa akieleza nia ya kutaka kujiua baada ya kuzidiwa na madeni yaliyotokana na kukopa katika vikundi (Vicoba) tofauti, alivyokuwa mwanachama wake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Manda Chini, Ernest Mrosso amesema mwanamke huyo amekuwa akipambana mwenyewe kujitafutia riziki na kwamba wingi wa madeni unaweza kuwa chanzo cha kujitoa uhai.
“Amekuwa akiweka wazi nia ya kutaka kujitoa uhai, na mara kadhaa amejaribu kufanikisha hilo kwa kunywa sumu na mpaka tukio hili linatokea, ni siku moja tangu ametoka hospitali alikokuwa akipata matibabu baada ya jaribio la kujiua kwa kunywa sumu,” amesema kiongozi huyo wa kijiji.
Mroso amesema marehemu alikuwa mwananchama mwenzake katika moja ya Vicoba ambako alikuwa anadaiwa Sh900, 000 na alishindwa kurejesha mkopo huo kwa wakati.
“Kabla ya kujiua alionekana akinunua kamba ya kufungia ng'ombe na kesho yake asubuhi tulipata taarifa ya kwamba amejiua na sisi tulienda eneo la tukio tukakuta ni kweli amejiua kwa kutumia kamba ya kufungia ng'ombe.”
Kwa mujibu wa mwenyeketi huyo, kikundi kingine cha Vicoba kijijini hapo kilikuwa kinamdai Sh200, 000 na kwamba kuna vikundi vingine ambavyo alikuwa hajaresha mikopo yake, licha ya muda muda wa kufanya hivyo kupita.
"Alikuwa na biashara nzuri ya ndizi, lakini inavyoonekana haya madeni yalimvuruga akili na akaamua kufanya maamuzi hayo, ila amechukua uamuzi magumu sana na inaonekana ni baada ya biashara yake kuyumba," amesema.
Bertha Joseph, mmoja wa wafanyabiashara wa Soko la ndizi Mamsera, amesema mama huyo alikuwa ni mtu wa kujituma na mzuri kwenye biashara yake.
"Huyu mama alikuwa mkopaji mzuri na awali alikuwa akirejesha fedha kwa wakati, sasa sijui ni nini ambacho kimemtokea,” amesema Bertha.
“Siku za hivi karibu alikuwa akilalamika kuhusu mikopo anayodaiwa, kwamba ameuza mzigo na watu hawajamlipa fedha zake, hii ilimfanya kuchukua fedha za mkopo kununua mzigo mwingine na fedha hazijarudi.”
Kutokana na mkasa huyo, Bertha amesema mama huyo alianza kulalamika akisema ni bora ajiue kuliko kushuhudia nyumba na mali zake zikiuzwa na kupotea. Na imetokea kweli, juzi Ijumaa amejiua; ni huzuni, alikuwa ni mpambanaji wa siku nyingi."
Mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, wilayani hapo ambapo anatarajiiwa kuzikwa Jumatano nyumbani kwake, Manda Chini.