Dereva mbaroni akidaiwa kumgonga, kusababisha kifo cha Trafiki

Gari la Shule ya Msingi Nyamuge usajili T.964 BRJ aina ya Mitsubishi lililomgonga Askari wa Usalama Barabarani na kumsababishia kifo.

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia dereva wa gari ya shule ya msingi Nyamuge mkazi wa Nyasaka, Philipo Mhina (52) kwa tuhuma za kumgonga Askari Polisi wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana (WP 3984), Sajenti Stella Alfonce (49) akiwa kazini na kusababisha kifo chake.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia dereva wa gari ya shule ya msingi Nyamuge mkazi wa Nyasaka, Philipo Mhina (52) kwa tuhuma za kumgonga Askari Polisi wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana (WP 3984), Sajenti Stella Alfonce (49) akiwa kazini na kusababisha kifo chake.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo Novemba Mosi, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbroad Mutafungwa amesema ajali hiyo imetokea leo asubuhi saa 12:45 katika Barabara ya Mwanza kuelekea Msoma eneo la Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

"Gari yenye namba za usajili T.964 BRJ aina ya Mitsubishi Rosa mali ya shule ya msingi Nyamuge iliyokuwa inaendeshwa na Philipo Mhina ilisimamishwa na Stella Alfonce aliyekuwa na wenzake katika kituo hicho cha ukaguzi wa magari na baada ya kukaguliwa ilikutwa na kosa,

“Ndipo dereva aliambiwa arudishe gari nyuma kwa ajili ya usalama wa watumiaji wengine wa barabara na wakati akirudi nyuma ndipo alimgonga askari huyo kwa nyuma na kusababisha kifo chake," amesema Mutafungwa

Ametoa wito kwa wananchi na madereva kuendelea kuchukua tahadhari huku wakifuata sheria za usalama barabarani.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi na  madereva kuendelea kuchukua tahadhari, kufuata sheria za usalama barabarani na kujali watumiaji wengine wa barabara ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika yatokanayo na ajali za barabarani," amesema Mutafungwa