Madiwani Kibaha wataka mamlaka huduma za maji

Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo.  Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha wameomba kugawanywa kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), ili wawe na mamlaka itakayohudumia Mkoa wa Pwani peke yake

Kibaha. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani  Pwani,  Mussa Ndomba ameiomba Serikali kuipatia halmashauri hiyo mamlaka ya usimamizi wa huduma za maji na usafi wa mazingira,  ili kuwa na bajeti inayoweza kuhudumia wananchi kikamilifu.

Ndomba amesema hayo leo Jumatano January 31, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri hiyo kililofanyika mjini Kibaha.

"Hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam na Kibaha zinahudumiwa na mamlaka moja  ya maji  (Dawasa)  na asilimia 99 ya miradi inayopitishwa bajeti kubwa  inaelekezwa Dar es Salaam, ila sisi huku Kibaha tunapata miradi michache.

“Hivyo ni bora tuwe na mamlaka yetu ili tutengewe  bajeti yetu wenyewe," amesema.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wamekuwa wakipata adha ya ukosefu wa maji na wateja wapya kuchelewa kuunganishiwa, jambo ambalo limekuwa likisababisha malalamiko mengi.

Kwa upande wake Diwani wa Tumbi, Raymond Chokala amesema kuwa changamoto ya mgao wa maji imekuwa ikisabababisha malalamiko kwa wananchi,  hivyo ni vema mamlaka hiyo ikafanya maboresho ya miundombinu yake ili kumaliza tatizo hilo.

Akizungumzia changamoto hizo, Meneja wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira wa Kibaha, Alpha Ambokile amesema kuwa tatizo la kukosekana kwa huduma ya maji litaisha siku si nyingi,   "hivi sasa tunajenga matanki makubwa yatakayotumika kuhifadhi maji ya akiba ili yanapokatika wananchi waendelee kupata huduma hiyo”. “Hivyo kutakuwa na uhakika wa uwepo wa huduma hiyo muda wote," amesema.