Madereva masafa marefu kitanzini usafirisaji dawa za kulevya
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo akizungumza kwenye mkutano wa uhamasishaji wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya Mkoa wa Mbeya uliohusisha wadau na vyombo vya dola. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCED) imetangaza kuanzisha ukaguzi kwa madereva wa mabasi ya masafa marefu yanayopita katika mpaka wa Tunduma Mkoa wa Songwe kuelekea nchini Zambia, ili kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya.
Mbeya. Mkoa wa Mbeya umetajwa kuwa lango la uingizaji wa dawa za kulevya zinazopelekwa mataifa mengine kupitia mpaka wa Tunduma mkoani Songwe, huku madereva wa mabasi ya masafa marefu wakitajwa kuhusika.
Hayo yameelezwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo leo Jumatatu Julai 22, 2024 kwenye mkutano wa uhamasishaji wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya uliohusisha vyombo vya dola na wadau wa sekta ya afya ulioandaliwa na Shirika la HJFMRI.
Lyimo amesema lengo la mkutano huo ni kutoa elimu kuhusiana athari za dawa kulevya kwa kushirikisha wadau vyombo vya dola kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti uingizwaji na usafirishaji kupitia mpaka wa Tunduma mkoani Songwe.
"Mbeya ni lango la uingizaji dawa za kulevya, kwani upo jirani na mpaka wa Tunduma, kuna watu wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi jambo ambalo linahitaji ushirikishaji katika udhibiti," amesema.
Amesema hivi karibuni wamefanya oparesheni na mmoja wa watuhumiwa alitoka Jijini Dar es Salaam, alikamatwa Mbeya akisafirisha dawa za kulevya kupeleka Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma.
"Kuna matukio kadhaa, lakini hilo ni mojawapo ambalo linaonyesha ni jinsi gani Mkoa wa Mbeya ulivyo lango la usafirishaji wa dawa za kulevya, ndio maana tumekuja na mikakati ya pamoja ya kudhibiti biashara hiyo katika maeneo ya mipakani na ukaguzi wa mabasi, ili kunusuru kundi la vijana ambao ni taifa la kesho," amesema.
Lyimo amesema Aprili mwaka huu walifanya oparesheni na kubaini kilo 767 za dawa za kulevya sambamba na kemikali bashirifu lita 19,000 zilizokuwa zikitumika kutengeneza dawa za kulevya zenye viashiria aina ya Heroini ambayo ni hatari kwa afya za watumiaji.
"Kuna mtu tulimkamata Jijini Dar es Salaam akiwa na kemikali za kutengeneza dawa za kulevya jamii ya Heroini ambayo alijifunzia katika mataifa ya nje, baada ya Serikali kudhibiti usafirishaji ndani na nje ya nchi sambamba na tani 3.5 za dawa za kulevya zilizokamatwa eneo la Kigamboni," amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mradi wa Shirika la HJFMRI, Nyanda za Juu Kusini, Dk Emmanuel Bahemana amesema wameweka mikakati ya kuwezesha waraibu wa dawa za kulevya kuwa na miradi endelevu sambamba na kupata za Methadone kupitia kliniki iliyopo Hosptali ya Rufaa ya Kanda.
Amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na kudhibiti changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kutoa elimu kwa madereva na makondakta kuepuka kusafirisha dawa za kulevya, kwani wako hatarini kuvipoteza.
"Kama Kamishna Jenerali alivyoelekeza Mbeya ni lango la uingizaji, tutahakisha kwa kushirikiana na vyombo vingine kudhibiti uingizaji na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto sambamba na kutahadharisha wamiliki kutoa elimu kwa madereva, ili kuepuka kutaifishwa," amesema.
Akitoa ushuhuda katika mkutano huo, Atuganile Bahati aliyekuwa mraibu wa dawa za kulevya, ameomba Serikali kudhibiti uingizaji wa dawa hizo, kwani zinachangia kupoteza nguvu kazi kwa Taifa.
Amesema dawa hizo zimemsababishia kupata maambukizi ya Ukimwi kutokana na kujihusisha na ngono isiyo salama kwa lengo la kupata fedha ya kununua dawa.