Wakamatwa Tanzania tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Tanzania (JNIA) Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi limewakamata watu wawili wakiwa na dawa za kulevya kilo7.54 aina ya heroin walizokuwa wakisafirisha katika mji wa Mumbai nchini India.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Tanzania (JNIA) Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi limewakamata watu wawili wakiwa na dawa za kulevya kilo7.54 aina ya heroin walizokuwa wakisafirisha katika mji wa Mumbai nchini India.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Agosti 13, 2021 Kamanda wa Polisi Viwanja vya JNA, Jeremia Shila watuhumiwa hao ni mwanamke (33), na mwanaume (35) wakazi wa Zanzibar (majina yamehifadhiwa) walikamatwa Agosti 11, 2021 saa 15:38 katika uwanja huo wa ndege eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Shila amesema mtuhumiwa mwanamke alikamatwa akiwa na pakiti nne za dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 2.91 alizokuwa amezificha ndani ya begi la kusafiria, na mtuhumiwa mwanaume alikamatwa akiwa na pakiti mbili zenye uzito wa kilo 4.63.
Kamanda Shila amesema watuhumiwa hao walikuwa wanatarajia kusafiri kuelekea Mumbai nchini India.
"Watuhumiwa hawa kila mmoja alikuwa na begi lake ndani ya begi walichana na kuweka pakiti hizo na kisha kulishona tena huku wakiwa wamejaaza nguo mbalimbali ili wasiweze kujulikana kilichomo ndani kutokana na umahiri tuliokuwa nao askari polisi wa JNIA pamoja na vyombo vingine vya ulinzi tulibaini ujanja huo," amesema Shila.
Amesema upelelezi unaendelea mara utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani
Shila ametoa onyo Kali Kwa watu wanaojihusisha na kusafirisha madawa ya kulevya kwani watakamatwa na kuchukuliwa hatua Kali za kisheria.