Maduka saba yafungiwa kwa kukaidi bei elekezi ya sukari

Muktasari:

Ufungiaji maduka hayo, umekuja baada ya Tume kufanya operesheni maalumu na kubaini wapo baadhi ya wafanyabiashara wasiozingatia malekezo hayo.

Pemba. Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar imeyafungia maduka saba Kisiwani Pemba baada ya kuuza sukari kinyume cha bei elekezi iliyowekwa na Serikali.

Hatua hiyo imekuja baada ya kufanya operesheni maalumu na kubaini wapo baadhi ya wafanyabiashara wasiozingatia malekezo hayo.

Huu ni mwendelezo wa operesheni ambao ilianza kufanywa na Tume hiyo Unguja, ambako maduka 20 yalifungwa.

Bei elekezi kwa Unguja ni Sh2,650 na Sh2,700 kwa Pemba kwa kilo moja ya sukari.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani Halali ya Biashara Zanzibar, Mohamed Sijamini Mohamed amesema operesheni hiyo ilitokana na malalamiko ya wananchi kwa Serikali kuhusu bidhaa hiyo kuuzwa bei ya juu wakati tayari kuna bei elekezi.

Amesema badala ya Sh2,700 kwa kilo sasa wanauza kwa Sh3,000 hadi Sh4,000 hali iliyoifanya Tume kufanya operesheni maalumu ili kuwabaini wafanyabiashara hao waweze kuwachukulia hatua za kisheria.

"Tumefanya operesheni hii kuwasaka ambao wamekiuka agizo la Serikali, ilitolewa bei elekezi ya bidhaa ya sukari iuzwe kwa bei ya Sh2,700 kwa kilo katika kipindi cha Ramadhani ili kuwapunguzia gharama za bidhaa wananchi lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekaidi, tumewafungia ili wafuate sheria," amesema.

Said Salum Hemed, mfanyabiashara wa bidhaa hiyo, amesema jambo linalowafanya kuuza bei ya juu ni kutokana na gharama walizonunulia kuwa juu.

Alisema wamekuwa wakinunua bidhaa hiyo Sh150,000 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh3,000 kwa kilo, ndiyo maana wanaamua kuuza bei ya juu, iwapo wakiuza kwa bei elekezi inakuwa hasara kwao.

Kwa upande wake Mohamed Juma Mohamed, amesema bei elekezi ilitolewa wakati wameshanunua bidhaa hiyo.

Ameiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria matajiri wanaowauzia wao kwa bei ya juu.

"Hatukatai sisi kuuza bei hiyo, lakini ilikuja tayari tumeshanunua na tukiuza kwa bei hiyo ni hasara, hivyo tunaiomba Serikali iwachukulie hatua na wale wanaotuuzia bei ya juu," amesema.