Madereva wanolewa matumizi ya vilainishi

Baadhi ya madereva kutoka mikoa mbalimbali wakiwa katika mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT). Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Maafisa usafirishaji na madereva 56 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepata mafunzo ya namna bora ya kutumia vipuri na vilainishi kwenye magari ili kupunguza gharama za uendeshaji serikalini.

Mtwara. Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kimeanza kutoa mafunzo kwa maofisa usafirishaji na madereva wa Serikali kutoka mikoa mbalimbali nchini ili waweze kujua namna bora ya kutumia vipuri na vilainishi kwenye magari yao na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Akizungumza Novemba 21, 2023 katika mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza jana, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma na Utafiti wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dk John Mahona amesema Serikali ina magari mengi na matumizi yake ni makubwa, hivyo lazima madereva wajue kupunguza matumizi.

 “Serikali ina magari mengi na hata matumizi ni makubwa, tumeamua kujikita kwenye magari ya Serikali kuwafundisha watumiaji na waendeshaji waweze kutumia vipuri na vilainishi kwa usahihi ili kupunguza matumizi ambayo ni makubwa,” amesema Dk Mahona.

Katika kipindi hiki magari mengi ni ya kisasa na yapo kwenye teknolojia mpya, hivyo tunawafundisha kuyatuma kwa uaminifu na uadilifu ili kupunguza matumizi ya Serikali,” amesema.

Akizungumza katika mafunzo hayo yanayonufaisha maofisa 56, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema mabadiliko ya teknolojia yanabeba vitu vingi kwenye magari hayo, ndiyo maana elimu hiyo ni muhimu kwa madereva hao.

"Elimu hii itawasadia katika mifumo ya kawaida na barabara zetu ambazo kwa sasa tunazo zaidi ya moja, zamani ilikuwa barabara moja na sasa tuna zaidi ya mbili na nyingine ni za juu.

“Kwa mabadiliko haya tunaweza kujikuta ni chanzo cha ajali badala ya kuzizuia. Hawa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na kuzuia ajali na uharibifu wa vyombo vyetu,” amesema Kanali Abbas.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Elina Joanes ambaye ni ofisa usafirishaji Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Mwanza, amesema yatasaidia kupunguza gharama kubwa zilizopo kwenye matumizi ya magari.

"Mafunzo haya yanatupatia mbinu za kuongeza tija katika utendaji na kupunguza gharama za usafirishaji kwa kuwa katika kila shirika tunatumia gharama kubwa kwenye matengenezo na ununuzi wa vilainishi,” amesema Joanes.